HATIMAYE Manispaa ya Ilala imekiruhusu Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kutumia viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam
kuzindua kampeni zake.
Wakati hayo yakijiri, mgombea wa chama hicho chini ya mwamvuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, jana alikutana na
wanawake kutoka vyama vinavyounda umoja huo na kuwaambia wana CCM bado
wana nafasi ya kujiunga naye.
KURUHUSIWA JANGWANI
Jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, alisema
viwanja vya Jangwani viliombwa na CCM, kwa ajili ya kufanyia bonanza
pamoja na shughuli nyingine za wabunge na madiwani wao.
Alisema hata hivyo tayari wamewaandikia barua ya kuwaruhusu Ukawa kuendelea na mkutano wao kesho.
“Hatujawakatalia wala kuwazuia Ukawa kufanya mkutano katika viwanja
hivyo, bali walipoomba tuliwaeleza kuwa viwanja hivyo kuna mtu ambaye
tayari ameshalipia.
“Utaratibu umekwishafanyika na tayari tumeandaa barua ya
kuwafahamisha Ukawa kutumia viwanja vya Jangwani kwa ajili ya uzinduzi
wa kampeni zao Jumamosi,” alisema.
Manispaa imesema gharama ya kukodi viwanja hivyo ni Sh 75,000 kwa
siku na CCM ilikodi kwa siku nne kuanzia Agosti 28 hadi 31, lakini
katika kibali chao inaonyesha wameruhusiwa kwa siku mbili tu, Agosti 28
na 29 kwa gharama ya Sh 150,000 badala ya Sh 300,000 kwa siku nne kama
ilivyoainishwa na manispaa hiyo.
Kibali hicho chenye namba 00012339 na risiti namba 380835 iliyotolewa
Agosti 26, mwaka huu, kinaonyesha waliokodi viwanja hivyo kuanzia kesho
ni Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) inayomilikiwa na CCM.
CCM WATAKA UKAWA WAWAANGUKIE
Hata hivyo, pamoja na hatua ya Manispaa ya Ilala, Katibu wa Siasa na
Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba, alisema watawaruhusu
Ukawa kufanya mkutano wao wa uzinduzi wa kampeni kesho endapo wataenda
kwa viongozi wa CCM pamoja na Manispaa ya Ilala kuomba.
Alisema CCM hawana tatizo, wameridhia kutoa viwanja hivyo, lakini
viongozi wa Ukawa wakaonane na viongozi hao ili kibali kilichotolewa na
Manispaa ya Ilala kibadilishwe.
“Hata sisi mwanzoni tuliomba kufanya uzinduzi wetu katika Uwanja wa
Taifa kutokana na kwamba viwanja vya Jangwani vilikuwa havifai kutokana
na uchafu uliokuwepo, lakini tulikataliwa.
“Tulifanya utafiti katika viwanja vya Biafra Kinondoni, Mbagala na
Tanganyika Parkers tukaona kuwa viwanja hivyo havikidhi kutokana na
wingi wa watu.
“Kama chama tuliamua kufanya usafi katika viwanja vya Jangwani kwa
gharama zetu hatimaye tulifanikiwa na tulifuata taratibu zilizowekwa na
manispaa na kulipia viwanja hivyo kwa ajili ya kufanyia shughuli zetu za
burudani, sanaa na kufanya kampeni kwa wabunge na madiwani wetu,”
alisema.
Simba alisema waliomba kibali kihalali katika Manispaa ya Ilala
Agosti 21 na kulipia Agosti 26 mwaka huu kiasi cha Sh 150,000, kwa ajili
ya kuutumia Agosti 28 hadi 31 mwaka huu.
“Uchaguzi una utaratibu na sheria zake, tunawashangaa Ukawa
wanakurupuka na kutaka kufanya mkutano wao Jangwani wakati hawajaomba
uwanja huo, ni vyema kila chama kinapohitaji kufanya shughuli mbalimbali
za kampeni ziandae maeneo yao mapema ili vyama mbalimbali visije
vikakutana na kusabaisha vurugu na uvunjifu wa amani.
“Ukawa wanalalamika ili waonewe huruma, lakini huruma haipo,
kilichopo ni kufuata utaratibu wa sheria ili kuweza kufanikisha malengo
yao,” alisema.
NEC YANENA
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema Chadema kwenye
rasimu yao ya ratiba waliyowasilisha tume, haikusema kuwa itazindulia
kampeni zake kwenye uwanja gani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima, alisema: “Hilo
suala wanapaswa waongee wenyewe wayamalize, nina ratiba hapa ya kampeni
nchi nzima, lakini katika Chadema wameandika watazindua kampeni Agosti
29 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni.”
Wakati Kailima akisema hayo, jana gazeti hili pia lilifanikiwa kuona
barua ya NEC kwenda halmashauri za jiji, manispaa, miji na wilaya,
ikitaka ratiba za uchaguzi zilizoandaliwa na tume zizingatiwe na
kuheshimiwa.
“Pale ambapo mgombea urais, makamu wa rais, akihitaji kutumia kiwanja
katika halmashauri apewe kipaumbele, katika kutumia kiwanja hicho, kwa
ajili ya mikutano ya kampeni bila kujali chama anachotoka mgombea huyo.
“Wagombea wote wahudumiwe kwa usawa bila upendeleo. Mikutamo ya
wagombea ubunge na udiwani isizuie mikutano ya wagombea urais na umakamu
wa rais kufanyika katika viwanja husika,” ilisema sehemu ya barua hiyo
iliyosainiwa na Kailima.
HELKOPTA PALEPALE
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas
Katambi, alisema hawatakubaliana na ukandamizaji wa aina yoyote
inayowafanya wakose haki yao katika kipindi hiki cha uchaguzi.
“Vijana hatutakubaliana na udhalilishaji wowote katika kipindi hiki
cha uchaguzi. Tutatumia usafiri wa helkopta kwa sababu hakuna sheria
ambayo inatuzuia, tutatumia kwa kufuata utaratibu wa sheria.
“Pia kuhusu uwanja wa Jangwani hakuna zuio lolote la maandishi
tulilolipata, na kwa vyovyote vile tutatumia ule uwanja kuzindua mkutano
wetu,” alisema Katambi.
Mwenyekiti huyo wa Bavicha aliwataka vijana wa vyama vya Ukawa kujiandaa kufanya maandamano nchi nzima endapo haki haitatendeka.
Katambi ambaye anagombea ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini
kupitia Chadema, alikumbushia siku alivyotekwa na kuchaniwa fomu zake
ambapo pamoja na kumbaini askari mmoja, lakini hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa.
“Tunachoomba hivi sasa Serikali ituambie kama na yenyewe ni sehemu ya
uchaguzi kwa kupendelea CCM na kukandamiza upinzani…vijana hatutakubali
kufanyika uonevu wa aina yoyote,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Asifiwe George, Aziza Masoud na Elizabeth Hombo
Home
News
Ukawa moto wa kuotea mbali,waliobana uwanja waachia,Lowassa apokelewa kama mfalme na wanawake Millenium Tours.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment