Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias ameondolewa
kwenye kikosi cha waandishi wa habari wanaoandika habari za kampeni za uchaguzi
za mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kwa madai kuwa aliandika habari
isiyostahili.
Hii ni mara ya pili kwa CCM kumtimua mwandishi wa gazeti
hilo kutoka kwenye msafara wa mgombea wake wa urais. Mara ya kwanza ilikuwa
mwaka 2010 wakati ilipomtimua Midraj Ibrahim kwa kuripoti tukio ambalo chama
hicho kikongwe hakikupenda litangazwe kwenye vyombo vya habari.
CCM imesema imechukizwa na kitendo cha mwandishi huyo
kuripoti habari ya tukio la wanachama wa Chadema kumnyooshea alama ya vidole
viwili na kumzomea mgombea wa CCM wakati aliposimama Uyole, Mbeya.
Alama ya vidole viwili ni nembo iliyo kwenye bendera ya Chadema.
Elias amesema kuwa juzi mkurugenzi wa mawasiliano wa CCM,
Godfrey Chongolo ndiye aliyemweleza kwamba chama hicho kimesikitishwa na habari
hiyo, akidai kuwa kulikuwa na habari nyingi zaidi zinazomhusu mgombea huyo wa
urais.
Elias alisema alielezwa na Chongolo kuwa CCM imeshindwa
kuvumilia habari ya magufuli kuzomewa akisema haikustahili kupewa uzito.
Mkurugenzi huyo alimwambia mwandishi huyo kuwa alitarajia
kuona taarifa hiyo ikiripotiwa “Vijana wa Chadema wafanya fujo kwenye
mkutano wa kampeni wa Dk Magufuli.”
Kutokana na habari hiyo, Chongolo alimtaka Elias kutoendelea
kubaki katika kikosi cha waandishi kwa sababu anawaharibia katika vita
wanayopigana kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
“Unajua sisi tuko vitani, kwa hiyo unapoandika kwamba
Wanachadema walimzomea kwa kuonyesha vidole viwili juu, maana yake ni kwamba
hawamkubali mgombea wetu, sasa hapo unawaeleza nini Watanzania?”
“Siku ile ya tukio Magufuli alifanya mikutano ya barabarani
zaidi ya mitano, nashangaa ninyi mkaona ile ndiyo habari ya kuandika na kuacha
nyingine za maana,” alisema Elias akimnukuu Chongolo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa
kuhusu suala hilo alisema amesikia na baadaye akakata simu.
Akizungumzia uamuzi huo Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari
Machumu amesema kampuni imesikitishwa na hatua hiyo lakini haitakatishwa tamaa
katika kutekeleza majukumu yake kwa umma.
0 comments:
Post a Comment