CHAMA cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), kimelaani kitendo cha
mwanachama wake ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Lawrence Masha, kunyimwa dhamana mahakamani.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, TLS
imesema mahakama imekuwa na tabia ya kunyima watu haki yao hiyo kwa
kisingizio cha kuhakiki nyaraka za dhamana.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimesema kitaunda tume maalumu ya
kuchunguza uvunjwaji wa taratibu za mahakama unaosababisha watu kukosa
haki za dhamana.
Masha ambaye pia ni wakili, alikamatwa hivi karibuni Kituo cha Polisi
Oysterbay, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, alipokwenda kuwawekea
dhamana vijana waliokamatwa kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria.
Inadaiwa kuwa Masha alitoa lugha ya matusi kwa askari aliowakuta
katika kituo hicho, hivyo naye akakamatwa na kuwekwa mahabusu kabla ya
kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako alinyimwa dhamana na
kupelekwa gereza la Segerea.
Rais wa TLS, Charles Rwechungura, alisema katika taarifa hiyo kuwa
kumekuwa na tabia ya mashtaka huchukua muda mrefu kushughulikiwa na
mshtakiwa anatakiwa abaki rumande akiwa na dhamana yake mfukoni.
“Tunalazimika kueleza hisia zetu kama wanachama wa kundi hili
kutokana na tukio la hivi karibuni la kuomba dhamana kwa mmoja wa
wanachama wetu. TLS inalaani bila kujuta na bila kuomba radhi kwa tabia
hiyo ya aibu ambapo mwanachama wetu Lawrence Masha (Wakili) alifanyiwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu,” alisema Rwechungura.
“Kosa alilokuwa akishtakiwa Masha la kutoa lugha chafu kinyume cha
Kifungu cha 89(1) (a) cha Kanuni ya Adhabu [Cap 16 R.E.2002] linaangukia
katika kundi la makosa madogo yanayotolewa dhamana,” aliongeza
Rwechungura katika tamko hilo.
Alisema kutokana na ukiukwaji huo wa taratibu za mahakama, TLS
itaunda tume maalumu ya kukusanya taarifa ili kukomesha tabia hiyo.
“Tanganyika Law Society itaunda tume maalumu ya kukusanya taarifa za
kutosha iwezekanavyo kwa uvunjifu wa taratibu za mahakama katika utoaji
wa dhamana, ili kuushirikisha mhimili wa mahakama kurejesha hali ya
kawaida,” alisema Rwechungura.
Hata hivyo, alisema TLS haihoji kukamatwa kwa Masha na kama ni
mkosaji au kosa aliloshitakiwa litachukuliwa kwa uzito gani na mahakama,
bali wanacholalamikia ni kitendo chama mahakama kusababisha Masha
kukosa haki yake ya dhamana.
“Wala TLS haihoji masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama kwa
sababu kwa maoni yetu kwa masharti hayo yangesaidia. Tunacholalamikia na
kukosoa ni uhalali na umakini wa mahakama kuacha jukumu lake na
kusababisha Masha kukosa haki yake ya dhamana,” alisema.
Alisema wakati wote TLS imekuwa ikikemea kupitia matukio mbalimbali
vitendo vya wazi vya kudharau mahakama na hasa pale mahakama inajikuta
kwenye mazingira kama hayo.
“Kama wanachama tumeshuhudia mambo tunayoweza kusema yamekuwa
yakirudiwa, yakihusisha mahakama na waendesha mashtaka ya kukataa kutoa
dhamana kwa watuhumiwa wanaofikishwa mahakamani.
Kuna utaratibu mpya ambao haujaandikwa popote umeanzishwa ambapo
mahakama inatoa haki kwa mkono mmoja na kwa mkono mwingine kumrudisha
kwenye mashtaka kwa kisingizio cha kuhakikisha vielelezo,” alisema
Rwechungura.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment