HATIMAYE aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Yusuph
Makamba amefichua siri kuhusu sakata la Richmond kwa kile alichodai kuwa
Lowassa hakujiuzulu bali alifukuzwa na chama hicho kutokana na sakata
hilo.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Kawawa,Makamba alisema wakati akizungumza na wananchi mkoani Morogoro alisema
kwa kifupi kuhusu Lowassa kuihama CCM.
Makamba alisema hatua ya Lowassa kuhama CCM mwaka huu haikuwa kwa
mara ya kwanza kwani mwaka 1995 alitaka kuhama kutokana na kukosa urais
huku akisema kama anaona ni uongo ajitokeze.
Alidai kuwa mwaka 1995 Lowassa alionekana ana mali nyingi ambazo
alishindwa kuzitolea maelezo hivyo akaonekana hafai tatizo ambalo
limejirudia tena mwaka huu kabla ya kuhama CCM.
Makamba alisema Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alijitokeza
akamuuliza Rais Kikwete kuwa nani anahusika na Richmond ambapo alijibiwa
kuwa mhusika wanazunguka naye mikoani kumnadi kama mgombea urais
kupitia Ukawa pamoja na kumwombe kura.
“Lowassa hajawajibika kwa manufaa ya Watanzania na chama bali
alifukuzwa na CCM baada ya kuonekana kuwa anamiliki mali ambazo
haziendani na anachofanya ambapo alipotaka kuzitolea ufafanuzi aligoma,”
alisema.
Aliongeza kuwa shahidi wa hilo alikuwa ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Zitto Kabwe ambao walikwenda viwanja vya
Mwembeyanga, Temeke na orodha ya watu 11 ya mafisadi na ndani yake jina
la Lowassa lilikuwa namba tisa.
Makamba alidai kuwa mashahidi wengine wa suala hilo ni Anna Abdallah
na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela na kwamba
viongozi wa Ukawa wanapodai kuwa Lowassa ni msafi haitoshi kwani
wanasema amewajibika wakati alifukuzwa na CCM.
Alisema suala la Richmond lilipoibuka Kamati ya Uongozi ya CCM ya
wabunge wote wa Tanzania ilikaa wakaamua kuwa Lowassa amehusika hivyo
wakaenda kwa Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete na kumtaka amwondoe.
Makamba alifafanua kuwa walipofika mlangoni walikutana naye (Lowassa)
anatoka kisha wao wakaingia wakamwambia Kikwete kuwa hafai kwani
ameshiriki kwenye Richmond hivyo aondolewe kwa manufaa ya CCM.
Alisema Kikwete aliwajibu kama wamemuona hapo nje wakati anatoka
wakajibu ndiyo akawaambia amemjulisha kuwa anateua waziri mwingine hivyo
kesho yake Lowassa akawa analalamika kuwa anaonewa na CCM.
Hata hivyo, alisema anashangazwa na kuona Mwanasheria wa Chadema,
Lissu anampangusa mavumbi Lowassa wakati ndiye aliyekuwa anasema
mafisadi.
Alisema alipokuwa Morogoro alisema ataonesha mfano wa uongozi na
Sumaye aliogopa kwenda Mvomero kutokana na kuogopa kuzomewa huku akidai
kuwa kama ni tamaa ya fedha na utajiri Lowassa tayari ameonesha.
Aliongeza kuwa Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa wanapochagua Rais
hawaangalii sura, dini, ukoo bali wanapaswa kuangalia kama ni mwadilifu,
mchapakazi na kama anaweza na si kuangalia viongozi wanaoangalia
maslahi yao binafsi.
Makamba alisema Magufuli anaweza kuimarisha umoja na amani ya
Tanzania ambayo Rais ameiacha kutokana na maendeleo aliyoacha kwa miaka
10 ya uongozi wake kwa kulinda chama kwa maslahi ya taifa na chama kwa
ujumla.
“Kikwete ni mwana maendeleo kwa miaka 10 ya uongozi, amelinda chama
kwa manufaa ya nchi hivyo hakuna zawadi ya kumpa zaidi ya kumchagua
Magufuli ili kukipa heshima chama chake,”alisema.
Bulembo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi CCM, Abdallah Bulembo
alimtaka Lissu aache kucheza ngoma anayotaka, pia Lowassa ajitokeze
hadharani aseme kuhusu suala hilo.
“Ukawa wasiudanganye umma kuwa kura zitaibiwa ni uongo mtupu kutokana
na kila mtu amejinadi, Chadema mjipange Watanzania wameshaamua kuwa
Magufuli ndiyo rais na kama hawaamini wakaazime king’amuzi kwa jirani
ili waangalie kampeni za CCM zinavyofanyika mikoa mbalimbali
nchini,”alisema.
Magufuli
Kwa upande wake, mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli alisema amekuja
kuomba kura kwa wananchi ili kutengeneza Tanzania mpya yenye maendeleo
ambayo yatawagusa Watanzania wote, makabila, dini na vyama vyote kwa
kuwa maendeleo hayana chama.
Alisema Mji wa Kigoma miaka ya nyuma ulikuwa kama kisiwa, usafiri
ulikuwa treni hivyo ikikosekana hakuna kusafiri lakini CCM ilianza
jitihada kwa kutengeneza barabara za Uvinza na Ujiji lakini kuna
nyingine zinapaswa kuongezwa Kibondo na Kasulu.
Magufuli aliwahakikishia wana-Kigoma kuwa waziri wake atakayemteua
kuwa Waziri wa Ujenzi ambaye anasimamiwa na rais aliyekuwa waziri wa
ujenzi anamaliza barabara hiyo ili mji huo uwe mkubwa kama Dar es Salaam
na Mwanza.
“Kwa sababu nataka kutengeneza Tanzania mpya, natengeneza na Kigoma
mpya…Kigoma kuna madini yanayoitwa limestone ni kwa ajili ya kutengeneza
sementi hivyo tutajenga kiwanda cha sementi ili vijana wapate ajira
kupitia kiwanda hicho,”alisema.
Alisema wanatarajia kujenga uwanja mkubwa wa ngege kama mikoa mingine
ili nchi za jirani ziweze kutua ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa
biashara.
Magufuli aliwakikishia wana-Kigoma kuwa Kiwanda cha Chumvi Uvinza
kitaboreshwa ambapo ajira zitazalishwa ili kupunguza hali ya umaskini
kwa watu pamoja na kilimo cha tumbaku.
Alisema Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa mifugo hivyo wataanzisha
viwanda mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza viatu na mabegi ya ngozi na
kuwahakikishia kuwa Watanzania watanufaika na rasilimali zao, ikiwemo
madini.
M4C
M4C
Hata hivyo, Magufuli alisema M4C ya Chadema maana yake ni Magufuli
for change hivyo Watanzania wamchague kwani ataleta mabadiliko. Alisema
Mji wa Kigoma una matatizo ya maji hivyo atamaliza kesi hiyo kwa kipindi
ambacho ataingia madarakani.
Pia, aliwataka wananchi kutokitoa CCM madarakani kwani akiharibu
mmoja wasiadhibiwe wote kwani kipindi chake ni cha kazi na kutekeleza
anayoahidi.
“Watu wamezidi uongo kwani huwezi kusema kwamba ukichaguliwa utajenga
nyumba zote zilizo na nyasi, huo ni uongo kwani cha kufanya ni
kupunguza bei za vifaa vya ujenzi ili Watanzania wote waishi kwenye
nyumba za bati,”alisema.
Kabourou
Aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo miaka kadhaa iliyopita, Dk. Aman
Walid Kabourou alikataliwa na wananchi waliofika kusikiliza sera za
mgombea urais wa chama hicho.
Mlenda Nyanje mkazi wa eneo hilo alisema kuwa sababu za kukataliwa
kwa mgombea huyo ubunge ni kutokana na ubinafsi wake alipokuwa mbunge
kwa vyama tofauti miaka kadhaa iliyopita.
Akisimama mbele ya umati uliofurika katika Uwanja Kawawa mkoani humo,
alisema kuwa nia yake ya kuwania tena nafasi hiyo ni kutokana na
kuhitaji kuleta maendeleo ikiwemo kuzifanya manispaa kuwa majiji.
Aliomuomba Dk. Magufuli ampatie kilomita 50 ili aziwekee lami ambayo
itakuwa ni sehemu ya maendeleo. Licha ya kusema hayo wananchi
waliofulika waliendelea kumkataa kwa kuonesha mikono.
0 comments:
Post a Comment