SERIKALI imefuta hati miliki ya mashamba makubwa manne ya wawekezaji mkoani Arusha.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa kunyang’anya viwanja, kama ilivyojitokeza
wiki iliyopita katika mikoa ya Morogoro na Pwani. Kutokana na uamuzi
huo, sasa mashamba hayo yatagawiwa kwa wananchi wenye uhaba wa ardhi,
waliojiorodhesha kutokana na migogoro hiyo.
Zaidi ya watu 2,000 wanatarajiwa kupata maeneo ya makazi na kilimo
mkoani Arusha. Katika mkoa wa Arusha, mashamba yaliyofutiwa hatimiliki
ni Tanzania Plantations Limited iliyokuwa na mashamba matatu na Shamba
la Noors lililopo kijiji cha Laroi na Kisima cha Mungu, Oljoro mkoani
hapa.
Kufutwa kwa mashamba hayo na serikali kutaondoa mgogoro wa muda
mrefu, uliokuwa unasababisha mapigano ya mara kwa mara na uvamizi wa
mashamba na wananchi hao, kwa kudai ardhi iliyokuwa inamilikiwa na
wawekezaji hao bila kuendelezwa.
Akizungumza jijini hapa, jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi alisema serikali imeamua kufuta miliki ya
mashamba hayo ili kuwapa wananchi waweze kugawiwa kihalali na kupimiwa
maeneo yao kwa watu, ambao hawana ardhi ambao waliainishwa hapo awali.
Alisema mashamba yaliyofutiwa hati hizo na Rais ni Tanzania
Plantations lenye hati NP 305, NP 304 na C.T.No 5189 yenye ukubwa wa
ekari 6,396 na ni mali ya serikali na stahili ya mwekezaji huyo ni
fidia. Lakini pia katika ufutaji wa mashamba hayo, mwekezaji ameachiwa
shamba lenye namba N.371 ambalo analimiliki kihalali.
Alisema serikali imeamua kutoa ekari 100 kwa ajili ya kuwasaidia
wananchi wenye uhaba wa ardhi na kilimo katika Halmashauri ya Meru.
Alisema baada ya ubatilishaji wa mashamba ya Tanzania Plantations Ltd na
ardhi aliyoitoa mwekezaji huyo kwa hiyari yake, Halmashauri ya Wilaya
ya Arusha imepata jumla ya ekari 6176.5 na Halmashauri ya Meru ekari 925
.
Alisema zaidi ya wananchi 2,000, watapata maeneo ya kujenga (makazi)
na kilimo. Alisema kazi hiyo itasimamiwa na timu ya wataalamu,
iliyoundwa kwa ajili ya kusimamia ugawaji wa maeneo hayo kwa wananchi
wenye uhaba wa ardhi.
Lukuvi pia alisema idadi ya watu wanaohitaji ardhi ni kubwa, lakini
wahusika watajua ni kina nani wana mahitaji ya ardhi kwani Halmashauri
ya Wilaya ya Arusha wananchi wanaohitaji ardhi kwa ajili ya makazi na
mashamba ni 2000 na Halmashauri ya Meru wananchi wanaohitaji ardhi kwa
ajili ya makazi na mashamba ni 2,891.
Alisema katika shamba la Noors ambalo linahusisha wananchi wa kijiji
cha Laroi na Kisima cha Mungu, awali mwekezaji aliridhia kutoa ekari 696
kutoka shamba lake lenye ekari 2,296. Alisema shamba hilo mpaka hivi
sasa linamilikiwa na mwekezaji kwa hati namba 14,294 ikiwa miliki ya
miaka 90 na miezi kumi kuanzia 1/7/1959, hivyo hati yake itaisha mwaka
2050.
“Kumbukeni huu ni utekelezaji wa ahadi za Rais. Kulikuwa na migogoro
mingi ya ardhi na hivi sasa mingi tumeshaitatua” alisema.” Aliongeza
kuwa, wiki iliyopita mashamba zaidi ya 7 wilayani Mvomero, yalifutiwa
umiliki wa ardhi, 10 wilayani Kibaha mkoani Pwani na hivi mashamba ya
watu wakubwa 10 yaliyopo Kilombero mkoani Morogoro yatafutwa hati miliki
zake.
Alisisitiza kuwa haiwezekani matajiri kula maisha mazuri wakiwa
mijini na kuyatelekeza au kuyakodisha kwa wazawa wasio na ardhi.
Alipotafutwa baada ya mkutano ili kufafanua vigogo waliohusika na
umiliki wa mashamba hayo, Lukuvi hakupatikana.
Wakati huo huo, serikali imefuta hati miliki za mashamba 48
yaliyokuwa yanamilikiwa na wawekezaji wilayani Monduli. Kwa mkoa wa
Manyara, Rais amefuta hati miliki ya shamba la Ufyomi Gallapo Estate,
lenye ukubwa wa ekari 120 ili kufidia wananchi 340 waliohamishwa kupisha
Hifadhi ya Tarangire.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment