KWA vijana wa mjini, wanaweza kusema kwamba alichofanya Dk.
Willibrod Slaa juzi kwa kuachana na siasa na kurusha tuhuma kwa chama
chake, ni sawa na kumwaga ugali, na majibu aliyotoa mkewe wa kwanza,
Rose Kamili jana, ni sawa na kumwaga mboga.
Mke huyo aliyedai kutelekezwa na Dk. Slaa mwaka 2010 pamoja na
watoto, alisema kiongozi huyo ni mwongo na ni dhaifu kwa wanawake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rose alisema
ameshtushwa na kauli zilizotolewa na Dk. Slaa, na hasa zile
zilizoelekezwa kwake moja kwa moja na familia yake.
Rose ambaye ni mke wa ndoa wa kiongozi huyo wa zamani wa Chadema,
alisema kauli Dk. Slaa kuwa familia yake imekuwa ikishindia mihogo kwa
sababu ya kuhangaikia na Chadema, ni kiashiria cha uongo wa wazi.
“Siwezi kusema kwamba mihogo ni mibaya kuliwa, lakini napenda kukiri
kwamba katika maisha yetu niliyokaa na Dk. Slaa kuanzia mwaka 1986,
sikuwahi kushuhudia familia yetu ikila mihogo kwa sababu ya kukosa
chakula kama alivyosema kwenye hotuba yake,” alisema.
Aliongeza kuwa hata kauli yake kwamba Serikali ilimwekea pingamizi
ili asifunge ndoa na mchumba aliye naye sasa, Josephine Mushumbusi, ni
uongo kwani ni yeye ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwa sababu ni mkewe
rasmi wa ndoa.
“Jambo la kujiuliza hapa ni kwamba tangu lini Serikali ikaweka
pingamizi wakati aliyepinga ni mkewe. Ukweli ni kwamba mimi ndiye
niliyeweka pingamizi hilo ili kunusuru kunyang’anywa nyumba na hatimaye
kuhangaika na watoto,” alisema.
Kuhusu kauli ya Dk. Slaa kwamba anamchukia Lowassa na hajazungumza
naye kwa muda mrefu, Rose alisema waziri mkuu huyo wa zamani, ndiye
aliyemshauri kuhamia Chadema mwaka 1995 na kugombea ubunge wa Karatu
baada ya jina lake kukatwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
“Nakumbuka wakati tukizungumzia suala hilo ilikuwa jioni na
tulikwenda nyumbani kwa Lowassa, Monduli baada ya jina lake kukatwa na
CCM, ndiyo akamshauri kuhamia chama kingine, sasa hizo chuki zinatoka
wapi?” alisema na kuhoji.
Kuhusu Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Rose alisema pia ni
uongo mwingine kwa sababu wawili hao walipigiana simu na kufanya
mazungumzo wiki iliyopita.
“Kwanini aonyeshe chuki na watu wakati sisi ametutelekeza kwa muda
mrefu, lakini tumekuwa tukimlinda? Sasa inashangaza ni kwa nini padri
huyu mstaafu anaonyesha chuki kwa wengine,” alisema.
Aidha Rose pia alionyesha kusikitikia hatua ya mumewe kuzusha maneno
ya uongo kwa viongozi wa dini, akiwatuhumu kuhongwa zaidi ya shilingi
milioni 60 na Lowassa ili wamuunge mkono.
Pia alisema kumuhusisha Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, kwamba ndiye alimleta Lowassa Chadema ni kichekesho kwa
sababu muunganishaji mkubwa wa suala hilo ni yeye (Dk. Slaa) ambaye
anasali katika kanisa hilo.
Uongo mwingine alioutaja mkewe huyo wa ndoa ni kuhusu kukataa kwake
kutojiandaa kuwania urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
wakati inajulikana kuwa alikuwa akifanya maandalizi ndani na nje ya nchi
kwa ajili ya suala hilo.
Rose aliendelea kubainisha kuwa tatizo kubwa la mumewe ni kuzungumza
mambo kwa kukurupuka na kutokuvumilia, na hata kudiriki kutoa siri za
viongozi wenzake waliokuwa wakimtaka arudi ofisini.
“Aliniambia kwamba alikuwa akifuatwa na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana aliyemuahidi kwamba iwapo atakaa kimya atateuliwa
kuwa mbunge na baadaye kuwa waziri, akaniambia Rais Kikwete alimuahidi
kumpatia ubalozi, ikiwamo na kuitwa na Kardinali Pengo ambaye hakusema
walizungumza jambo gani.
“Maneno hayo nimekuwa nikiyapata kutokana na tabia ya Dk. Slaa kwa
kutokuwa na mdomo na ulimi usiokuwa na mfupa, hivyo kila jambo
analoelezwa huwa analiweka wazi, na inawezekana safari aliyokwenda
Afrika Kusini baada ya kumalizika kikao ndiyo kaelekea Ubalozi wa Afrika
Kusini,” alisema Rose.
Rose alipasha kwamba Dk. Slaa ambaye amekuwa akimfahamu, amekuwa
tofauti na huyu aliyemsikia akizungumza kwenye mkutano ule na hilo
limetokana na udhaifu mkubwa alionao kwa wanawake.
“Dk. Slaa siye ninayemjua, anaonekana anaendeshwa na mwanamke aliye
naye na ndiyo maana hata alikubali kumleta Lowassa kwa asilimia 80,
lakini alipofika nyumbani alibadili msimamo baada ya kulazwa nje ya
nyumba yake,” alisema.
Rose ambaye ni mbunge wa viti maalumu (Chadema) aliyemaliza muda
wake, alisema amekuwa akiwasiliana na mumewe huyo kwa muda mrefu, na
hata alipopata taarifa za kugoma kwenda ofisi za Chadema, wanawe
walikwenda nyumbani kwa Dk. Slaa kumjulia hali.
“Cha kushangaza ni kwamba watoto walivyofika nyumbani kwake walibisha
hodi, lakini walizuiliwa ndipo babu yao (baba yake Dk. Slaa) ndiye
alitoka na kuzungumza nao nje ya geti huko JKT Mbweni,” alisema Rose
aliyeambatana na watoto wake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment