UTAFITI mpya wa kampuni ya Ipsos (Synovate) unaonesha kwamba mgombea
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli atashinda kwa asilimia 62
dhidi ya asilimia 31 za mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, endapo
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ungefanyika leo.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo iliyotolewa kwa waandishi wa
habari Dar es Salaam jana, mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna
Mghwira angepata asilimia 0.3 huku asilimia 7 ya wapiga kura wakiwa
hawajui watampigia kura mgombea yupi miongoni wa wagombea wote wa urais
kwenye uchaguzi ujao.
Akitoa taarifa hiyo, Mwakilishi Mkazi wa Ipsos hapa nchini, Charles
Makau, alisema utafiti huo ulifanyika kati ya Septemba tano hadi 22
mwaka huu na umehusisha wananchi 1,836 kutoka mikoa yote ya Tanzania
Bara. “Zanzibar haikuhusishwa katika utafiti huo kutokana na sheria
zilizopo visiwani humo kuhusu masuala ya utafiti.
Utafiti ulifuata vigezo vyote vya kisayansi ingawa hatusemi kwamba
haya ndiyo matokeo yatakayotokea baada ya upigaji kura wa Oktoba 25
mwaka huu,” alisema. Huu ni utafiti wa pili katika kipindi cha wiki moja
ambapo taasisi inayoheshimika kwa masuala ya utafiti inatoa matokeo
yanayomwonesha Dk Magufuli kuwa mgombea anayeongoza.
Mapema wiki hii, taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo yaliyomwonesha
mgombea huyo wa CCM akiongoza kwa asilimia 65 dhidi ya asilimia 35
alizopata mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Lowassa ambaye pia anawakilisha umoja wa vyama vya upinzani vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Nchi (Ukawa).
Tofauti kubwa kati ya utafiti uliofanywa na Twaweza na Ipsos, ni
kwamba wakati ule wa kampuni hiyo iliyokuwa ikifahamika kwa jina la
Synovate huko nyuma ulifanyika kwa njia ya mazungumzo ya ana kwa ana,
ule wa Twaweza ulitumia mawasiliano ya simu za mkononi.
Makau alisema utafiti wa Ipsos ulibaini mambo mbalimbali yakiwamo
mambo matano yanayowakera zaidi Watanzania. Mambo hayo ni bei kubwa za
vyakula, mafuta na gharama kubwa za kuishi, masuala ya afya, chakula na
njaa, maji pamoja na elimu.
Katika sifa mahususi za wagombea urais; wananchi walitoa maoni yao
yanayoeleza ni nani wanadhani anaweza kutatua kero kuu zinazowakabili.
Dk Magufuli ameonekana kuaminika zaidi katika eneo la miundombinu,
ambako asilimia 44 ya waliohojiwa walisema wanaamini atafanya mambo
makubwa kwenye eneo hilo huku asilimia 26 wakiamini Lowassa anaweza
kufanya hivyo.
Lowassa ameonekana kumzidi Dk Magufuli katika eneo la vita dhidi ya
rushwa ambapo asilimia 27 ya waliohojiwa walisema mgombea wa Chadema
ataweza kupambana na tatizo hilo huku asilimia 26 wakisema Waziri huyo
wa Ujenzi ataweza kupambana na tatizo hilo.
Utafiti huo ulihoji pia ni kwa kiasi gani wananchi wanahisi wako
karibu na vyama vya siasa; ambako wale waliosema wako karibu na CCM
walikuwa asilimia 60, huku asilimia 29 wakisema wako karibu na Chadema,
asilimia 3 wakidai kuwa karibu na CUF huku asilimia moja wakisema wako
karibu na NCCR-Mageuzi.
Kwa upande wa jinsia, Magufuli ameonekana kukubalika na wanaume kwa
asilimia 51 huku Lowassa ikiwa ni asilimia 37 lakini kwa upande wa
wanawake, Magufuli anapendwa na asilimia 69 ya waliohojiwa huku asilimia
21 wakiwa wanampenda Lowassa.
Kama ilivyokuwa kwa utafiti wa Twaweza, Lowassa ameonekana kuwa
kivutio cha wenye elimu ya juu na wakazi wa mijini, huku Magufuli
akionekana kupendwa na wananchi wa vijijini pamoja na watu wenye elimu
ya wastani.
Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi hapa nchini, utafiti huu wa Ipsos
ndiyo utakuwa wa mwisho kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mnamo
Oktoba 25 mwaka huu. Sheria haziruhusu utafiti wa kisiasa kufanyika na
kutangazwa katika muda wa ndani ya siku 30 kabla ya kufanyika kwa
Uchaguzi Mkuu.
0 comments:
Post a Comment