MGOMBEA urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema yeye ndiye
anayetosha kupambana na umaskini wa wananchi huku Waziri Mkuu Mstaafu,
Fredrick Sumaye, akiitaka CCM ianze kuondoa hirizi Ikulu kama zipo kwa
vile Ukawa wanaingia madarakani.
Waliyasema hayo kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika wilayani Temeke Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Tungi Kigamboni, Lowassa alisisitiza lengo lake ni kupambana na umaskini.
“Nitaanza na elimu kutoka shule ya watoto wadogo hadi elimu ya juu
ambayo itakuwa ni bure… elimu ni muhimu kuanzia kwa mtoto mdogo hadi
elimu ya juu.
“Baada ya elimu kinachofuata ni kilimo cha kisasa cha umwagiliaji,
kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya mama lishe, wamachinga na
bodaboda , kufungua viwanda kwa ajili ya ajira kwa vijana.
“Mkinichagua baada ya kuapishwa nitaanza na kivuko cha feri
ambako wananchi mtavuka bure bila malipo yoyote,” alisema Lowassa.
Akiwa kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya Chanika Magengeni
wilayani Temeke, alisema anawashangaa baadhi ya watu wanaofuatilia
safari zake zikiwamo ziara zake sokoni na kwingineko wakati
wanaosafirisha wanyama hai nje ya nchi wakiwamo twiga, hawahojiwi.
Alisema hata alipopanda daladala baadhi ya watu walihoji kitendo
hicho lakini bado wamekuwa hawahoji waliopeleka twiga nje ya nchi.
Lowassa alisema kwa sasa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wamechoka kula mlo mmoja na kwamba wanahitaji maisha mazuri ambayo watayapata kwa kufanya mabadiliko.
Lowassa alisema kwa sasa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wamechoka kula mlo mmoja na kwamba wanahitaji maisha mazuri ambayo watayapata kwa kufanya mabadiliko.
“Wananchi wanahitaji mabadiliko na maisha mazuri, nina imani fedha za
kufanya haya yote zipo …tutatoa elimu bure kuanzia shule za watoto
wadogo hadi Chuo Kikuu kwa kuwa uwezo huo upo, kama fedha hamna mbona
mashangingi kila siku yanaongezwa?” alisema Lowassa.
Sumaye
Naye Sumaye alisema ni vema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijiandae
kuachia Ikulu na kama kuna kirizi kilizoweka kizitoe kwa sababu Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaingia madarakani.
“Kama kuna hirizi ama kitu kingine ambacho wamekisahau, sasa muda
umefika watoe kila kilicho chao kwa sababu Ukawa wanaingia madarakani,”
alisema Sumaye.
Alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ni sawa na mtu aliye
kwenye kitanda ambacho kina wadudu ikizingatiwa chama chake kilivyo
hivyo kumchagua ni kuendelea kupoteza mwelekeo wa maendeleo.
“Kitanda chenye wadudu kinachomwa moto, hivyo Magufuli anafananishwa
na kitanda hicho …kama vipi aje Ukawa akishindwa tutamtupa porini na
kitanda chake,”alisema Sumaye.
Sumaye alisema nchi ipo katika kipindi ambacho wananchi wenyewe wana
hiari ya kuamua kujikomboa au kubaki katika shida huku wana CCM
wakiendelee kushiba.
Alisema ana imani wananchi wanahitaji mabadiliko lakini kwa kuichagua CCM hakuna matumaini mbele yao.
“CCM lazima iondoke madarakani, haiwezi kuangalia afya ya wananchi …
ni aibu mno eti Dar es Salaam tunaugua kipindupindu ni aibu
sana,”alisema Sumaye.
Alisema anamshangaa Magufuli kudai eti nchi ni yake wakati hajapata ushindi na kuhoji endapo atapata ushindi wao wataishi wapi.
“Namshangaa Magufuli kusema nchi yake, je akishinda sisi wengine tutajificha wapi?” alihoji Sumaye.
Alisema pia kwamba CCM inatoa maneno ya vitisho kwa wananchi lakini
wao Ukawa hawasumbuki bali watafanya siasa ya amani na demoktasia.
Alisema watakaosababisha machafuko ni CCM kwa kukataa demokrnasia ya wanachi kwa sababu Ukawa wanahitaji amani.
Mgombea ubunge wa Kigamboni, Lucy Mageleli alisema Lowassa ni kama
Musa aliyekuja kuwakomboa watu wa Kigamboni kutoka utumwa wa CCM.
Alisema Serikali ya Lowassa ikiingia madarakani itahakikisha umaskini
kwa watu wa Kigamboni unaisha na Mungu atawapa nchi yenye asali na
maziwa.
“Wananchi kivuko siyo starehe ni sehemu yetu na ni haki yetu
hatutakiwi kukilipia, pia hayo magari ya Ridhiwani yanayoegeshwa hapo
kusubiri wamanchi tutakapoingia madarakani yataondoka na tutabakia na
daladala zetu za Buguruni, Mbagala na Gongo la mboto.
Duni
Naye mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma haji Duni, alisema taifa
linahitaji mabadiliko ya fikra kwa kupata elimu bora, nafasi mpya ya
kufikiri akisema CCM imeshindwa kutekeleza ahadi zake.
Alisema mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anataka urais
aliahidi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania lakini hali hivi sasa
imekuwa mbaya zaidi ya awali.
“Hata huyo Magufuli kwanza hatufai kwa kuwa yeye kila kitu anashangaa
tu kama ilivyo kwa mwenzake ambaye alikuwa anacheka twiga wanaondoka,
yeye anacheka… kila kitu yeye anacheka tu.
“Tunahitaji mabadiliko tena ya fikra … inatupasa kupata elimu hivyo
ni lazima kila mtu apate haki hiyo na Lowassa si mtu wa kuchekacheka,”
alisema.
Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wananchi
wamekubaliana kuwa mwaka 2015 wamechoka maumivu na wanachohitaji ni
mabadiliko tu.
“Wananchi wamechoka, wanahitaji mabadiliko na ndiyo maana hata sisi tumesimamisha mgombea mmoja tu wa Ukawa,”alisema Mbowe.
Akifafanua kuhusu mkanganyiko wa mgawanyo kwa wagombea katika kuwania
udiwani na ubunge katika Ukawa, alisema kauli ya wengi ni ya Mungu,
kwa pamoja walikaa na kuamua kumsimamisha mgombea mmoja kutoka chama
chochote anayekubalika katika kila kata na jimbo.
Mbowe alisema ili waende na kasi ya mabadiliko ni lazima wapate mgombea makini na anayekubalika kwa umakini wake.
“Natoa saa 48 kwa viongozi mbalimbali kufanya uamuzi wa kuwapitia
wagombea ambao wana sifa… awe wa chama chochote ili mradi wa ushirika
wetu na atakayekiuka haya tutamfukuza, hatuna haja ya
kubembelezana,”alisema Mbowe.
Hata hivyo, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuona umuhimu wa
kushughulikia kauli iliyotolewa na kiongozi mmoja wa CCM aliyedai CCM
kitaachia majimbo yote na kata lakini si Ikulu.
MABANGO
Wananchi hao muda wote walikuwa wakishangilia huku waionyesha mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali.
Baadhi yaliandikwa, ‘Toroka uje Ukawa ndiyo mpango mzima’, ‘Malofa
katika ubora wetu’, ‘Vijana Chanika tulitumika na CCM sasa zamu ya
Ukawa’, ‘Tumeikataa CCM jumla tunataka mabadiliko’, ‘Wazee wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki tusaidiwe’.
Mengine yalisomeka, ‘Magufuli huwezi kuitengeneza injini ya gari
ukiwa ndani ya gari bovu shuka uichungulie injini hiyo…hamia ukawa’.
Mengine yalisema, ‘Tunamchagua Lowassa kutoka UKAWA maendeleo
yatakuja’, ‘mchawi mpe mwana akulelee’, ‘heri Kipindupindu kuliko CCM’,
‘miaka 50 ya kudanganywa inatosha’, ‘M4C bado tuna imani na Lowassa
hatuyajali maneno mnayoyasema wembe ni ule ule’ na wengine walikuwa na
msalaba uliokuwa umeandikwa ‘John Pombe Magufuli kuzaliwa mwaka 1961
kifo 25, Oktoba 2015’.
0 comments:
Post a Comment