Image
Image

Nec yatoa onyo kwa Lowassa kuhusu udini*Yasema chama kitakacho kiuka mashariti kuzuiwa kampeni zake.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU KUTUMIA MAJENGO YA DINI KUOMBA KURA NA SHUTUMA DHIDI YA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mara nyingine inawakumbusha wagombea na Vyama vyao kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambayo walikubali kuyafuata.Waliotia saini tarehe 27/7/2015.

Inasikitisha kuona kiongozi au mgombea anatumia madhabahu kufanya kampeni na mbaya zaidi kuomba kura kwa misingi ya kidini.  Kitendo kilichofanywa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh. Edward Lowassa kuomba Kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye hakikubaliki kwani kinawagawa Watanzania na kuwapa muelekeo wa kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa kifungu cha 2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015. “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya Udini, Ukabila, jinsia au rangi.”

Aidha, Tume inavikumbusha Vyama vya Siasa kuzingatia kifungu cha 2.1(k) cha Maadili kinachoelekeza Vyama au Wagombea kutotumia majengo ya Ibada kufanya kampeni, na pia Vyama au Wagombea kutowatumia viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya Vyama vya Siasa au wagombea wao.

Tunatumia fursa hii tena kuwaasa viongozi wa madhehebu yote ya dini kutoruhusu Vyama au Wagombea au Wanachama wa Vyama vya Siasa kutumia nyumba za Ibada kufanya kampeni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mbali ya hilo Mh. Lowassa na Viongozi wengine wa CHADEMA  wamekuwa na kauli za kuwaogofya wananchi kuwa ‘kura zitaibiwa’ na kwamba Tume itasababisha machafuko bila kutoa ufafanuzi jambo ambalo ni hatari. 

Kauli hizo zinashangaza na kustaajabisha na ni kauli za hatari sana kipindi kama hiki,  kwa sababu kwa mujibu wa maelekezo kwa Vyama vya Siasa na wagombea, ambayo wagombea wote na Vyama vya Siasa walipewa,  yana maelekezo kuhusu utaratibu mzima wa kupiga  na kuhesabu Kura katika ngazi ya kituo, kujumlisha Kura katika ngazi ya Kata, Jimbo na Taifa.

Taratibu zote hizo hushuhudiwa na Mawakala wa Vyama vya Siasa na Wagombea ambapo kura zikihesabiwa ngazi ya kituo, Mawakala hupewa nakala ya matokeo katika fomu Na. 21A Kura za Urais, 21B Kura za Mbunge na 21C Kura za Udiwani.

Katika ngazi ya Jimbo hesabu ya kura za kila kituo zilizopo pia katika nakala la Fomu 21A za Urais na 21B za Mbunge hujumlishwa na matokeo kujazwa katika fomu 24A kwa Rais na 24B Mbunge na Nakala ya matokeo wanapewa mawakala wa Vyama na Wagombea waliopo katika kituo cha kujumlishia kura ngazi ya Jimbo.

Katika ngazi ya Taifa, Tume hujumlisha matokeo ya kura za Rais mbele ya wagombea na mawakala wa Vyama na kutangaza matokeo.Katika hali hii itabidi waeleze wizi unafanyika wapi?

Tatu jana,Mhe.Freeman Mbowe naye amesema kuwa Tume inaegemea Chama Tawala.Hivyo itasababisha uvunjifu wa amani.Hili nalo ni tamshi lisilo la ukweli kabisa.Wakati wote Tume haiegemei wala kupendelea chama chochote katika kazi zake Mhe.Mbowe anajua hivyo Chaguzi zote Tume imefanya kwa kutegemea Kura halali zote na ndiyo maana hata Wabunge wa Vyama vingine walitangazwa.Viongozi,wote hasa wakuu wanaogombea Urais yafaa wawe waangalifu katika matamshi yao. Vinginevyo matamshi ya aina hiyo yanaweza kujenga msingi wa vurugu baadaye wao wenyewe.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakumbusha Vyama vya Siasa vijielekeze kwenye kutumia muda mwingi kuelezea, Sera za Vyama vyao ili ziweze kupimwa na Wapiga Kura badala ya kuchochea uhasama kati yao na Serikali na Tume ya Uchaguzi.

Kwa kumalizia,Tume haitasita kukifikisha Chama au Mgombea mbele ya Kamati ya Maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake na anaposhindwa Kamati itaweza kutoa adhabu kali kwa Chama au mgombea husika ikiwa ni pamoja na kukatazwa kampeni kwa muhusika.

Jaji (mst.) Damian Lubuva

MWENYEKIITI

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment