MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward
Lowassa, ameisimamisha tena Dar es Salaam kwa saa kadhaa huku akiwataka
Watanzania kutokosa usingizi kwani hakuna kura itakayoibwa.
Lowassa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti
alipokuwa kwenye mikutano ya kampeni Wilaya ya Kinondoni katika majimbo
ya Kawe na Kibamba.
Akiwa katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi,
Bunju A kwenye Jimbo la Kawe, alisema watu wasikose usingizi bali
wasubiri Oktoba 25 ifike.
Licha ya kwamba Lowassa alifika Bunju saa saa 9:25 alasiri, viwanja
hivyo vilianza kufurika watu kuanzia asubuhi kwani mkutano ulitarajiwa
kuanza saa 5:00 asubuhi.
Hali ilikuwa hivyohivyo kwenye Jimbo la Kibamba ambako licha ya
kiongozi huyo kufika katika eneo hilo saa 11:30 jioni, watu walianza
kufurika asubuhi, hali iliyofanya barabara ya Morogoro kupitika kwa
shida.
MSIKOSE USINGIZI
Akizungumza katika Mkutano wa Kawe, Lowassa alisema shaka dhidi ya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iliyopo sasa inatokana na jeuri ya
wapinzani wao.
“Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusu NEC… nawahakikishieni hawataiba ng’o, tuko imara, tutalinda kura zetu hadi zitakapohesabiwa.
“NEC na CCM hamtaweza kuiba kura zetu, Watanzania tukatae kuibiwa kura na kulaghaiwa,” alisema Lowassa.
Aidha Lowassa alisema kuna watu wa ofisini wanataka mageuzi, lakini
wanatishwa, na wengine ni wafanyabiashara wanaotaka kutusaidia.
“Hao wanaowatisha walie tu, hawawezi kumshughulikia mtu yeyote,” alisema.
Alisema atabadilisha mfumo wa utendaji kazi wa Serikali kutoka ulivyo sasa na kuwa wa kasi. “Itakuwa ni spidi 120”, alisema.
Aliendelea kusema: “Zimebaki siku 48, tukatae msongamano wa magari
Dar es Salaam, adha na tabu katika hospitali na vituo vyetu vya afya,
michango ya shule za sekondari na msingi, tatizo la maji na ajira.
“Fanyeni uamuzi mgumu tuibadilishe wizara ya elimu, tuwe na kilimo
cha kisasa na kuanzisha viwanda kwa ajili ya vijana wetu nchini,”
alisema.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alipanda jukwaani saa 9:55
alasiri na kuonya kuwa kama CCM haitakubali kushindwa inaweza
kusababisha machafuko.
“Nchi hii iko kwenye mfumo wa vyama vingi na ili viwe na maana lazima
kila chama kiwe tayari kushindwa kama hakijafanya vizuri, lakini CCM
hakitaki, hali hii ni hatari sana.
“Libya, Misri na Tunisia zimefika zilipofikia kwa sababu waliokuwa
kwenye madaraka walikuwa hawataki kuachia na kukandamiza watu. CCM
isipokubali mabadiliko itakuwa inataka yale ya Gadafi,” alisema Sumaye.
Alifananisha matusi yanayotolewa na wapinzani wao dhidi yake na Lowassa kuwa ni sawa na kumpiga teke chura.
“Wanatengeneza timu za kututukana, lakini nawaambia hapo ni sawa na
kumpiga teke chura. Lowassa alitoka serikalini miaka minane iliyopita na
tume ya Bunge ilisema hakukuwa na jambo lililomgusa moja kwa
moja…alijitosa ili kumuokoa rais na Serikali yake,” alisema.
Waziri Mkuu huyo pia aliibeza hoja ya mgombea urais wa CCM, Dk. John
Magufuli kuwa hataweza kupambana na rushwa kwa sababu tayari ameonyesha
udhahifu katika wadhifa aliokuwa nao wa Waziri wa Ujenzi.
“Utabadilishaje Tanzania wakati leo hii wewe ni waziri, lakini kwenye mizani kumejaa rushwa?
“Ataitoa wapi nguvu ya kupambana na rushwa, ndani ya CCM huwezi kufanya kitu chochote,” alisema.
Sumaye pia alisema kitendo cha kutoweka jina la chama katika mabango
ya mgombea urais wa CCM kinaonyesha kuwa ndani ya chama hicho hali ni
mbaya.
“Mabango yanasema “Chagua Magufuli” hayasemi “Chagua CCM”, kama anajua CCM haimpeleki kokote si angekuja Ukawa?
“Mimi niko Ukawa, lakini sigombei urais, kazi yangu ni kuwakomboa wananchi,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa “CCM ni shida”.
MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitamba kuwa wananchi wote wako tayari kufanya mabadiliko.
“Tumekwenda Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora na
leo (jana) tuko Dar es Salaam, nchi imeshalegea na iko tayari kwa sababu
ya Lowassa,” alisema Mbowe.
Huku akiwaelekeza wananchi kuzungusha mikono kama ishara ya kufanya
mabadiliko, Mbowe alionya kuwa kama machafuko, basi yataletwa na NEC
kutokana na kitendo chao cha kujaribu kuibeba CCM.
“Sasa hivi CCM haibebeki hata ukileta mbeleko, wanawatumia baadhi ya
watu kumchafua Lowassa, Sumaye na wote walioondoka CCM…wapuuzeni watu
wamefika bei,” alisema.
MDEE
Mgombea ubunge katika Jimbo la Kawe, Halima Mdee, aliomba idhini ya
viongozi wa chama hicho kufanya maandamano ya kuishinikiza NEC kuacha
kufanya hujuma.
“Tuna mashaka na zoezi linaloendelea la uhakiki, kuna watu
wanaandikisha vitambulisho vya vijana na kina mama, CCM na NEC wanataka
kufanya uhuni.
“Tunaomba kauli yenu kama ikibidi tuandamane hadi NEC tukakinukishe, tutafanya hivyo,” alisema Mdee.
Kwa mujibu wa Mdee,katika jimbo hilo wamefanikiwa kutatua migogoro
ya ardhi katika eneo la Chasimba na Nakerekwa, lakini bado kuna mgogoro
katika eneo la Boko kwa Sonji ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 20 na
katika eneo la Magereji lenye vijana zaidi ya 4,000.
“Mtaji wa vijana hawa wa gereji ni zaidi ya Sh bilioni tano na
wamekaa hapa tangu mwaka 2007, lakini leo hii wanaambiwa waondoke,”
alisema.
MWALIMU
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema CCM wameishiwa sera na sasa wanafanya matamasha ya burudani.
“Magufuli anazunguka nchi nzima kufanya matamasha ya burudani badala
ya kunadi ilani ya chama chake…ukiingia muachie wizara ya utamaduni,”
alisema Mwalimu.
KUWASILI UWANJANI
Maelfu ya wananchi walianza kuwasili viwanjani hapo saa 3 asubuhi na ilipofika saa 7 mchana uwanja ulikuwa umejaa.
Baadhi ya watu walilazimika kupanda juu ya miti na wengine kupanda
juu ya mapaa ya Shule ya Msingi Bunju A ili waweze kushuhudia matukio
mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika mkutano huo.
Waendesha bodaboda walikuwa ni kivutio pekee katika mkutano huo kwani
wengine walionekana kuendesha pikipiki kwa mbwembwe kubwa huku wakipaa
juu na wengine walikuwa wakizunguka uwanja huo mara kwa mara.
Baadhi ya watu walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kama
vile ‘Dk. Slaa kiapo cha kanisa kimekuponza uchizi unakunyemelea’ na
‘ulipo tupo’.
JIMBO LA KIBAMBA
Katika mkutano uliofanyika Jimbo la Kibamba kwenye Uwanja wa Mbezi
Mwisho, Lowassa alisema hana muda wa kubishana na wanachama wa CCM
wanaomtukana majukwaani, na kwamba watakutana katika sanduku la kura.
“Mahaba yananifanya nijiamini, ndiyo maana ndugu zangu
wanahangaika nikiwa na nguvu ya umma kama hii, nawaambia tukutane kwenye
sanduku la kura,” alisema.
Lowassa alisema endapo watu wanataka mabadiliko katika maeneo
mbalimbali ikiwamo elimu, wanapaswa kuandaa shahada zao na kuwapigia
kura wagombea wa Ukawa Oktoba 25.
Naye Sumaye alisema katika uchaguzi wa mwaka huu CCM lazima itoke madarakani hata kama haitaki.
“CCM hakitaki kutoka madarakani hata kama watu hawakitaki, wanatumia
hila zote, tunasema safari hii mtatoka tu ,mnahangaika kuchafua
viongozi, mnanihangaika hadi mimi ambaye sigombei,” alisema Sumaye.
Alisema kitendo cha wanachama wa CCM kujipanga na kumtukana hakisaidii badala yake kinamwongezea nguvu ya kupigania maendeleo.
Sumaye alisema alikihama chama hicho kwakuwa kimeshapoteza matumaini ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
MNYIKA
Mgombea ubunge Jimbo la Kibamba, John Mnyika, alimfanisha aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Samson wa kwenye Biblia
aliyedanganywa na Delila.
“Mnamfahamu Samsoni wetu? Alisema tumemchukua mtu chooni tukamwingiza
chumbani, amesahau kwamba yeye katoka chumbani ameenda chooni,
msiendelee kumsikiliza Samsoni, mpuuzeni hana jipya.
“Mzee wetu kadanganywa ameenda chooni kuwaunga mkono CCM,” alisema Mnyika.
Katika hatua nyingine, alimtaka Lowassa akiingia madarakani kuangalia
tatizo la maji ambalo ndilo kubwa ndani ya jimbo la Kibamba.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, aliituhumu CCM kuwa inatumia
Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) kukwepa kodi ya mafuta ili ikusanye Sh
bilioni 50 za kununua shahada za kupigia kura.
“Kuna mkakati wa kuitumia TRA kuingiza mafuta ambayo hayatalipiwa
kodi ili wapate Sh bilioni 50 kwa ajili ya kuwasaidia kununua shahada
za kupiga kura. Tunawaambia tumewabaini na waache mara moja huo mchezo,
tunataka watukabidhi nchi ikiwa na hazina ili tuweze kuleta mabadiliko
ya kweli,” alisema Mbowe.
Alisema anao ushahidi ju ya hilo na kuongeza kuwa CCM inaweweseka mwaka huu.
Home
News
Lowassa*Amwaga ahadi,asema hakuna kura itakayoibwa*Mnyika amfananisha Dk. Slaa na Samsoni, Delila.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment