WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 39 kujeruhiwa vibaya baada
ya basi la Kampuni ya Metro, kuacha njia, kutumbukia bondeni na
kupinduka.
Basi hilo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Rombo mkoani Kilimanjaro.
Miongoni mwa waliokufa ni watatu wa familia moja, ambao ni baba, mama
na binti yao mwenye umri wa miaka 12, wote wakazi wa mjini Moshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Alisema ilitokea majira ya saa 5 asubuhi kwa kuhusisha basi la
kampuni ya Metro, aina ya Scania lenye namba za usajili T 442 DFA.
Alitaja waliokufa kwenye ajali hiyo ni Elimringi Minja (50), Eziwa
Minja (47) na Haika Elimringi (12) ambao ni wa familia moja, Innocent
Shayo (49) mkazi wa Moshi na Zakaria Kitumpa (43) mkazi wa mjini Korogwe
mkoani Tanga.
Alisema basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Raymond Urio, mkazi wa
Kibamba, Dar es Salaam, lilipata ajali hiyo katika kitongoji cha
Zimbabwe Kata ya Manga wilayani Handeni katika barabara kuu ya Segera -
Chalinze.
“Baada ya basi kufika eneo hilo lenye kona, ghafla gari lilihamia
upande wa kushoto wa barabara na kutoka, ndipo dereva akajaribu
kulirejesha lakini bila mafanikio,” alisema.
Kamanda Mwombeji alisema; “Ndipo likamshinda kwa kuwa lilimvuta
upande wa kushoto wakati akijaribu kukata hiyo kona na ndipo likaangukia
kwenye bonde na kupinduka.”
Akizungumzia majeruhi 39, Kamanda huyo alisema 30 kati yao,
walitibiwa katika Kituo cha Afya cha Mkata na kuruhusiwa kurejea
nyumbani. Alisema wengine 9 hali zao sio nzuri.
“Majeruhi tisa bado wanatibiwa kwa sababu wameumia sehemu mbalimbali
za mwili na huenda baadaye wakalazimika kuhamishiwa katika hospitali za
wilaya za Handeni au Korogwe kwa matibabu zaidi kadri daktari
atakavyoona inafaa,” alisema.
Alisema dereva wa basi hilo, alitoroka muda mfupi baada ya tukio na
kwamba askari wanaendelea kumtafuta. Alisema uchunguzi kuhusu chanzo cha
ajali hiyo, unaendelea.
0 comments:
Post a Comment