MSAFARA wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John
Magufuli, umenusurika kupata ajali, baada ya lori la mizigo kuuvamia na
kugonga magari matatu likiwamo lililokuwa limembeba mpiga debe wa chama
hicho, Amon Mpanju.
Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika eneo la Njia Panda jirani kilomita chache kabla ya kuingia Maswa mjini.
Akizungumza na MTANZANIA , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemin Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema wakati msafara huo ukitoka wilayani Meatu, askari polisi
waliokuwa wakiuongoza msafara huo walimuaru dereva wa lori hilo lenye
namba za usajili T 217 DDY kuegesha pembeni gari lake, lakini alikaidi.
“Msafara wa mgombea urais ulikuwa jirani kuingia Maswa, dereva wa
lori aliamuriwa kuliweka pembeni akakaidi, tena kibaya akaongeza mwendo
hali iliyosababisha ajali.
“Lori hili ni mali ya Kampuni ya Dilchadri Mill Ltd ya jijini Mwanza,
liligonga magari matatu likiwamo gari lenye namba za usajili T 217 CYM
aina ya Toyota Land Cruser ambayo iliharibika vibaya na kushindwa
kuendelea na safari.
“…Baada ya tukio hili, dereva amekimbia na polisi wanamsaka ili afikishwe mbele ya vyombo vya sheria,” alisema Kamanda Mushi.
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Mushi amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Alisema hakuna mtu aliyeumia katika ajali hiyo.
Wakati huo huo, mgombea huyo aliendelea na mikutano yake katika wilaya za Maswa, Kishapu na Igunga.
Kwa nyakati tofauti katika mikutano hiyo, Dk. John Magufuli,
aliwataka Watanzania kuchagua wabunge ambao watatetea masilahi yao
badala ya wale wanaotoka bungeni kila zinapowasilishwa bajeti.
Alisema endapo atachaguliwa anataka kuona Bunge linalotimiza wajibu wake, ikiwemo kupigania kero za waliowachagua.
“Haiwezekani wakati wa kujadili hoja za wananchi, wenzako wanatoka nje wanafanya hivi kwa kumkomoa nani?
“Maswa ninyi ni mashahidi kwa muda mrefu hamkuwa na mtu wa kuwasemea
tatizo la maji, barabara na hata huduma za afya. Maana kila zinapopangwa
bajeti wao wanatoka nje je waziri atajuaje kama kuna tatizo eneo
husika.
“Hii si demokrasia hata kidogo ila ni kuwatesa wananchi, kwa hali
hiyo sasa Watanzania wote chagueni wabunge wenye masilahi kwenu na
watakaosemea shida zenu na si wale wanaotoka nje kila wakati (Ukawa),”
alisema Dk. Magufuli
Aonya lugha chafu
Alisema ni vema viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kampeni za matusi, kwani hazina tija kwa Taifa.
“Matusi si hoja, ndiyo maana kila ninaposimama situkani mtu, najenga
hoja. Tunahitaji kujenga nchi yetu iwe ya amani siku zote,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment