MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema ana uhakika
wa kuingia Ikulu kwa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo,amewataka wanaomkosoa wawe wanajibu hoja kwa
kuwa yeye ana utaratibu wa kuwaeleza Watanzania atawafanyia nini baada
ya kuingia madarakani.
Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi kwenye
mkutano wa kampeni uliofanyika Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
“Naomba nitofautiane na Tundu Lissu ambaye amesema hapa, kwa kusema
ni lazima tuiondoe CCM madarakani kwa sababu hali yetu ni shwari kabisa.
“Nawatahadharisha waache, watu hao waache kusema uongo na kuwapotosha wananchi kwani matusi hayasaidii chochote.
“Nawaomba wajibu hoja za mendeleo, wao wanapiga maneno ya uongo kwa sababu ya kitu wanachotaka kukifanya.
“Kwa mfano, tumesema katika ilani yetu tutahakiki mikopo ya nje kwani
hapa Sumaye amesema kila Mtanzania ana mzigo wa mkopo wa nje wa
shilingi laki nane.
“Kwahiyo, hapa tunataka kujua hizo shilingi laki nane wanazodaiwa
Watanzania zilitumikaje ili zisije zikawa zilitumika kuzungukazunguka
duniani.
“Nawaambia waache kupiga kelele nyingi, watutayarishie maelezo tu,
maana lazima Ikulu tutaingia watake wasitake. Tutakapoingia tutawataka
vilevile wajibu hoja ikiwa ni pamoja na hili soko lenu la Kibaigwa
limefikia wapi,” alisema Lowassa.
Pamoja na hayo, alisema atakapoingia madarakani, Serikali yake
itatekeleza ahadi zote zilizoahidiwa huku ikiwaletea maendeleo ya kasi
Watanzania wote.
“Nchi yetu toka mwaka 1961 haijaondokana na umasikini na badala yake
umasikini unaongezeka kila siku. Kwahiyo sisi tutahakikisha kila mtu
anaishi maisha bora, na kama alikuwa akila mlo mmoja, ale milo mitatu,
kama alikuwa ana gari moja, awe na magari mawili, kama alikuwa na
baiskeli moja, awe na pikipiki, kama alikuwa anavaa kanga mbili, avae
tano.
“Tunataka maisha ya Mtanzania yawe ni ya mtu anayejiamini zaidi, na
tutamwezesha ajitegemee zaidi kwani kuna watu wametudanganya kwa miaka
mingi na wanafikiri umasikini ndiyo uongozi.
“Wanafikiri ukiwa kiongozi umasikini ndiyo unafaa, wanawadanganya,
huo ni uongo ndiyo maana mimi nauchukia umasikini na hakuna mtu
anayependa umasikini duniani.
“Naomba ruksa ya kwenda Ikulu nikawaonyeshe Watanzania namna ya kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Lowassa.
Pamoja na hayo, alizungumzia taarifa zilizosambaa nchini, kwamba
anamiliki shamba mpakani mwa wilaya za Kongwa na Kiteto ambapo alisema
hamiliki shamba lolote katika eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, alimtaka mwenye shida na shamba hilo, akalichukue kama anaamini ni mali yake.
“Wamekuja hapa wanasema mambo ya uongo, nataka niwaambie mambo
yafuatayo, kwamba ni uongo kwamba namiliki shamba na namiliki ardhi.
“Mtu ambaye anafikiri ardhi hii ni ya kwangu, kwa ruksa yangu namtaka
akachukue bure hilo shamba wanalosema ni la Lowassa, nawaruhusu
wakachukue bure.
“Nataka niwahakikishieni sina ardhi huko, na mimi siyo mwendawazimu,
kwahiyo anayesambaza uongo huo, akachukue hilo eneo liwe mali yake,”
alisisitiza Lowassa.
Wakati Lowassa akiyasema hayo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
alisema Serikali iliyoko madarakani ni dhaifu na kwamba udhaifu huo
unachangia uwepo wa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na hali hiyo, alisema kama Lowassa angekuwa madarakani,
migogoro hiyo inayosababisha mauaji ya wakulima na wafugaji isingetokea
kwa sababu ni kiongozi makini na anajua wajibu wake.
“Nawashangaa sana viongozi wetu, yaani watu wanauana mahali halafu waziri mkuu anakwenda kwenye tukio baada ya miezi sita.
“Huu ni udhaifu wa Serikali kwani mimi nilipokuwa waziri mkuu, siku
moja watu wawili waliuawa wilayani Kilosa kutokana na mgogoro wa ardhi
kati ya wakulima na wafugaji.
“Nilipopata taarifa, nilipanda helkopta mara moja, nikaenda huko na
mgogoro huo nikaumaliza, ingawa ulikuja kurudi baada ya kuondoka
madarakani.
“Enzi zangu pia kule Ukuryani makabila mawili yalikuwa yakiuana kwa
mishale, nikawaambia vijana waandae helkopta niende huko, wakasema
nisiende eti kwa sababu wataniua, mimi nilikataa, nikasema nitakwenda
huko kwa sababu nyinyi kazi yenu ni kunilinda mimi, na mimi kazi yangu
ni kuwalinda wananchi.
“Nilipokwenda huko, mgogoro huo niliumaliza kwa sababu nilikuwa
makini tofauti na Serikali yenu ambayo ni dhaifu. Kwahiyo kama Lowassa
angekuwa madarakani, nawaambia hiyo migogoro isingekuwapo, mpeni kura
awaongoze vizuri,” alisema Sumaye.
Pamoja na hayo, alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli
haipendi CCM ndiyo maana katika mabango yake anasema ‘Chagua Magufuli’
badala ya ‘Chagua CCM’ kama ilivyozoeleka.
Katika siku ya jana, Lowassa alihutubia mikutano katika majimbo ya Kibakwe, Mtera, Kongwa na Gairo na leo atakuwa mjini Dodoma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment