MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli,
amesema iwapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha anakomesha vitendo
mbalimbali vya kihalifu nchini ukiwamo ujambazi.
Mgombea huyo pia ametoa onyo kwa watu wasioitakia mema Tanzania
wanaoingiza nchini silaha haramu na kusema kuwa siku zao zinahesabika.
Wakati Dk. Magufuli akitoa onyo hilo, naye mgombea urais wa Chadema
chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa ametoa kauli inayofanana na
hiyo akisema iwapo ataingia Ikulu atajenga Tanzania mpya, kwani hataki
mchezo.
Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, alipokuwa
akihutubia mikutano ya kampeni iliyofanyika wilaya za Buhigwe, Kasulu na
Kibondo.
Katika mikutano hiyo, Magufuli alisema watu hao waovu hutoka nchi za
jirani baadhi yao wamekuwa wakishirikiana na Watanzania waliokosa
uzalendo kwa taifa lao.
Alisema watu hao huteka magari pamoja na kuua raia wasiokuwa na
hatia, jambo ambalo alisema kamwe hatolivumilia katika serikali yake.
Alisema moja ya kazi atakayoifanya endapo akichaguliwa kuwa rais, ni
kuhakikisha anakomesha vitendo vya uhalifu vinavyoharibu sifa ya taifa.
Alisema anashangazwa na matukio ya uhalifu katika mikoa ya Kigoma,
Kagera na Katavi, hali inayolazimu askari polisi kuwa na kazi ya
kusindikiza mabasi kila siku.
“Kigoma ipo jirani na Burundi, kuna watu ambao si wema huingia nchini
wakiwa na silaha na mabomu…cha kusikitisha wanashirikiana na Watanzania
wenzetu na hufanya matukio mabaya ya uhalifu.
“Kutokana na hofu ya usalama sasa polisi wamekuwa na kazi ya
kusindikiza mabasi…wakati wana kazi nyingine za kufanya. Nasema siku zao
zinahesabika, Serikali ya Magufuli itakomesha mambo haya.
“…ndio maana CCM katika ilani yetu ya uchaguzi, imesema italinda
amani amani amani… hata akija rais mwingine kupitia CCM naye atalinda
amani,” alisema Dk. Magufuli.
“Tunahitaji amani, ole wenu mnaoingia Tanzania na mabomu yenu , nawaambia yaacheni hukohuko,” alifoka Dk. Magufuli
Aliwaonya watu wanaoingia nchini kutoka nchi za Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Rwanda kuacha kuingiza silaha nchini.
“Nawaomba ndugu zangu, Serikali ya awamu ya tano itaimarisha
uhusiano na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na dunia kwa
ujumla,”alisema.
Atambia lugha
Dk. Magufuli ambaye kabla ya kuanza kuomba kura huanza kwa
kuwasalimia wananchi kwa lugha mbalimbali, jana alifanya hivyo na
kuamsha shangwe.
Alisema suala la yeye kuanza na salamu, halina uhusiano na masuala ya ukabila.
“Lugha ninazoongea si kwamba naendeleza ukabila… jamani Watanzania wote watakuwa wangu katika Serikali yangu,” alisema.
Akizungumzia mikakati ya Serikali yake, alisema elimu ya msingi hadi
kidato cha nne itakuwa bure sambamba na kuondoa michango ya kero kwa
wazazi.
“Kodi zote za kero tutaziondoa pamoja na kumaliza mgogoro wa Msitu wa
Kagera Nkhanda, ambao wananchi wanahitaji eneo kwa ajili ya kilimo,”
alisema.
Edwad Lowassa
Naye mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, amesema atakapoingia madarakani atajenga Tanzania mpya kwa sababu hataki mchezo.
Amesema kwamba, pamoja na umasikini unaowakabili Watanzania, Serikali
yake itaondoa hali hiyo kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi za
kukabiliana na umasikini huo.
