WATU wasiojulikana wamechoma moto makanisa matatu ya Kipentekoste
katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, usiku wa kuamkia jana. Makanisa
hayo yaliyochomwa moto ni Pentecostal Assemblies of God (P.A.G)
lililoko eneo la Buyekera, kata ya Bukoba, Living Water International na
Evangelical Assemblies of God (E.A.G), yote yako katika eneo la
Kashura.
Akizungumzia tukio hilo, Mchungaji wa Kanisa la Living Water
International, Vedasto Athanas alisema saa 10 alfajiri alipigiwa simu na
jirani yake kuwa kanisa linaungua moto na kukimbia kwenda eneo la
tukio.
Mchungaji Athanas alisema baada ya kufika eneo la tukio alikuta moto
mkali ambao wasingeweza kuuzima na kuwa vitu vyote vilivyokuwa vimebaki
kanisani humo viliteketea kwa moto, ikiwamo viti 60, meza, benchi, vifaa
vya ujenzi na madhabahu.
Alisema hawajafahamu akina nani wamehusika na tukio hilo, lakini
alidai waliponusa baadhi ya vitu walisikia harufu ya mafuta ya taa, hali
iliyowafanya wahisi kuwa wachomaji walitumia mafuta ya taa
kuliteketeza.
Alisema kuwa hili ni tukio la tatu la kuchoma makanisa ya Living
Water International na kuwa kanisa la kwanza lilichomwa Septemba mwaka
2013 na jingine likachomwa Aprili 2014.
Kwa upande wake, Mchungaji Alistides Kabonaki wa E.A.G, alisema saa
11.50 asubuhi aliitwa na msichana wake wa kazi za ndani na kumweleza
kuwa kuna moto katika kanisa lao. Kabonaki alisema kuwa kanisa lake lote
limeteketea pamoja na mali zilizokuwemo na kuwa hajafahamu waliohusika
na uchomaji huo.
Alisema tayari wametoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa na Polisi na
kuwa wanasubiri hatua za kiuchunguzi za jeshi hilo ili kubaini
waliohusika na sababu za kufanya hivyo. Alisema kabla ya uchomaji huo
watu wasiofahamika walivamia kanisa lao na kuiba baadhi ya mali
zilizokuwemo ikiwamo viti na vitambaa vya madhabahuni.
Mwananchi ambaye ni jirani wa Kanisa la E.G.T, Regina Bakera,
akizungumzia tukio hilo alisema yeye kama muumini amesikitishwa na
matukio hayo na kuwa hawafahamu yanasababishwa na nini.
Bakera alisema matukio hayo yanadhihirisha kuwa kuna kikundi
kilichoandaliwa kwa ajili ya kuchoma makanisa na kuiomba serikali
kuyashughulikia kwa kufanya upelelezi wa kina. Kutokana na uchomaji wa
makanisa hayo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wachungaji katika Mkoa wa Kagera,
Crodward Edward alisema wamepanga kufanya maandamano ya kulaani kitendo
hicho.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera,
Augustine Ollomi alisema kwa sasa yuko safarini na kuwa atatoa ufafanuzi
kuhusu tukio hilo baadaye akisharejea Bukoba.
0 comments:
Post a Comment