MGOMBEA ubunge Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’,amejikuta katika wakati
mgumu baada ya msafara wake kushambuliwa na mawe na watu wanaodhaniwa
kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika vurugu hizo,watu wawili wamejeruhiwa akiwamo dereva aliyekuwa
akimwendesha mgombea huyo aliyejulikana kwa jina moja la Gabi, maarufu
kwa jina la DJ BBG, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Vurugu hizo pia zilisababisha gari aliyokuwa amepanda mgombea huyo kupasuliwa kioo cha mbele.
Vurugu hizo zilisababisha mgombea huyo ahairishe kuwahutubia wakazi
wa Kata ya Iziwa jijini Mbeya kwa muda, kutokana na kulazimika kuripoti
kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.
Tukio hilo la kushambuliwa kwa msafara huo, limetokea saa 11 za jioni
katika Kata ya Ghana – njia kuu ya kuelekea Kata ya Iziwa ambako
mgombea huyo alikuwa anakwenda kuomba kura kwa wananchi.
Wakati msafara huo ukiwa katika mwendo, ulifika katika eneo la Kata
ya Ghana, ambako kulikuwa na mkutano wa CCM wa kumnadi mgombea udiwani,
ndipo ghafla ulianza kushambuliwa kwa kurushiwa mawe.
“Wakati wafuasi wa CCM wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi
mgombea wao ngazi ya udiwani katika Kata ya Ghana, msafara wa sugu
ulipita katikati ya mkutano huo, hivyo kushindwa kuvumilia na kuanza
kurusha mawe huku wengine wakishikana kutaka kupigana,” alisema mmoja wa
mashuhuda wa tukio hilo.
Wakati mshikemshike huo ukiendelea, imeelezwa kuwa Sugu alitoa
taarifa polisi kuomba msaada ambapo askari walifika katika eneo la tukio
na kufanikiwa kutuliza vurugu hizo.
Baada ya polisi kuingilia kati, Sugu alikwenda kituoni na kuchukuliwa
maelezo na baada ya hapo aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake, lakini
gari yake T 161 CPP Toyota Land Cruiser VX aliyokuwa akiitumia katika
kampeni zake ilibaki polisi.
0 comments:
Post a Comment