HALI si shwari ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya
Chama cha NCCR-Mageuzi kuibuka na madai kuwa kuna vyama washirika
vinavuruga umoja huo, na kwamba chama chao kinaweza kufa baada ya
uchaguzi mkuu.
Ukawa ni umoja unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na
NLD ambavyo vimekubaliana kuungana katika uchaguzi mkuu na kusimamisha
mgombea mmoja kwenye urais, ubunge na udiwani.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa
Landmark Hotel jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti Bara wa
chama hicho, Leticia Mosore na Katibu Mkuu wake, Mosena Nyabambe
walisema hali hiyo inatokana na kukiukwa makubaliano mbal imbali
yaliyofanywa na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa.
“NCCR Mageuzi tulijitoa muhanga kweli kwa kukubali kuwaacha watu wetu
ili tu tujenge Ukawa iliyotakiwa, lakini sasa tumegundua Chadema
wanafanya mambo yao kivyao,” alisema Nyabambe na kuongeza kuwa hali hiyo
imewapa shaka kuwa huenda chama chao kitakufa baada ya uchaguzi.
Alisema tangu chama hicho kijiunge Ukawa, kimeendelea kudhoofika
tofauti na lengo la umoja huo ambalo lilikuwa ni kuimarisha vyama vyote.
“Uchaguzi wa 2010 tulisimamisha wagombea katika majimbo 67, lakini
sasa hivi tumepewa majimbo 12 tu…yaani tumerudishwa nyuma sana,”
alisema.
Nyambabe alisema Chadema wamekuwa wakiwafanyia fujo kuliko
wanavyofanyiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo hata majimbo hayo
waliyopewa bado wamewaingilia kwa kusimamisha wagombea wao katika
majimbo sita kinyume cha makubaliano.
Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Korogwe Mjini, Manyovu, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Kigoma Mjini na Kigoma Vijijini.
Hata hivyo, Nyambabe alisema msimamo wa chama chao ni kuendelea
kubaki Ukawa ili kuiondoa madarakani CCM na kuwataka viongozi wa umoja
huo kukutana na kurekebisha kasoro hizo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti, Mosore, alisema Ukawa ilianza
kukiuka makubaliano ya ushirikiano wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, na
sasa wanakiuka makubaliano ya Jangwani, waraka wa uteuzi wa madiwani na
waraka wa makubaliano juu ya wagombea ubunge ambayo yote yalisainiwa na
viongozi wa Ukawa.
Alimtupia lawama Mwenyekiti wao James Mbatia kuwa amekuwa msemaji wa
Chadema, huku akikisahau chama chake na kukiacha kikidhoofika.
Kutokana na hali hiyo, Mosore alitoa ushauri kwa mwenyekiti huyo
kuacha kuisemea Chadema na kuwa wanamtaka ahitishe vikao vya kikatiba
kujadili masuala hayo.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kuwapo kwa baraka za
Mwenyekiti Mbatia, katika kutoa malalamiko hayo pamoja na kujadili suala
hilo ndani ya chama, Katibu Mkuu, Nyambabe, alionekana kujiumauma na
kushindwa kutoa jibu la moja kwa moja kwa kudai kuwa suala hilo linahusu
Ukawa na si la chama.
“Kuhusu baraka za mwenyekiti, naomba mwelewe suala hili
tunailalamikia Ukawa na wala si chama chetu, na ndani ya chama
tumejadili mara nyingi na mwenyekiti,” alisema Nyambabe japo alishindwa
kuelezea msimamo wa mwenyekiti wake katika majadiliano hayo.
WAHUNI
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kauli za viongozi hao, Msemaji wa
NCCR-Mageuzi, Florian Rutayuga, alisema hazina baraka ya mwenyekiti wao,
Mbatia aliyesaini makubaliano ya Ukawa kwa niaba ya chama, hivyo
waliojitokeza mbele ya waandishi wa habari, wachukuliwe kama wahuni.
“Hao wahesabiwe kama wahuni, msemaji mkuu wa chama ni mwenyekiti, na
yeye ndiye aliyesaini makubaliano baina ya viongozi wa Ukawa, anajua
nani anapaswa kupata jimbo gani, kungekuwa na matatizo angesema,”
alisema Rutayuga.
Alisema kwa utaratibu wa chama chao, baada ya mashauriano na
Halmashauri Kuu ya chama, mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumza.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene,
alisema NCCR Mageuzi inapaswa kufuata taratibu za kuwakilisha malalamiko
kwa kuanzia katika vikao vya ndani ya chama chao.
“Mambo ya NCCR yanapaswa yatatuliwe ndani ya chama, wana fursa ya
kuyazungumza katika vikao vyao na baadaye wakakutana katika vikao vya
Ukawa yatajadiliwa, hakuna jambo ndani ya Ukawa linashindikana, likija
tutalitatua,” alisema Makene.
Mwingiliano wa wagombea ubunge wa umoja huo umekuwa ukijitokeza
katika maeneo mbalimbali nchini ambapo katika Jimbo la Mtwara mjini
mgombea mwenza wa urais chadema alimtangaza mgombea ubunge wa Cuf badala
ya yule wa NCCR aliyepitishwa na Ukawa na kuzua vurugu.
Juzi akiwa Nzega, Duni alilazimika kuwaomba wananchi wa Jimbo la
Nzega Vijijini kumchagua Dk. Khamis Kigwangala wa CCM baada ya kumkataa
mgombea wa CUF aliyepitishwa na Ukawa na kumtaka wa Chadema.
0 comments:
Post a Comment