SERIKALI imekionya Chama cha Tanzania Peoples (TPP) kuacha mara moja
kujishughulisha na shughuli za kisiasa kwa sababu hakina usajili na
kuendelea kufanya hivyo kinavunja sheria.
Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari jana, Msajili
Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema vyama
vilivyosajiliwa ndivyo vinavyopaswa kuendelea na shughuli mbalimbali za
kisiasa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema hadi sasa ofisi yake inavitambua vyama 22 ambavyo
vimekamilisha usajili na vina sifa zote ambapo TPP haitambuliki na
ilifutiwa usajili tangu Machi 20, mwaka 2002 kutokana kupoteza sifa
ikiwamo kukosa viongozi wa kitaifa.
“Chama cha TPP hakitambuliki na hakipo kwenye orodha ya vyama vyetu
kutokana na kukosa sifa na wanachama na viongozi waliokuwapo, awali
walipewa taarifa,” alisema Nyahoza.
Alisema TPP ilisajiliwa rasmi mwaka 1993, lakini kutokana na sababu
mbalimbali ilishindwa kufikia matakwa ya vyama vya siasa na msajili
aliamua kuiondoa kwenye orodha yake.
Nyahoza alisema kabla ya kufutiwa usajili, taratibu mbalimbali
zilifuatwa ambapo pamoja na chama hicho kujitetea, utetezi wao haukuwa
na mashiko na waliamua kukiondoa katika orodha ya vyama vya siasa.
Alisema kutokana na kufutiwa usajili huo TPP hawakushiriki uchaguzi
mkuu wa mwaka 2005 na hata ule wa 2010, hivyo wanashangaa kuibuka sasa
na kudai wao hawatambui kufutiwa usajili.
“Kwa niaba ya Msajili Jaji Francis Mutungi, napenda kuwatahadharisha
wanasiasa na baadhi ya vyama vinavyoibuka kuacha kuvunja sheria na
kuheshimu sheria zilizopo chini ya msajili,” alisema Nyahoza.
Alisema wahusika waliosajiliwa na ofisi ya msajili ndio wanaoruhusiwa
kuendelea na kampeni ambazo ni za kistaarabu na zenye amani.
“TPP hakipo kwa mujibu wa sheria, kifungu cha 7 (3) cha sheria ya
vyama vya siasa sura ya 358 kinakataza taasisi kufanya kazi kama chama
cha siasa bila ya kusajiliwa na msajili wa vyama,” alisema Nyahoza.
Pia alisema kifungu cha 8 (b) cha sheria ya vyama vya siasa kama
ilivyorekebishwa mwaka 2009 kinakataza mtu yeyote kufanya shughuli za
kisiasa kwa jina la chama ambacho yeye si mwanachama.
Akizungumzia kuhusu kampeni zinazoendelea hivi sasa, alisema ofisi
yake inaendelea kushughulikia matamko ya gharama ya uchaguzi ambapo
wakurugenzi husika wanaendelea kukusanya fomu kwa vyama mbalimbali.
Alisema hadi sasa vyama vyote vilivyopo kwenye usajili vinaendelea
vizuri, lakini alivitahadharisha kuacha matumizi ya lugha chafu.
Alivitaja baadhi ya vyama vinavyotambuliwa kuwa ni Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Chama cha NCCR – Mageuzi, Demokrasia Makini
(MAKINI), Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), Chama cha Kijamii (CCK) ,
Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), na vingine.
Home
News
Msajili acharuka akionya Chama cha Tanzania Peoples (TPP) kuacha mara moja kujishughulisha na shughuli za kisiasa
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment