Image
Image

Homa ya Mapafu Kwa watoto (Pneumonia).

Homa ya mapafu ni aina ya maambukizi yanayoathiri mapafu. Ni ugonjwa ambao unaua watoto wengi hasa katika nchi zinazoendelea duniani. Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio chini ya miaka 5 maisha yao hupotea kila mwaka kutokana na ugonjwa huu. Kutokana na vifo vingi vinavyotokana na homa ya mapafu tarehe 12 ya mwezi wa Novemba kila mwaka imefanywa kuwa siku rasmi ya homa ya mapafu duniani, ili kuwajuza walimwengu maradhi hayo na kuwahamasisha namna ya kujikinga na kuyatibu. Kabla hatujaendelea mbele ni bora kwanza tuwaeleze wasikilizaji wetu muundo wa mapafu ulivyo na sehemu ambayo ugonjwa huu hushambulia.
Mapafu yanajumuisha mirija mikubwa ya hewa inayoitwa bronchi ambayo hugawanyika na kufanya mirija midogo zaidi ya hewa inayojulikana kama bronchioles, ambayo nayo hutengeneza vifuko vidogo vidogo vya hewa vinavyoitwa alveoli. Vifuko hivi vidogo vya hewa vina mishipa ya kupitisha damu ambayo husaidia kuchuja na kusafirisha hewa safi ya oksijeni tunayovuta kuingia kwenye damu, na hewa chafu ya kaboni dioksidi kuondolewa kwenye damu na kuingizwa kwenye mapafu tayari kwa ajili ya kutolewa nje ya mwili. Kwa kawaida vifuko hivi vidogo hujaa hewa muda wote tayari kusafirishwa. Inapotokea mtu akapata homa ya mapafu, vifuko hivi hujaa maji au usaha, hivyo kuathiri upitishaji wa hewa safi kwenye damu na kusababisha tatizo la kupumua.
Lakini baada ya kujua hayo, je, homa ya mapafu husababishwa na nini?
Kuna aina kadhaa ya vimelea ambao vinaweza kusababisha maambukizi katika mapafu. Vimelea hivi hujumuisha bakteria, virusi, parasaiti na fangasi.
Vimelea hivi hushambulia mwili wa binadamu kulingana na umri na kinga ya mwili wake. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa watoto wakubwa.
Baadhi ya vimelea wa bakteria wanaoshambulia watoto ni pamoja na Streptococcus pneumonia, ambao ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto. Wapo pia Haemophilus influenzae aina b (Hib), ambao ni aina ya pili ya bakteria walio maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa ya mapafu kwa watoto. Staphylococcus aureus ni aina nyingine ya bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wachanga. &&&&&&
Kwa upande wa virusi, aina ya Respiratory syncytial virus ndio wanaoongoza kwa kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.
Aidha, vimelea wa Pneumocystis jiroveci ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasaiti ni maarufu zaidi miongoni mwa parasaiti wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini hususani watoto wenye virusi vya Ukimwi. Aina nyingine za bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na Mycoplasma pneumonia na Chlamydia pneumonia.
Baada ya kujua aina mablimbali za vimelea wanaosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu kwa watoto wadogo, sasa tuangalie jinsi homa ya mapafu inavyoenezwa.
Kuna namna nyingi za kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa kawaida, virusi na bakteria hupatikana katika sehemu ya juu ya mfumo wa njia ya upumuaji yaani upper respiratory tract. Inapotokea kinga ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yeyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji yaani lower respiratory tract na hatimaye kushambulia mapafu. Hali kadhalika, vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya kuzaliwa yaani kipindi cha mimba. Dalili za ugonjwa wa homa ya mapafu
hutegemea umri wa mtoto. Kwa watoto wadogo, dalili za awali zinaweza kuwa homa kali pamoja na mtoto kuhangaika na kunyong'onyea. Watoto wanaozaliwa wakiwa na maambukizo ya bakteria aina ya Streptococcus kundi B wanaweza kuwa na homa na kupumua kwa shida. Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na dalili ambazo si maalumu kama vile kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yeyote ya kushindwa kupumua. Hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule. Dalili za kawaida za homa ya mapafu ambazo huwapata karibu watoto wote wanaoathirika na ugonjwa huu ni pamoja na:- Kuwa na homa, kuhisi baridi na kikohozi. Kupumua kwa haraka kuliko kawaida na kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa kupumua. Dalili nyingine ni mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa kupumua na pia maumivu ya tumbo. Mtoto kutokuwa na hamu ya kucheza na kupoteza hamu ya kula na kushindwa kunyonya. Pia mtoto hubadilika rangi na kuwa na rangi bluu katika midomo na kucha. Hata hivyo, si lazima dalili zote hizi ziwepo kwa kila mtoto. Baadhi ya watoto huonesha kupumua kwa haraka kama dalili pekee ya homa ya mapafu. Iwapo vimelea vimeshambulia sehemu za chini ya mapafu karibu ya tumbo, sehemu ijulikanayo kama kiwambo au diaphragm, mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya kushindwa kupumua ingawa anaweza kuwa na homa na kuhisi maumivu makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika. Watoto wachanga wanaweza kushindwa kunyonya, na pia kupoteza fahamu na kupata degedege.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment