TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekemea vurugu na
mauaji yaliyotokea wakati wa mikutano ya kampeni za vyama vya siasa
inayoendelea katika sehemu mbalimbali nchini.
Tume hiyo pia imesema inasikitishwa na lugha zinazotumiwa na baadhi
ya wagombea ambazo ndizo zimekuwa chanzo cha uchochezi na uvunjifu wa
amani wakati wa kampeni za urais, wabunge na madiwani zinazoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tume hiyo na kusainiwa na
Mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga,Tume yake ilipokea taarifa ya vurugu
kutoka katika vyombo vya habari kuhusu uvunjifu wa amani katika baadhi
ya maeneo hapa nchini.
Aidha, taarifa hiyo ilisema tume inasikitishwa kuona kampeni za
uchaguzi zilianza vizuri katika hatua za mwanzo za uzinduzi lakini sasa
hivi zinaingia dosari kitu ambacho ni kinyume na ni ukiukwaji wa haki za
binadamu.
Taarifa hiyo ilisema kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la vurugu
zinazotokea kutokana na wafuasi wa vyama vya siasa kuingiliana katika
mikutano ya kampeni ya vyama vingine na kusababisha vurugu, ama wafuasi
hao kupigana.
Taarifa iliongeza kuwa vurugu za hivi karibuni zimesababisha kifo cha
mtu mmoja na watu wengine kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga, pamoja na
kuharibiwa kwa gari la mgombea ubunge wa jimbo la Tarime Mjini, Esther
Matiko katika vurugu za vyama vya CCM na Chadema zilitokea kijiji cha
Mangucha, jimbo la Tarime Vijijini, Septemba 10, 2015.
Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa tume inasikitishwa na taarifa ya
vurugu zilizofanyika hivi karibuni wakati wa kampeni zilizofanyika
katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo majimbo ya uchaguzi ya
Kyela, Bunda mjini, Dodoma mjini, Dar es Salaam na Zanzibar.
Matukio haya yote yanaelezwa kukiuka haki za binadamu na utawala bora
pamoja na kwenda kinyume na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani ya Mwaka 2015 yaliyotiwa saini na vyama vya siasa.
Katika maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015, vyama vya siasa na wahusika
wake vinatakiwa kukataa na kulaani vitendo vya vurugu, fujo, chuki,
mafarakano, matumizi ya lugha za matusi na kejeli na kubeba silaha
yoyote inayoweza kumdhuru mtu wakati wa kampeni.
0 comments:
Post a Comment