TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema majina ya watu
waliojiandikisha zaidi ya mara moja katika Daftari la Wapigakura,
yamekabidhiwa kwa vyombo vya dola ili taratibu za kisheria zifuatwe
ikiwamo kuwapeleka mahakamani.
Akizungumza katika kituo cha uchakatuaji (maandalizi) wa vitambulisho
vya wapigakura jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa
NEC, Ramadhani Kailima, alisema sheria inawataka watakaotiwa hatihani
kutumikia kifungo au kulipa faini.
Aidha alisema kuwa endapo muhusika atahukumiwa kifungo kuanzia miezi sita atapoteza sifa ya kupiga kura katika uchaguzi ujao.
Mkurugenzi huyo alisema, idadi ya waliojiandikisha zaidi ya mara moja
imefikia 52,780 kutoka 52,000 idadi ambayo ilitangazwa awali.
“Awali tulisema watu wanaojiandikisha zaidi ya mara moja hawataweza
kupiga kura na tutawakamata tu kupitia mfumo wetu, waliofanya hivyo
wajue wamefanya kosa la jinai.
“Hadi leo (jana) asubuhi tumewagundua watu 52,780 waliojiandikisha
zaidi ya mara moja, wengine mara sita na wengine mara saba,” alisema
Kailima.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa uchaguzi, idadi ya watu waliojiandikisha nchi nzima hadi sasa ni milioni 23.7.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya walemavu wa macho wanaodaiwa
kutengwa katika zoezi la kupiga kura, alisema viongozi wa kundi hilo
walifika ofisini hapo Jumanne ya wiki hii kwa lengo la kutafuta njia
sahihi ya kuwasaidia waweze kupiga kura.
“Tumepanga kuwawekea utaratibu wao kuna kamati ambayo imeundwa na
wenyewe watapanga njia nzuri ya kuwawezesha kupiga kura ikiwemo
kutengeneza karatasi maalumu ambazo zitagharimiwa na tume,” alisema
Kailima.
Akizungumzia kuhusu raia wa kigeni waliojiandikisha, Kailima
aliwataka watu hao kuvisalimisha vitambulisho vyao katika ofisi za kata,
wilaya na mikoa kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.
“Mashine ina utaratibu wa kutambua mtu aliyejiandikisha na sio raia
kwa kushirikiana na watu wa uhamiaji kuna watu wamepingwa na mfumo si
raia, nawapa siku saba wakabidhi vitambulisho katika ofisi za serikali,”
alisema Kailima.
Alisema hakuna raia wa kigeni atakayefanikiwa kupiga kura na endapo
NEC itaamua kumfuata mtu aliyejiandikisha na hakustahili atafikishwa
katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Daftari la Wapiga kura Dk. Sisti
Karia aliwatoa hofu wananchi na kusema kuwa hakuna kura haramu
zitakazoongezwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment