MOTO ulioteketeza nyumba na kuua watu tisa wa familia moja, umeacha
simanzi baada ya kuelezwa kwamba mmoja wa waliopoteza maisha ni bibi
aliyefariki akiwa amekumbatia wajukuu zake watatu na mama aliyemkumbatia
mwanawe.
Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana eneo la Buguruni
Malapa, Ilala jijini Dar es Salaam, baba mwenye nyumba hiyo, Masoud
Mattar, ndiye aliyesalimika kwa sababu alikuwa kazini.
Moto huo unadaiwa kutokea saa 9 usiku wa kuamkia jana na unaelezwa
kusababishwa na hitilafu ya umeme ambayo tangu juzi kuanzia saa 2 usiku
ilikuwa imeanza kutokea kwenye nguzo ya umeme iliyopo nje ya nyumba
hiyo.
MTANZANIA lilishuhudia miili hiyo ikitolewa kwenye nyumba hiyo ikiwa
imeshikana mithili ya watu waliokumbatiana huku wakisali, kuonyesha
kwamba walifariki dunia wakiwa wamekumbatiana.
Baba wa familia hiyo, Mattar, akiwa ameketi chini kwenye viwanja vya
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), aliwaambia waandishi wa habari hana
cha kusema zaidi ya kuomba asionyeshwe miili ya wanafamilia yake hao
kwani na yeye anaweza kufariki.
“Ninachowaomba ndugu zangu mniache nipumzike…sina cha kusema zaidi ya
kuomba nisionyeshwe maiti kwani na mimi naweza kufa, watoto wangu
wamekufa bado wadogo, tena wamekumbatiana,” alisema Mattar huku
akibubujikwa machozi.
Ofisa uhusiano wa hospitali hiyo, John Steven, alisema waliipokea
miili ya watu hao juzi usiku ikiwa imeungana na kuihifadhi kwenye chumba
cha maiti.
“Kwa kweli inasikitisha, watu wale walikuwa wameungua vibaya mno kiasi kwamba ilikuwa tabu kuwatambua kwa haraka,” alisema.
WALIOFARIKI KATIKA TUKIO HILO
Steven aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Samira Ibrahim (42) – mke
wa Mattar na watoto wake Aisha Masoud (17), Ahmad Masoud (15), Abdilhah
Masoud (10) na Ashiraf Masoud (5).
Wengine ni Bimdogo Masoud (72), ambaye ni mama mzazi wa Samira,
msichana wa kazi Samira Haroub (17), Waadhat Swalleh (27) – mtoto wa
kaka yake Samira, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msasani Islamic English
Medium na mwanawe Fahir Fesal (2).
WAFARIKI DUNIA WAKIOMBA MSAADA
Wakati moto huo ukiendelea, MTANZANIA lilishuhudia mama mmoja
akitokea katikati ya moto akiwa amemshika mtoto na kutupa funguo nje
kupitia mlango uliokuwa wazi ili wasamaria wema wafungue mlango wa chuma
uliokuwa umefungwa na kuwaokoa.
Baada ya kurusha funguo hizo nje, mama huyo alirudi ndani kwenye
baadhi ya vyumba ambavyo vilikuwa havijaanza kushika moto kutokana na
eneo hilo la mlango mkubwa kuwa na moto mkali.
Lakini kutokana na moto kuwa mkali, majirani waliokuwa wakihangaika
kutaka kufungua mlango huo, hawakuweza kutumia funguo hizo kuwaokoa
kutokana na kuzidiwa na moto.
Wakati wote huo, sauti zilizokuwa zikisikika kutoka ndani ya nyumba
hiyo zilikuwa zikisema: “Majirani tusaidieni, tunakufa, tusaidieni.”
Wakati juhudi za kutaka kuwaokoa zikiendelea, mtungi wa gesi uliokuwa
ndani ya nyumba hiyo ulilipuka na kung’oa mabati na kisha moto kusambaa
nyumba nzima.
Kitendo hicho kiliwafanya majirani wakimbie kutokana na kishindo cha
mtungi huo na ndipo ulipokuwa mwisho wa kelele kutoka ndani ya nyumba
hiyo.
MLANGO WA CHUMA KIKWAZO
Baadhi ya majirani waliliambia MTANZANIA kuwa, mlango wa chuma
ulioshindikana kufunguliwa, uliwekwa hivi karibuni baada ya wezi kuiba
kwenye nyumba hiyo.
Walisema baada ya kuwekwa mlango huo, familia hiyo ilikuwa haitumii tena na badala yake walikuwa wanatumia wa uani.
ZIMAMOTO
Baada ya kikosi cha Zimamoto na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala kufika
eneo hilo, utaratibu wa kubomoa mlango huo wa chuma ulianza na
kufanikiwa, lakini tayari watu wote walikuwa wamepoteza maisha.
Mmoja wa majirani alilieleza MTANZANIA kuwa juzi jioni aliona wageni
wawili waliofika katika nyumba hiyo wakiwa na mtoto mchanga, ambao
anadhani kuwa nao waliteketea kwa moto huo.
Jirani mwingine, Mbarouk Mohamed, alisema mazingira ya nyumba hiyo
yaliwapa shida watu hao kuweza kujiokoa kwakuwa sehemu ya sebule ilikuwa
jirani na jiko, hivyo moto ulivyopamba walishindwa kujiokoa kwakuwa
ndiyo ilikuwa njia ya wao kupita.
Alisema watu hao walikuwa wamelala katika baadhi ya vyumba vitano
vilivyokuwa nyuma ambapo mlango mkubwa wa kutokea ndio uliokuwa umepamba
moto tayari.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, alisema kamati ya
ulinzi na usalama imepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa na inatoa
pole kwa familia ya marehemu.
Alisema tukio hilo limetokea kwa mapenzi ya Mungu kwakuwa jitihada zilifanyika, lakini ikashindikana kuokoa maisha ya watu hao.
“Mwenyezi Mungu alete subira katika kipindi hiki kigumu ambacho
kimetokea katika familia hii… ila tunachoweza kusema kwa sisi tunaoamini
dini, siku zao zilifika na Mungu awape pumziko kwani hatuna namna
nyingine ya kuongea,” alisema Sadiki.
Alisema kwa taarifa alizozipata ni kuwa familia hiyo siku za hivi
karibuni waliingiliwa na wezi hivyo wakalazimika kufunga mlango mmoja na
kutumia mwingine ambao pia waliweka mlango wa chuma.
Sadiki alisema kutokana na hali hiyo, familia hiyo ilikuwa na mazoea
ya kutumia mlango mmoja tu hali ambayo ilichangia jana kushindwa
kujiokoa kwakuwa mlango mmoja ulikuwa haufunguki.
Alisema kutokana na ukubwa wa tukio hilo, Serikali itachangia sanda pamoja na chakula kwa wafiwa.
“ Tunaelewa mwenzetu (Mattar) alivyopata mshtuko kwa tukio hili, sisi
kama Serikali tutaangalia namna ya kumsaidia ili ajiweke katika hali
nzuri, hata kama ni mfanyakazi tunaamini tukio hili limemuweka katika
hali ngumu,” alisema Sadiki.
KAMISHNA KOVA
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova,
alisema ni vyema jamii inapojenga nyumba na kuweka milango ya chuma
ikaweka pia mlango wa dharura kwa sababu za kiusalama.
Kamishna Kova aliwataka wananchi kujenga mazoea ya kuweka filimbi
ndani ya nyumba zao zitakazowasaidia kupeana taarifa pindi panapotokea
dharura.
NENO LA SHUKRANI
Katibu wa Msikiti wa Ghuram uliopo Buguruni Malapa, Jamalidin Ayoub alisema moto huo ulizimwa saa 10 alfajiri.
Alisema baba wa familia, Mattar, wakati tukio hilo likitokea alikuwa
amekwenda kazini na muda huo alikuwa akirejea na ndipo alipokuta nyumba
imeteketea yote na mali iliyokuwapo pamoja na familia yake.
Kutokana na hali hiyo, katibu huyo alisema walilazimika kumpeleka msikitini kwa ajili ya kumfariji na kuweka mambo sawa.
“Hali ya ndugu yetu ilikuwa mbaya, tulijitahidi sana kumfariji.
Lakini hata hivyo tunaishukuru Serikali pamoja na watu mbalimbali ambao
walijitokeza kumfariji na wananchi wamejitahidi kuchanga zaidi ya Sh
500,000 kwa ajili ya mwenzetu,” alisema.
Hadi MTANZANIA, familia ya marehemu pamoja na kamati ya ulinzi
wakiondoka katika viwanja vya nyumba hiyo iliyopo jirani na kituo cha
mabasi cha Buguruni Malapa saa 5:30 asubuhi, moto ulikuwa ukiendelea
kuwaka, huku kuta zikiendelea kuporomoka hali ambayo iliwafanya polisi
kuweka uzio maalumu ili wananchi wasipate madhara zaidi.
HALI ILIVYOKUWA MUHIMBILI
Miili ya marehemu ilifikishwa hospitali ya Muhimbili jana saa 12
asubuhi na ilipofika saa 7:00 mchana umati wa watu ulikuwa umefurika kwa
ajili ya kutoa salamu za mwisho kwa marehemu hao ambao walikuwa
wanasomewa dua katika msikiti uliopo ndani ya hospitali hiyo.
Katika eneo lililoko karibu na chumba cha kuifadhia maiti kulikuwa na
idadi kubwa ya waombolezaji walioonekana kuwa na nyuso zilizojawa na
huzuni.
“Jamani wenzetu wana msiba mkubwa, watu tisa wote Mwenyezi Mungu
awafanyie wepesi awape faraja maana inatia huzuni,” alisikika mmoja wa
waombolezaji hao akiwaeleza wenzake.
Maiti hizo ziliondoka saa 7:40 mchana baada ya dua na kuelekea katika makaburi ya Kisutu kwa ajili ya mazishi.
Miili hiyo ilipakiwa katika gari lenye namba za usajili T 963 BUJ
Toyota Canter na T 224 BQJ Canter na kufuatiwa na msafara mkubwa
kuelekea makaburi ya Kisutu kwa ajili ya maziko.
MADEREVA NA WANAFUNZI WALONGA
Mwanafunzi Mohamed Nassor wa darasa la sita katika Shule ya Msasani
Islamic English Medium alisema wamepata pigo kutokana na kifo cha
mwalimu wao, Waadhat aliyekuwa anawafundisha kompyuta.
Alisema watamkumbuka mwalimu huyo kwa ucheshi wake pamoja na uchapakazi.
Naye Ally Nassor ambaye ni dereva wa basi la shule hiyo, alisema
watamkumbuka daima mwalimu huyo ambaye wamefanya naye kazi kwa muda wa
miaka sita, kutokana na ucheshi, upole na ukarimu wake.
Alisema mwalimu huyo ambaye alikuwa akiishi maeneo ya Magomeni –
Morocco Hotel, alikwenda Buguruni Malapa kumsalimia bibi yake akiwa na
msichana wake wa kazi, Samira na mtoto wake mdogo, Fahir ambao wote
wamefariki.
Habari hii imeandaliwa na VICTORIA PATRICK (TSJ), CHRISTINA GAULUHANGA, TUNNU NASSOR na VERONICA ROMWALD.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment