Kocha wa timu ya Simba, Dylan Kerr, amesema tatizo linalokwamisha maendeleo ya soka la Tanzania ni kukosekana kwa wafungaji.
Muingereza huyo amesema kama timu mojawapo ya Tanzania ingekuwa na wamaliziaji wazuri, wangekuwa wanaona ligi nyepesi sana.
Akizungumza baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya African Sports kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga juzi, Kerr alisema: “Tatizo la Tanzania ni
wafungaji. Kama ukiwa na wafungaji wazuri ligi ingekuwa nyepesi sana.”
Simba ilipata ushindi wa kwanza na goli la kwanza Mkwakwani tangu
Agosti 24, 2011 kupitia Mganda Hamis Kiiza na Kerr amesema wachezaji
wake walicheza kwa kiwango cha juu licha ya tatizo katika umaliziaji.
Mchezaji wa mwisho kuifungia Simba Mkwakwani alikuwa Patrick Mafisango
katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union 2011.
“Nina furaha sana kwa ushindi huu ambao umevunja rekodi ya Simba
kutoshinda kwa miaka minne kwenye uwanja huu, nimefurahishwa na kila
wachezaji kwa kufanya kazi yake vizuri, Kiiza pia kwa kufunga bao pekee
na Majabvi kucheza vizuri nafasi ya ulinzi leo (juzi),” alisema Kerr.
Kocha huyo aliongeza ataendelea kuwaboresha washambuliaji wake ili waweze kufunga zaidi katika mechi zinazofuata.
“Siijui Mgambo, ila katika maandalizi tuliyofanya ilikuwa ni
kuimarisha timu kwa lengo la kupambana na yeyote atakayekuja, naamini
tutakuwa tofauti zaidi ya leo kwa sababu kila mchezo una mkakati wake,”
Kerr alisema.
Aliongeza kwamba anaahidi kasi ya timu yake itaongezeka na mechi ya keshokutwa Jumatano pia itakuwa na ushindani.
0 comments:
Post a Comment