MGOMBEA urais wa Zanzibar wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali
Mohamed Shein amesema katika uchaguzi wa mwaka huu kuwanyoa wapinzani ni
lazima na nywele hazitoota watabaki na vipara.
Aidha, amesema wakati uchumi wa Zanzibar ukiendelea kuwa mzuri, kima cha
chini cha mshahara kitakuwa shilingi 300,000, hivyo wananchi waongeze
ari ya kufanyakazi kwa kujituma.
Alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni zake Kisiwani Pemba jana
na kubainisha kuwa uchumi wa Zanzibar unakuzwa na jitihada za wananchi
kufanya kazi kwa kujituma kitu ambacho kinafanya uchumi kusonga mbele.
Dk Shein alisema kilimo cha tija kitaongeza ajira kwa wananchi wa
Zanzibar kwani hakuna ambaye anaweza kutoa ajira kwa vijana wote bila ya
wao wenyewe kujitoa na kujituma.
“Niliweza kusimamia sekta ya kilimo kwa miaka mitano iliyopita kwa kutoa
mbolea, trekta na vitendea kazi kwa wakulima wa mpunga, pia naahidi
kufanya hivyo kama nikichaguliwa kwa mwaka huu,” alisema mgombea huyo.
Alisema Septemba 13, mwaka huu alipewa Ilani ya CCM na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na kwamba ni lazima kuitangaza
na kutekeleza kama alivyofanya kwa miaka mitano iliyopita.
Mgombea huyo wa urais alisema mwaka huu watawanyoa vipara wapinzani kwa
kutumia wembe ambapo nywele zao hazitoota na itakuwa mwisho wa vyama
hivyo.
“Wapinzani kuwanyoa ni lazima tena safari hii hata nywele hazitoota watabaki na vipara,” alisema Dk Shein.
Alisema alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza aliahidi na kusisitiza
kuhusu amani ambapo aliweza kutuza amani hiyo kwa Zanzibar kwani wote ni
wamoja japo kuna watu wanachochea uvunjifu wa amani pamoja na kutaka
kuweka matabaka ya watu.
Balozi Seif
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif
Ali Idd alisema upinzani usahau kushinda katika chaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, Chama cha Wananchi (CUF),
kikikataa matokeo imekula kwao kwani Dk. Shein ataunda Serikali ya chama
kimoja.
Seif alisema ikitokea kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk. Shein
atamtaka Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Maalim Seif Sharif Hamad kuleta majina matatu badala ya moja alilolileta
mwaka 2010.
Alisema amekuwa kiongozi anayeng’ang’ania madaraka kwa muda mrefu, hivyo
asitarajie kupata uongozi. Aliwataka wananchi wa Zanzibar kumchagua Dk.
Shein kwa kuwa ni kiongozi mwenye sifa za pekee za ukweli, uaminifu na
uadilifu.
Kwa upande wake, Dk Maua Daftari alimwagia sifa Dk. Shein kuwa ni
kiongozi thabiti mwenye uwezo mkubwa wa kuviongoza Visiwa vya Zanzibar.
Alisema amewahi kufanya kazi na Dk. Shein na hivyo anamfahamu vizuri
kuwa ni mchapa kazi thabiti.
Balozi Ali Karume alisema Wazanzibar wasifanye makosa kuwachagua
viongozi nje ya CCM kwani wataurudisha Usultani ambao ulishaondolewa
katika visiwa hivyo wakati wa mapinduzi mwaka 1964.
Balozi Karume alisema anamfahamu Dk. Shein kuwa mchapakazi mwenye ndoto ya kuliinua Taifa lake kimaendeleo.
Nkumba aibuka
Wakati huo huo mwandishi wetu kutoka Sikonge anaripoti kuwa mgombea
urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ameendelea na
mikutano yake ya kampeni ya kujinadi kwa wapigakura ili wamchague awe
rais wa awamu ya tano.
Akitubia mkutano wake jana mjini hapa ghafla aliyekuwa Mbunge wa
Sikonge, Said Nkumba alijitokeza na kusababisha wananchi kuanza
kushangilia huku akikanusha kuhamia ACT-Wazalendo kama ilivyoripotiwa na
baadhi ya watu.
Nkumba alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi vitatu mfululizo, lakini
mwaka huu aligonga mwamba kwa kuanguka katika kura za maoni ndani CCM.
Kujitokeza kwa Nkumba katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini hapa
baada ya mjumbe wa kamati ya kamapeni, Abdallah Bulembo kumshambulia
Nkumba kwa kuwa kigeugeu na kuhama vyama vya siasa kwa sababu ya kukosa
ubunge.
“Nkumba nilisikia Kahamia Chadema na kuna taarifa amejiunga tena
ACT-Wazalendo, ndugu zangu CCM hakuna mwenye hatimiliki ya ubunge kila
mwanachama ana haki na huenda kuna ukweli maana hata hapa hayupo ila
ajue CCM itashinda tu na maisha yataendelea,” alisema.
Mara baada ya Bulembo kusema hivyo alimkaribisha Magufuli jukwaani na
kushangazwa na hatua ya Nkumba huku akisema si mwanasiasa mvumilivu.
“Uvumilivu ni suala muhimu, nasikia amekimbia ndivyo dunia ilivyo,”
alisema.
Wakati Magufuli akiendelea kuhutubia alijitokeza Nkumba katika mkutano
huo na wananchi kuanza kushangilia. Kutokana na ujio huo wake, Dk.
Magufuli alimwita jukwaani na kumkabidhi kipaza sauti huku akimtaka
kueleza ukweli kuhusu tukio la kuhama kwake na amuombee kura za urais.
Nkumba alisema hajaondoka CCM tangu aliporejea Agosti 23, mwaka huu
Jangwani jijini Dar es Salaam. Alifafanua chama kimemtenga na haitwi kwa
shughuli za chama kama awali.
“Kwa moyo mkunjufu ninapenda kumuombea kura mdogo wangu John Joseph,
madiwani pamoja rais mtarajiwa Dk. Magufuli muwachague Oktoba 25, mwaka
huu kwenye uchaguzi mkuu,” alisema.
Ufafanuzi huo ulimfanya Dk. Magufuli kuendeleza kueleza vipaumbele vyake
iwapo atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano na kumtaka mbunge huyo wa
zamani kurejesha kadi ya Chadema.
Hata hivyo, alisema ameiacha nyumbani kwake huku Dk. Magufuli
akiagiza apewe gari akaifuate ambapo Nkumba alifanya hivyo na kuikabidhi
kwa mgombea huyo.
Dk. Magufuli alisema ana changamoto wanazokumbana na wakulima wa tumbaku nchini ikiwemo Mkoa wa Tabora, alisema hivi sasa kuna wajanja wachache wamekuwa wakiwaumiza wakulima wa zao hilo na kwamba atasimama kidete ili wapate haki yao.
Dk. Magufuli alisema ana changamoto wanazokumbana na wakulima wa tumbaku nchini ikiwemo Mkoa wa Tabora, alisema hivi sasa kuna wajanja wachache wamekuwa wakiwaumiza wakulima wa zao hilo na kwamba atasimama kidete ili wapate haki yao.
0 comments:
Post a Comment