Katika siku za karibuni kumeibuka tena taarifa za vurugu kati ya wakulima na wafugaji katika wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Hivi karibuni kulikuwa na taarifa za kuuawa ng’ombe 68 na kujeruhi
108 ikiwa mwendelezo wa mapambano kati ya wakulima na wafugaji kwenye
eneo hilo.
Kujirudia kwa vurugu hizi ni jambo la kusikitisha kwani linazua
maswali mengi kuhusu utendaji wa viongozi wa vyombo vya dola kwenye eneo
hilo.
Ugomvi kati ya wakulima na wafugaji kwenye eneo hilo ni wa miaka
mingi lakini katika hali ya kushangaza hakuna ufumbuzi wa kudumu juu ya
tatizo hilo.
Suala hili limeongelewa sana kwenye duru za serikali na hata vikao
vya Bunge lakini katika hali ya kushangaza kumekuwa hakuna ufumbuzi wa
mgogoro huu.
Mgogoro huu wa Mvomero haujaanza leo, ni wa miaka mingi, lakini
jambo linalosikitisha ni kuwa suala hili limekuwa likichukuliwa kisiasa
zaidi. Imetokea kila mara katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu
viongozi wanakuja na ahadi nyingi za kutatua mgogoro huo kati ya
wakulima na wafugaji.
Hata hivyo, viongozi hao wanapopewa dhamana husahau ahadi zao za
kumaliza mvutano na badala yake damu imekuwa ikiendelea kumwagika kwenye
eneo hilo.
Mgogoro wa Mvomero siyo pekee hapa nchini, kwani kumekuwa na
mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji kwenye maeneo
mengine mbalimbali.
Mathalani, katika wilaya ya Kilosa ambayo iko mkoani Morogoro na pia Kiteto, mkoani Manyara na Handeni mkoani Tanga.
Kushindwa kupatiwa ufumbuzi kwa migogoro hii kunadhihirisha jambo
moja tu kuwa kuna udhaifu mkubwa wa kiutendaji miongoni mwa viongozi
waliopewa dhamana ya kuongoza maeneo hayo.
Haiwezekani eneo lenye mkuu
wa mkoa au wilaya, makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya na watendaji
wa kuajiriwa wa serikali wanashindwa kupata dawa ya matatizo hayo.
Jambo moja ambalo linafanya watu wajiulize maswali mengi ni kuwa,
serikali haina dhamira ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo haya au ni
uzembe wa utendaji wa viongozi wa maeneo hayo.
Ifike wakati sasa kwa
viongozi wa kisiasa na serikali kuhakikisha wanakuja na majibu ya
kutatua matatizo hayo.
Serikali inapaswa kuja na sera inayoeleweka juu ya masuala ya ardhi
na hasa sheria na kanuni za kuendesha sekta za kilimo na ufugaji.
Lazima kuwapo na sheria za kulinda wakulima na mazao yao, lakini pia kwa
upande wa wafugaji pawekwe taratibu za kuwaongoza.
Kwa mfano, suala la
wafugaji kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kutafuta malisho ya
mifugo linapaswa kuwekewa utaratibu wa kitaifa.
Kitu kikubwa kinachokwamisha ni kuwa viongozi wachache wenye tamaa
wamekuwa wakinufaika na migogoro hii aidha kwa kushirikiana na wakulima
au wafugaji.
Bila kuwekwa kwa utaratibu ni ndoto kwa migogoro hii kumalizika na
badala yake damu itaendelea kumwagika kwa kuwa hakuna ufumbuzi.
Ni fedheha kubwa kwa nchi kama Tanzania inayojivunia kuwa ina amani
na utulivu wakati kuna wananchi wake wanauana kwa migogoro ya ardhi.
Serikali lazima ije na ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hii ili
kuhakikisha kuwa maeneo yenye vurugu watu wake wanaishi kwa amani na
kuendesha shughuli zao na hili litafanikiwa ikiwa viongozi na vyombo vya
dola vitatimiza wajibu wao ipasavyo.
0 comments:
Post a Comment