CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kampeni za urais Zanzibar huku
mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, akisema hawawezi kushinda bila
kujipanga vyema.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo katika Uwanja wa Demokrasia wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
“Hatuwezi kushinda hivi hivi, ni lazima tujipange vizuri, uchaguzi wa mwaka huu ni man to man (mtu na mtu)
“Lazima umjue mtu wako vizuri, umkabe ipasavyo, uombe kura na uipate.
Uchaguzi huu pia ni kiambo kwa kiambo, nyumba kwa nyumba, chumba kwa
chumba, shuka kwa shuka,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa.
Alisema kutokana na umati mkubwa uliojitokeza katika mkutano huo, ni
dhahiri chama hicho kimeshinda na kwamba wengine wataendelea kuwa
wasindikizaji.
“Huu umati unaonyesha ni jinsi gani tulivyoshinda, wengine
wataendelea kuwa wasindikizaji na wale wasindikizaji wazoefu wataendelea
kutusindikiza tu,” alisema.
Alisema CCM ina haki ya kuchaguliwa tena kutokana na kuongoza nchi
vyema na kwamba pale ambako amani ilikosekana ilisababishwa na wengine.
Rais Kikwete aliwaambia wananchi hao kuwa wasiwape nafasi tena
wapinzani na kwamba Zanzibar itendelea kuwa na amani endapo watamchagua
Dk. Ally Mohamed Shein.
Rais Kikwete alimrushia kijembe mgombea urais wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad, ambaye anadai Serikali ya Zanzibar haijafanya maendeleo
yoyote wakati alikuwa sehemu ya Serikali hiyo kama makamu wa kwanza wa
rais na alishindwa kuleta maendeleo.
Rais Kikwete alitumia hotuba yake kwa njia ya maswali ambapo alikuwa akiwauliza wananchi nao walijibu huku wakimshangilia.
“CCM imeongoza vema na nchi imetulia, Zanzibar imetulia haijatulia? …ambapo wananchi wakiitikia…imetulia
“Hao wanaolalamika msiwape, ni jambo la kusikitisha hao wanaolalamika
wako kwenye Serikali, kama mtu ni Makamu wa Rais halafu anasema
Serikali imeshindwa kwa nini hajiuzulu?
“Huwezi kuwa kwenye serikali, wewe mwenyewe ni makamu wa kwanza wa
rais halafu serikali hiyo haina maendeleo sasa kwanini hujaondoka,
msiwape nafasi…washindwe,”alisema Rais Kikwete.
Alieleza kushangazwa na watu ambao wamekuwa wakisema Dk. Shein ni
mpole wakati hekima na busara zake ndivyo vilivyomfikisha hapo huku
wengine wakifanya fujo.
“Hao wanaofanya fujo waendelee kuwa wa pili lakini Shein ni mzalendo
wa kweli na ana uchungu na Zanzibar, hana sura mbili na hana ndimi mbili
lakini anayo sura moja ya kizanzibari, anayo lugha moja ya kutetea
mapinduzi na kulinda muungano.
Dk. Shein
Kwa upande wake, mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dk. Shein alisema kwa
kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali yake imelinda mapinduzi na
ataendelea kulinda kwa kuwa hakuna maendeleo bila mapinduzi.
“Tutaendelea kuyalinda mapinduzi yetu kwa sababu ndiyo ngao na nguzo na hakuna amani na mshikamano bila mapinduzi,”alisema.
Alisema sera ya CCM ya kujenga umoja wa kitaifa, amani na utulivu ni nguzo ya pili.
“Amani ni msingi mkubwa ya maendeleo ya dunia nzima. Amani hii
haikuja bure, ilitafutwa kwa udi na uvumba. Hadi leo amani ndiyo sera
yetu kubwa na tutaendelea kuidumisha.
“Nimekabidhiwa ilani leo na Rais Kikwete tutahubiri amani. Amani
itabakia amani, kupendana baina ya bara na visiwani, Zanzibar na wapemba
sote ni wamoja ni ndugu. Tutaendeleza amani hii kwa miaka mitano
ijayo,”alisema mgombea huyo.
Alisema uzoefu alioupata kuongoza Zanzibar ilihitaji uvumilivu wa
hali ya juu na kwamba kutokana na uzoefu huo hatashindwa kuendeleza
amani.
“Nilipata kusema katika uchaguzi uliopita kuwa sitaogopa mtu leo
narudia sitaogopa mtu yeyote bali Mwenyezi Mungu. Nitajenga heshima
yangu na wao wanijengee heshima. Nitafanya hivyo kwa kipindi kijacho
nitaitetea Zanzibar na Tanzania nzima,”alisema.
MUUNGANO
Alisema Muungano ni suala la msingi kwa kuwa hakuna mbadala mwingine
na kwamba hakuna muungano nchi nyingine Afrika iliyoweza kudumisha.
“Ni lazima tufanye uamuzi wa pamoja wa kumchagua Dk. John Magufuli
na Samia Suluhu Hassani. Wala msidanganyike, msitishike na hakuna mtu au
kikundi cha watu ambacho kitaweza kuvunja muungano.
“Nyerere na karume waliunganisha kwa ridhaa ya wananchi wenyewe hivyo
hauwezi kuvunjwa na mtu mmoja. Hawawezi kututishia kwa kauli nasema
haiwezekani mambo haya yana taratibu zake. Muungano ni jambo kubwa sana,
tutaendelea kuutetea kwa nguvu zetu zote.
UCHUMI
Alisema tayari serikali imekwishatunga sheria ya mafuta na kwamba
hawatanii katika hilo na kwamba wameshaandika maelewano ya awali ili
watoe kibali ya kuanza kuchimba gesi.
