MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya
mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, amesema wamekikamata pabaya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa Watanzania sasa wanataka mabadiliko.
Amesema pia kwamba, kitendo cha mamilioni ya Watanzania kutaka
mabadiliko, pia kinaungwa mkono na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, aliyewahi kusema Watanzania wanahitaji mabadiliko na
wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wanaokosoa Ukawa, wawe na hoja za msingi badala ya kutukana.
Lowassa aliyasema hayo mjini Kimboi, Jimbo la Iramba Magharibi,
mkoani Singida, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika
katika uwanja wa Shule ya Msingi Kiomboi Bomani.
“Nimekuja hapa kwa heshima kubwa ili niwaombe kura kwa sababu
uchaguzi ni mchezo wa hesabu, bila kura za kutosha hatuingii Ikulu ng’o.
“Nawaambia tusiwapowashinda mwaka huu, hatutawashinda tena, lazima
waondoke kwa sababu Watanzania wanataka mabadiliko, tunazo baraka za
Mungu na Mwalimu Nyerere.
“Wameanza kutuiga lakini wajue tunayoyafanya tumetoka nayo mbali,
tumewakamata pabaya kwa sababu wananchi wanataka mabadiliko na sisi tuko
tayari kwa mabadiliko, mabadiliko haya ni ‘unstoppable
(hayazuiliki),”alisema Lowassa.
Akizungumzia ajira kwa vijana, Lowassa alisema atakapoingia
madarakani, Serikali yake itaanzisha Benki kwa ajili ya vijana
wanaoendesha boda boda pamoja na benki ya wachimbaji wadogo wadogo.
Kwa mujibu wa Lowassa, sekta nyingine zitakuwa zikipatiwa ufumbuzi wa matatizo yanayozikabili kulingana na wakati husika.
“Nasema tutaondoa umasikini nchini kwa sababu nitaunda Serikali
inayofanya kazi kwa kasi na asiyekuwa na uwezo wa kukabiliana na kasi
yetu, atupishe.
Awali akihutubia mkutano mwingine katika Kijiji cha Ilogelo Jimbo la
Singida Kaskazini, mgombea urais huyo alisema kama Watanzania hawatapiga
kura za kuiondoa CCM madarakani, watakuwa wamejiangamiza.
Alisema kwamba, ingawa CCM wamekuwa wakitoa ahadi nyingi kwa
wananchi, wamekuwa hawatekelezi ahadi hizo, jambo linalowafanya
Watanzania wasiwe tena na sababu ya kukiamini chama hicho.
“CCM hawataki mabadiliko ingawa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema
Watanzania wasipopata mabadiliko ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM.
“Najua wananchi wanataka mabadiliko ndiyo maana niliwahi kusema siwezi kuzuia mafuriko kwa mikono lakini wakanidharau.
“Matokeo yake sasa yanaonekana kwa sababu tulipokwenda Iringa,
mafuriko yalikuwa ni haya haya, tulipokwenda Ruvuma, mafuriko ni haya
haya, tulipokwenda Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma, mafuriko yalikuwa ni
haya haya.
“Sisi hapa tumejitokeza kuongoza mabadiliko ili yaje, lakini jambo la msingi kwenu ni kupiga kura ili mabadiliko hayo yaje.
“Msipopiga kura tukashinda, mtakuwa mmejiangamiza na msipopiga kura
za uaminifu, mtaibiwa, CCM ikishinda mambo yatakuwa ni yale yale.
“Nawaambieni bila kura za kutosha tumeliwa na ili tushinde, mwambie
hata rafiki yako aliyeko popote, iwe na Dare es Salaam au kwingineko
nchini, kwamba Lowassa anataka kura yako.
“Kama mtanionyesha imani ya kutosha kwa kunipa kura za kutosha,
nawaahidi utumishi uliotukuka kwa sababu imani huzaa imani” alisema
Lowassa na kushangiliwa.
Pamoja na hayo, Lowassa ambaye amewahi kuwa waziri mkuu, aliwataka
pia Watanzania wasidanganywe na maneno ya baadhi ya watu wasioitakia
mema Tanzania.
Alisema kwamba, katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu,
yatatolewa maneno mengi yakiwamo yasiyokuwa na maana na kwamaba jambo la
msingi ni wananchi kuwa na msimamo wa kuiondoa madarakani CCM.
Akizungumzia mazao ya alizeti, nyanya na vitunguu yanayolimwa mkoani
Singida, alisema atakapoingia madarakani, atajenga viwanda vya kusindika
mazao hayo badala ya utaratibu wa sasa ambapo mazao hayo yananunuliwa
na Wakenya.
LISSU
Naye Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema Lowassa ndiye
kiongozi anayeifaa Tanzania kwa kuwa ana uwezo mkubwa kisiasa kuliko
mwanasiasa yeyote nchini.
Pamoja na hayo, Lissu alitumia muda mwingi kuwaeleza wananchi jinsi
Lowassa asivyohusika na kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.
Katika maelezo hayo aliyoyatoa katika mikutano ya Singida Kaskazini
na Iramba Magharibi, Lissu alitumia kitabu cha ripoti ya Kamati Teule ya
Bunge iliyosomwa bungeni mwaka 2008 na aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe.
MSINDAI
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Singida ambaye pia ni
mgombea ubunge katika Jimbo la Singida Mjini kupitia Chadema, Mgana
Msindai, aliendelea kusema CCM haina tena sifa za kuongoza Tanzania kwa
kuwa imepoteza mwelekeo.
Pamoja na hayo, alimshutumu aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini,
Lazaro Nyalandu (CCM), kwamba ameshindwa kuwasaidia ajira vijana wa
jimbo hilo licha ya kuliongoza kwa miaka 15.
MGEJA
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga,
Khamis Mgeja, alisema kitendo cha baadhi ya vigogo wa CCM kuhamia Ukawa
ni dalili ya chama hicho kupoteza mwelekeo.
Alisema ni aibu kwa Watanzania kuendelea kukiunga mkono CCM wakati
shida zimekuwa zikizidi kila mwaka ingawa nchi ina rasilimali za
kutosha.
Sumaye: Hakuna wa kuifufua CCM
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Jimbo la Ubungo
jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema kwa
sasa hakuna njia au mtu atakayeweza kuifufua CCM.
Sumaye alisema wamezunguka maeneo mengi ya nchi kila walipokuwa
wakienda wamebaini Watanzania hivi sasa wanahitaji mabadiliko na hawana
mpango wa kuongozwa tena na CCM.
Aidha Sumaye alipingana na wale wanaosema amejiunga Ukawa kwa uchu
wa madaraka, na kusema kuwa uchu wake wa kujiunga Ukawa ni kutaka
kuing’oa CCM.
“Sikuja Ukawa kutafuta cheo kwa sababu nimeshakuwa waziri mkuu na
hata hapa Ukawa hakuna nafasi ninayotaka kwa sababu nafasi ya urais yupo
Lowassa na nafasi ya waziri mkuu siwezi kupata kwa sababu sijagombea
ubunge ila ninachofanya ni kuhakikisha CCM inaondoka madarakani,”
alisema.
Sumaye alisema kwa kuingia kwake Ukawa, amejikuta akipata vitisho
kutoka serikalini ikimtishia kumny’anyang’anya mashamba yake, kitu
anachokiona ni sawa na kumpiga chura teke.
“suala la kunitisha kuninyang’anya mashamba yangu ni kunikomaza zaidi
kwa kuwa naamini suala hilo ni sawa na kumpiga chura teka.” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment