Image
Image

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wammwaga KINGUNGE.

Miezi kadhaa baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi na Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kingunge Ngombale Mwiru, kuonyesha wazi kumuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, katika mbio zake za kuusaka urais sasa ameanza kushughulikiwa ndani ya Chama.
Mzee Kingunge sasa amevuliwa wadhifa wake wa ulezi wa UVCCM, hatua inayothibitisha kuwa ni adhabu kutokana na kauli zake dhidi ya Chama kabla na baada ya Lowassa kukatwa jina lake na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kugombea urais kwa niaba ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza na Nipashe jana Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alisema kwa jinsi walivyompima Kingunge wameona hafai tena kuwa kamanda wa UVCCM kutokana na kauli zake na wanakiomba chama kumfuatilia kwa karibu.
Kushughulikiwa kwa Kingunge kumeanza kwa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM, kuazimia kumtema kwa nafasi ya ukamanda mkuu wa UVCCM kuanzia Agosti 15, mwaka huu, kwa kile wanachoeleza ni tabia na mwenendo wake wa hivi karibuni kwenda tofauti na maadili na taratibu za chama hicho.
Kingunge ni mwanasiasa mkongwe ambaye bila kumumunya maneno alikishutumu chama chake na kukitaadharisha juu ya rafu mbalimbali zinazochezwa kuwa zinaweza kukiangamiza chama hicho na kukichimbia shimo.
 Bila woga alijitokeza jijini Arusha wakati Lowassa akitangaza nia na wakati wa mikutano ya kusaka wadhamini wa kuomba kuteueliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho, na kueleza kuwa ni lazima chama kisome alama za nyakati ikiwa ni pamoja na kumweka kada anayekubalika ndani na nje ya chama, kulelewa ndani ya chama kama ilivyo kwa Lowassa na kinahitaji mtu wa namna hiyo ili kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 Baada ya Lowassa kukatwa alijitokeza hadharani na kueleza kuwa kitendo cha kumkata kimeacha kasoro kubwa ndani ya CCM.
Kingunge amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, kipindi cha awamu zote kuanzia ya Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete sambamba na kuwa waziri.
Amewahi kuwa mkuu wa mikoa kadhaa na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Kingunge ambaye alikuwa Naibu Kamanda alipewa nafasi ya Ukamanda mwaka 2008 baada ya kufariki Mzee Rashidi Kawawa. 
 Mapunda alisema maamuzi hayo yalitolewa kutokana na tabia na mwenendo wake wa hivi karibuni kwenda tofauti na maadili na taratibu za CCM.
“Kikao kimetoa mapendekezo kwa vikao vya CCM kuuangalia upya uanachama wake na kuchukua hatua zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
MATAKWA YA KATIBA YA CCM 
Kwa mujibu wa ibara ya 13 (1) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi 1977 toleo la 2012, uanachama wa mwanachama utakwisha (a) kufariki; (b) kujiuzulu mwenyewe (c) kuachishwa kwa mujibu wa Katiba (d) kufukuzwa kwa mujibu wa Katiba (e) kutotimiza masharti ya uanachama (f) kujiunga na chama kinine chochote cha siasa.
KINGUNGE: SINA TAARIFA 
Alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na maamuzi hayo ya UVCCM, Kingunge alisema kwa kifupi:
“Aah wamefanya hivyo! sina taarifa hadi sasa, ndiyo nasikia kutoka kwako.” 
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment