Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, amelazwa
katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitalini hapo kwa ajili ya
kupata matibabu.
Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa wauguzi wa zamu katika
kitengo hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai siyo msemaji wa
mgonjwa huyo wala hospitali, alisema Marando alifikishwa hospitalini
hapo juzi akiwa na hali mbaya.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa watu wa karibu na Marando hali
yake inaleta matumaini ikilinganishwa na alivyofikishwa hospitalini hapo
juzi.
“Alifikishwa hapa jana usiku (juzi), mimi sikuwapo ila hali yake
ilikuwa mbaya lakini kwa mujibu wa ndugu zake amboa ndiyo wako naye hapa
wanasema anaendelea vizuri ikilinganishwa na juzi,” alisema.
Alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya hawawezi kuruhusu
waandishi wa habari kuchukua taarifa yoyote na kwamba hata mke wake
amekataa kutoa taarifa za mume wake hadi hapo atakapopona.
“Hata mkienda hamuwezi kuongea naye chochote na tangu asubuhi
ukimuuliza kitu anakuangalia tu na anapotaka kuzungumza anabaki anaguna,
kwa hiyo kwa hali yake hawezi kuzungumza,” alisema muuguzi huyo.
Alisema wanamatumaini hali ya Marando itakuwa nzuri zaidi baada ya
siku mbili kwani kuna dawa wamempatia ambazo zinahitaji apumzike.
“Unajua hawa wanasiasa wanakosa muda wa kupumzika kutokana na kazi
zao na hata hapa tunamuona anahamu ya kuzungumza chochote lakini hawezi
kutokana na hali yake ndiyo maana tunataka apumzike zaidi,” alisema.
Naye mmoja wa ndugu wa Marando ambaye pia hakutaka kujitambulisha
jina lake, alisema mwanasheria huyo aliugua gafla akiwa nyumbani kwake
juzi usiku.
“Jana mchana hadi jioni (juzi) nilikuwa naye lakini nilishangaa
kupigiwa simu usiku kuelezwa kuwa aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na
hata hivyo hatujaweza kuzungumza naye zaidi ya kupewa taarifa za hali
yake na mke wake,” alisema ndugu huyo.
Alisema tangu wamempeleka hospitalini hapo bado hali yake ni mbaya ingawa anaendelea na matibabu.
Aidha, NIPASHE lilishuhudia ndugu jamaa na marafiki wa Marando
wakiwa nje ya jengo hilo wakisuburi kupata taarifa ya mgonjwa huyo.
Sababu za ndugu hao kuishia nje zilielezwa kuwa ni kutokana na hali ya Marando kutohitaji usumbufu wa watu kuingia wodini.
Miongoni mwa ndugu waliokuwa hospitalini hapo ni mama mzazi wa
Marando ambaye alikuwa amekaa nje akisubiri taarifa ya hali ya mwanaye.
Mtu mwingine wa karibu na Marando ambaye hakutaka kutaja jina lake
alisema, aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa hospitali ya
kwanza ambayo hata hivyo hakutaja jina na baada ya kumpatia huduma ya
kwanza walisema hawawezi kumtibu na hivyo kuhamishiwa Hospitali ya
Muhimbili.
“Hapa hospitali walimleta usiku akaanza kupatiwa matibabu na hali
yake ilikuwa mbaya lakini baada ya kupatiwa matibabu inaendelea vizuri
kidogo,” alisema.
Kwa upande wa mke wake ambaye pia hakutaka kujitambulish jina alisema kuwa, hawezi kuzungumzia hali ya mumewe bila ridhaa yake.
Mkewe huyo alitoka wodini majira ya saa 11:00 jioni na kuwapatia
ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamesimama nje ya jengo hilo taarifa
ya hali ya mumewe.
Alisema ni kweli mumewe ni mgonjwa lakini taarifa ugonjwa wake ataitoa mwenyewe.
“Ni kweli mume wangu ni mgonjwa lakini siwezi kumzungumzia bila
kibali chake na kuna waandishi wengine wamekuja sijawapa taarifa. Huyu
ni mwanasiasa na mnafahamiana, akipona tu atazungumza mwenyewe kila
kitu,” alisema na kuondoka eneo hilo.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Steven, alithibitisha kupokelewa Marando hospitalini hapo juzi saa 4:00 usiku.
“Ni kweli Marando kalazwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anapata
matibabu lakini taarifa kamili ya ugonjwa wake unaweza kuipata kwa
mwenyewe wodini au kwa ndugu,” alisema Steven.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hana taarifa ya kuugua kwa Marando.
“Sina taarifa hizi na ndio kwanza ninazisikia kutoka kwako,” alisema.
Marando ambaye ni mwanasheria mkongwe nchini, alishawahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki .


0 comments:
Post a Comment