Lowassa aliyasema hayo mjini Bariadi jana alipokuwa akihutubia
mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Halmashauri Jimbo la Bariadi
Magharibi, ambalo mbunge wake aliyemaliza muda ni Andrew Chenge (CCM).
“Rais wa Marekani Barack Obama alipokuwa akiomba kura kwa Wamarekani,
aliwauliza can we (tunaweza?), nao wakamjibu, yes we can (ndiyo
tunaweza).
“Kwa hiyo na mimi nawaambia tunaweza, nikiingia madarakani nitaijenga
Tanzania mpya ili aliyekuwa na gari moja awe na magari mawili,
aliyekuwa na baiskeli moja awe nazo kumi na aliyekuwa na boda boda moja,
awe nazo ishirini.
“Katika nchi yetu, tuna rasilimali nyingi na kama tukizitumia vizuri,
kila mmoja ataishi maisha mazuri kwani chini ya Serikali yangu, elimu
itatolewa bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
“Nawahakikishieni michango yote mashuleni itaondolewa, yaani mtoto
wako atakayefaulu darasa la saba mwaka huu, atakapoingia fomu one
mwakani hatalipa chochote.
“Hata baada ya kuapishwa, ushuru wote wa mazao utakoma, wakulima
watakuwa huru kwenda kuuza mazao yao popote, atakayetaka kuuza mazao
yake, Rwanda, aende, atakayetaka kuuza Kenya, Uganda au kwingineko ni
shauri yake, apeleke tu.
“Nawaahidi kwamba, nitaunda Serikali ya maendeleo sitaki mchezo,
nipeni kura kwa sababu kazi hiyo naiweza na ninatosha,” alisema Lowassa.
Pamoja na hayo, mgombea urais huyo aliwasisitizia Watanzania watunze
shahada zao za kupigia kura ili waweze kuzitumia Oktoba 25 mwaka huu,
kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wote wa Ukawa.
Akizungumzia sekta ya maji, Lowassa alisema Serikali yake itafanya
kila liwezekanalo kufikisha maji ya ziwa victoria katika mji wa Bariadi
kama alivyofanya kwa kusafirisha maji ya ziwa victoria kutoka Mwanza
hadi Shinyanga.
SUMAYE
Naye waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alipokuwa akiwahutubia
wananchi hao, alisema kama Watanzania wanataka maisha bora, lazima
waiondoe CCM madarakani kwa kuwa ndiyo iliyowasababishia maisha magumu.
Pamoja na hayo, alisema CCM ni kama mtumbwi uliotoboka na kuingia
maji na kwamba ili waliomo waweze kuokoa maisha yao, njia pekee ni
kushuka katika mtumbwi huo kabla haujazama.
“Tusipoiondoa CCM marakani kamwe hatutapata maisha bora Tanzania. Hebu angalieni, mnalima pamba kila mwaka lakini haiwanufaishi.
“Wakati wao wameshindwa kuwasaidia kupitia pamba, Serikali ya Ukawa
itaimarisha kilimo, Serikali ya ukawa itaimarisha huduma za afya
hospitalini tofauti na sasa ambapo huduma za afya ni mbovu.
“Nyie mliobaki huko CCM, kumbukeni Mwalimu Nyerere aliwahi kusema CCM
siyo mama yake, sasa wewe unayeng’ang’ania huko unataka kuniambia
unaijua vizuri CCM kuliko Mwalimu Nyerere?
“Serikali ya CCM imejaa mafisadi ambao kila siku wanamtukana Mzee
Lowassa na pia ufisadi umejaa katika Wizara ya Ujenzi anayoiongoza
Magufuli (Dk. John Magufuli, mgombea urais wa CCM).
“CCM maji hayako tena shingoni bali sasa maji yamewafika puani,
hawana jipya tena na ndiyo maana hata Magufuli kwenye mabango yake
ameandika Chagua Magufuli badala ya Chagua CCM,” alisema Sumaye.
0 comments:
Post a Comment