TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyama vya siasa nchini
viitumie ipasavyo kwa kuifikishia malalamiko wakati wote vitakapoona
vimedhulumiwa haki ili madai husika yatafutiwe ufumbuzi kwa mujibu wa
taratibu zilizopo, badala ya kunung’unika chinichini au kukimbilia
kwenye vyombo vya habari.
Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam juzi kati ya Tume hiyo na
wanahabari, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria za NEC, Emmanuel
Kawishe alisema, tangu kampeni za uchaguzi mkuu zianze karibu vyama
vyote vilivyolalamika kudhulumiwa haki vimekwepa kuchukua hatua ya
kuijulisha Kamati ya Maadili ya NEC kama vilivyokubaliana awali.
Kawishe alisema, badala yake, vimekuwa vikilalamika pembeni na kwenye
vyombo vya habari, hatua inayoifanya tume hiyo ishindwe kufanyia kazi
malalamiko hayo, kwa sababu si rasmi.
Inaelezwa kuwa, vyama vya siasa 22 vilikubaliana na kusaini Maadili
ya Uchaguzi yaliyohusisha kipengele kinachovitaka vitakavyoona kuwa
vimedhulumiwa haki wakati huo wa kampeni na uchaguzi, vifikishe
malalamiko hayo kwa kamati hiyo ya maadili ili yafanyiwe kazi.
Katika maelezo yake kwa wanahabari, Kawishe alisema vyama vya siasa
kuacha kufuata ngazi husika kupeleka malalamiko ni kukiuka maadili
viliyoyakubali na kuyasaini. Alivitaja moja kwa moja vyama vinavyounda
Ukawa; Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NLD, CUF na
NCCR-Mageuzi kuwa mfano wa vyama vinavyoendelea kukiuka makubaliano hayo
kwa kushindwa kushitaki kwenye tume kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya
umoja huo ili upatiwe suluhu.
Kawishe alisema, ingawa malalamiko yanayoripotiwa kwenye vyombo vya
habari ni mengi yanayohusisha vyama mbalimbali, kamati ya maadili
imepokea mawili tu yaliyo tofauti na malalamiko ambayo vyombo hivyo vya
habari vimeyaeleza.
Alieleza kuwa mashitaka yaliyopokewa yanahusu vyama kuingiliana
ratiba za kampeni zinazoendelea, ambayo hata hivyo yalishughulikiwa na
kupatiwa ufumbuzi kwa amani na haraka. Kwa mantiki hiyo, tunaona kuna
umuhimu wa vyama vya siasa kuanza kuitumia kamati hiyo kama vilivyo
kubaliana ili malalamiko yanayofikishwa kwenye chombo hicho yafanyiwe
kazi kwa haki.
Aidha, tunapenda kuwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa pamoja na
wanachama wao kuwa ingawa vyombo vya habari vipo kwa ajili yao,
kuvitumia kana kwamba vinaweza kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu malalamiko
au mashitaka yao ni kujipotosha.
Aidha, kwa kuwa NEC ilikwishaweka wazi mapema nia na wajibu wake wa
kuhakikisha uchaguzi mkuu unapita kwa usalama, itakuwa busara endapo
vyama vya siasa vitashiriki kuisaidia ifanikishe azma hiyo, badala ya
kuwa chanzo cha chokochoko zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Kwa
ufupi, vyombo vya habari vina wajibu tofauti na suala zima la
kushughulikia malalamiko.
Vinapaswa vitumiwe kwa mambo ya maendeleo na si kusambaza taarifa za
migogoro ya kisiasa baina ya vyama vya siasa au wafuasi wake. Kutokana
na ukweli huo, tunawajibika kuvikumbusha vyama vyenye migogoro
kutekeleza makubaliano kwa kushitaki ukiukwaji wowote wa maadili ya
uchaguzi kwa kamati hiyo. Hili litasaidia katika kuhakikisha migogoro
inafanyiwa kazi na kuchukuliwa hatua kabla ya siku ya uchaguzi ili
umalizike kwa amani.
0 comments:
Post a Comment