HAMISI Kiiza jana alituma salamu kwa Yanga baada ya kuifungia Simba
mabao matatu katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mechi ya
Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Hizo ni salamu kwa
Yanga kupitia mchezaji wake huyo wa zamani kwani watani hao wa jadi
Jumamosi watamenyana kwenye uwanja huo.
Yanga juzi iliifunga JKT Ruvu mabao 4-1 na kufikisha pointi tisa,
sawa na Simba zikiwa zimetofautiana uwiano wa mabao. Mechi hiyo ilianza
kwa kushambuliana kwa zamu na Kiiza alianza kuliona lango la Kagera
Sugar katika dakika ya 30 baada ya kuunganisha mpira wa kichwa wa Simon
Sserunkuma.
Bao hilo liliichanganya Kagera na kufanya mabadiliko ya haraka kwa
kumtoa Laurence Mugia na kumuingiza Babuu Ally, lakini hali haikuwa
shwari na kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na iliichukua Simba dakika sita tu
kuandika bao la pili likifungwa na Kiiza tena kwa kichwa akiunganisha
mpira wa adhabu uliopigwa na Said Ndemla. Dakika nne baadaye Kagera
ilipata bao lake la kufutia machozi likifungwa na Mbaraka Yusuph
aliyewapiga chenga mabeki wa Simba na kufunga kirahisi.
Baada ya bao hilo, kocha wa Simba Dylan Kerr alifanya mabadiliko ya
harakaharaka kwa kumtoa Sserunkuma, Emery Nibomana na Ibrahim Ajibu na
kuwaingiza Pape Ndow, Hassan Ramadhan na Mwinyi Kazimoto.
Huku mashabiki waliofurika uwanjani hapo wakiamini matokeo yangekuwa
2-1, dakika ya 90 Kiiza aliwainua tena mashabiki wa Simba kwa kufunga
bao la tatu akiunganisha pasi ya Kazimoto.
Katika matokeo mengine jana, Azam ilishinda bao 1-0 ugenini dhidi ya
Mwadui kwenye uwanja wa Mwadui Shinyanga na Coastal Union ikiwa ugenini
uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ililazimisha sare ya bila kufungana dhidi
ya Toto African.
Nayo Mtibwa Sugar iliendelea kung’ara baada ya kuifunga Ndanda 2-1
kwenye uwanja wa Manungu. Kikosi cha Simba jana: Peter Manyika, Emery
Nimubona/Hassan Kessy, Mohammed Hussein, Hassan Isihaka, Justuce
Majabvi, Awadh Juma, Simon Sserunkuma/Pape Ndow, Said Ndemla, Ibrahim
Hajib/ Mwinyi Kazimoto, Hamisi Kiiza na Peter Mwalyanzi.
Kagera Sugar: Agathon Anthony, Salum Kanoni, Said Hassan/ Abubakar
Mtiro, Ibrahim Job, Deogratius Julius, George Kavilla, Iddi
Kurachi/Kenneth Masumbuko, Lawrence Mugia/Babuu Ally, Mbaraka Yussuf,
Daudi Jumanne na Paul Ngalyoma.
0 comments:
Post a Comment