Kuna taarifa za kusikitisha kuwa mahujaji watano kutoka Tanzania ni
miongoni mwa waliofariki katika tukio la mkanyagano kwenye Mji
Mtakatifu wa Makka, nchini Saudi Arabia.
Kwa ujumla, watu 717 wameripotiwa kufa na wengine zaidi ya 800 kujeruhiwa katika tukio hilo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa jana ilieleza kuwa Watanzania hao walifariki wakati
wakiendelea na ibada ya Hijja kwenye eneo la Mina, ndani ya Mji
Mtakatifu wa Makka.
Hakika, huu ni msiba mkubwa. Sisi tunaungana na Watanzania wengine
kuwapa pole wafiwa na pia kuwatakia kheri wote waliojeruhiwa ili
wapate nafuu haraka.
Ni imani yetu kuwa serikali yetu, kwa kushirikiana na Saudi
Arabia, itaendelea kufanya kila linalowezekana ili taarifa kamili
ziendelee kupatikana kuhusiana hatima ya mahujaji wetu. Taarifa
zilizopo ni kwamba mwaka huu, Watanzania takriban 2,700 wamekwenda
kutekeleza ibada hiyo muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo. Mbali na
kwenda kuhiji Makka, nguzo nyingine kati ya tano za Uislamu ni kutoa
shahada, kusimamisha swala, kutoa zaka na kufunga (swaumu) Ramadhani.
Sisi tunaamini kuwa muhimu zaidi kwa sasa ni kwa kila mmoja
kuendelea kuwaombea mahujaji wetu waliosalimika ili mwishowe warejee
nchini wakiwa bukheri wa afya.
Aidha, ni muhimu pia kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili
awajaalie pepo yenye daraja ya juu mahujaji wetu waliopatwa na umauti,
hasa kwa kutambua kuwa kilichowapeleka Makka siyo kitu kingine bali ni
kujinyenyekeza mbele za Allah (Mwenye Mungu) ili mwishowe wapate radhi
zake.
Katika kipindi hiki, ni imani yetu kuwa ndugu, jamaa na marafiki wa
marehemu watajitahidi kuwa na subira kadiri wawezavyo. Ni kwa sababu,
kwa mujibu wa mafundisho, kila nafsi itaonja umauti. Na hili
lililotokea ni sehemu ya mtihani ambao siri ya kufaulu kwake
kwategemea kiwango cha subira kwa kila mmoja wao.
Pamoja na yote, tunaamini kuwa baada ya shughuli za uokoaji na
mazishi kukamilika, serikali ya Saudi Arabia itahakikisha kuwa
uchunguzi wa kina unafanyika ili mwishowe kubaini chanzo cha
mkanyagano na kuchukua hatua sahihi za kuzuia majanga ya aina hii.
Kinachotakiwa kuangaliwa na waandaaji ni taratibu za kutoa fursa
kwa kila hujaji kutekeleza ibada ya Hijja akiwa salama. Rekodi
zinaonyesha kuwa vifo vya aina hii vimewahi pia kutokea mara kadhaa
hapo kabla katika tukio hilo linalokutanisha watu wengi zaidi kwa
wakati mmoja duniani, huku mwaka huu likihusisha mahujaji takriban
milioni mbili.
Kwa mfano, mwaka 1990 walikufa mahujaji 1,426, mwaka 1994 (watu
270) na pia mwaka 2006 walikufa watu 360. Hali hii inapaswa kuzuiwa kwa
kupitia upya taratibu za kuwezesha waumini kutekeleza ibada hii
muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo.
Mungu awalaze pema peponi mahujaji wote waliotangulia mbele ya haki.
0 comments:
Post a Comment