Aidha alisema jitihada za utaalamu wa hali ya juu zikifanyika baada ya miaka mitano au sita wataanza kuchimba mafuta.
“Mambo yakipamba moto wataalamu hawa watafanya hivyo na hili litainua uchumi wa nchi yetu.
“Kuhusu Barabara, huduma za afya, elimu, yote nitaeleza mambo mazuri
kweli kweli yote yapo humu kwenye ilani. Nitafanunua kinagaubaga
katika mikutano yangu ya kampeni.
“Wote wanaopenda maendeleo yetu waje wanichague mimi, tuko 14 lakini
CCM ndiyo namba moja. Kazi hiyo tutaikamilisha tukimchagua Magufuli na
Samia Suluhu,”alisema.
Dk. Shein ambaye alihitimisha hotuba yake saa 11:55 jioni, aliwataka
wananchi hao kutunza vitambulisho vyao kwa kuwa kuna watu wanaviwangia.
“Vitunzieni vitambulisho vyetu kuna watu wanaziwangia, mvitunze mpaka
Oktoba 25, wembe ni ule ule. Mko tayari?,” Dk. Shein aliwahoji wananchi
hao huku akijibiwa; “Tupo tayari”.
Awali Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema anamshangaa
Maalim Seif aliposema kuwa endapo atachaguliwa ataibadilisha Zanzibar
kuwa kama Singapore wakati chama chake kina nusu ya baraza la mawaziri.
“Wana nusu ya baraza la mawaziri. Tulitarajia angetupa nusu ya
Singapore, aache kutudanganya, alikuwa waziri kiongozi hakuleta
Singapore. Kashagombea mara nne, sasa ni mara ya tano na hapati
tumwambie bye bye,”alisema Kinana.
Bilal
Naye Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal katika mkutano huo
aliwataka wananchi waache tofauti zao na kuwa kitu kimoja ili waweze
kushinda kwenye uchguzi huo.
“Huu ni mkutano wa aina yake kwa kuwa sijawahi kuona watu kuwa wengi
hapa Kibanda maiti kama hivi, nafahamu kuja huku ni kutaka kufahamu juu
ya wasiwasi mliokuwa nao juu ya uongozi wa nchi hii,”alisema Dk Bilal.
Dk. Bilal alisema anawaombea tiketi wagombea wao wa urais ambao ni
Dk. John Magufuli, Samia Suluhu, Dk. Mohamed Shein, wakiwamo na wagombea
wa nafasi nyingine za uongozi kama vile ubunge, udiwani, uwakilishi na
udiwani.
“Nyerere alisema nchi yetu itayumba bila ya uongozi wa CCM hivyo
mkae mtulie mtafakari, wagombea wote hao ndio watakao tuwezesha
kushinda pia nawaomba tusahau tofauti zetu ili tuwe wamoja,”alisema Dk
Bilal.
Mwinyi
Naye Rais Mataafu Ally Hassani Mwinyi alisema amekuwapo katika
ufunguzi huo ili kuhakikisha ushindi unapatikana kwa chama chake katika
uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
“Leo ni siku ya kulala pamoja ambapo tukiondoka kila mmoja wetu anajua nafasi yake ili CCM ishinde na kura zote tumpe Dk Shein.
“Mliopo hapa mmeiona hatari inayowakabili wapinzani, hali kama hii
sijapata kuiona mahali popote Zanzibar, Mwenyezi Mungu yupo kwa wengi na
sisi ndio wengi,”alisema Mwinyi.
Mkapa
Rais Mstaafu Benjamini Mkapa alisema kwamba anaimani na Dk. Shein kwa
kuwa amefanyanaye kazi na kupata nafasi ya kuufatilia uongozi wake
alipokuwa na Rais Jakaya Kikwete akiwa kama makamu wa rais.
“Amedhihirisha umakini , uadilifu, pamoja na uchapakazi wake nina
imani anastahili kupewa kipindi kingine cha uongozi wa Zanzibar kwa kuwa
tunataka kiongozi atakayeenzi muungano wa nchi hii na asiyesahau
wakombozi wa taifa hili.
“Zaidi ya hapo muwe na imani mikononi mwake taifa litakuwa salama
hivyo wapigieni kura wanaCCM zaidi ni fahari sana kwangu nina imani na
Dk. Shein, shein kweli… Kweli, Mna imani na Shein? Mikono juu,”alisema
Mkapa.
Naye Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Karume alisema ni hekima kwa CCM
kukubali mfumo wa vyama vingi na kudai kwamba ni muhimu kwa wananchi
kuisimamia na kuilinda amani ili nchi iendelee kuwa na umoja.
Pia rais huyo mstaafu alihoji kwa baadhi ya wanasiasa wanaotumia lugha ya matusi wakiwa jukwaani kama ni lazima wafanye hivyo.
“Kwani lazima wanasiasa wanapokuwa jukwaani watukane? Mimi sina
tabia ya kumsema mtu kwa kuwa baada ya kumsimfu baadae utaanza
kumkashifu,” alisema.
Awali watu walianza kuingia katika uwanja huo saa sita mchana huku
wakiongezeka kadri muda ulivyokuwa unakwenda, huku vikundi mbalimbali
vya burudani vikiendelea kutumbuiza.
Dk Shein aliingia uwanjani hapo akiambatana na viongozi mbalimbali wa
chama na Serikali hku ulinzi ukiimarishwa kila kona ya uwanja huo.
Wasanii mbali mbali waliotumbuiza kampeini hizo mbali na Diamond Platinums, Mzee Yusuph, Peter Msechu na Amini.
Home
News
Hatuwezi kushinda hivi hivi,ni lazima tujipange vizuri,uchaguzi wa mwaka huu ni man to man.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment