HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imetumia zaidi ya Sh milioni 500
kupambana na kipindupindu tangu kilipozuka Agosti 15 mwaka huu.
Hadi sasa watu 1194 wameugua ugonjwa huo katika Manispaa hiyo na 17 wamefariki dunia.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa dawa na vifaa tiba
uliotolewa na Benki ya CRDB, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mussa Natty,
alisema kila siku kuna wagonjwa wapya wanaripotiwa na jana walikuwa 15.
Msaada huo wenye thamani ya Sh milioni 15 ulitolewa na benki hiyo
kupitia sera yao ya kurudisha faida kwa jamii katika Wiki Maalum ya
Huduma kwa Wateja inayoadhimishwa na benki hiyo kila mwaka.
“Ni gharama kubwa sana kumuhudumia mgonjwa wa kipindupindu, katika
kila nyumba anayotoka mgonjwa lazima tumwage dawa nyumba 10
zinazomzunguka, tumetoa sana elimu lakini hali bado si nzuri na kesho
(leo) tutakutana na wenyeviti wote kuangalia namna ya kudhibiti ugonjwa
huu,” alisema Natty.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, alisema Wiki
Maalum ya Huduma kwa Wateja itaadhimishwa Oktoba 5 hadi 11 mwaka huu
katika matawi yote ya benki hiyo Tanzania Bara na Visiwani.
Naye Herieth Faustine anaripoti kuwa katika Manispaa ya Temeke
wameripoti wagonjwa 211 huku Ilala kukiwa na wagonjwa 968, hali
iliyosababisha manispaa hizo kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula holela
ikiwa ni jitihada za kupambana na ugonjwa huo.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala, David Langa alisema jana kuwa
idadi hiyo imekuwa ikiongezeka na kwa jana walipokelewa wagonjwa 28
kutoka katika kaya tofauti ndani ya manispaa hiyo.
0 comments:
Post a Comment