WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imejivunia mafanikio mbalimbali
yaliyopatikana katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne katika
kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Mafanikio hayo ni pamoja na kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito na
watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, kushuka kiwango cha
maambukizi ya malaria na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya
Ukimwi (VVU).
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa waganga wakuu wa wilaya
na mikoa Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Steven Kebwe alisema mafanikio hayo yameiwezesha wizara kuvuka lengo
namba nne la Maendeleo ya Milenia kabla ya kumalizika mwaka 2015.
“Katika eneo la huduma za afya ya uzazi na mtoto, tumefanikiwa
kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kutoka 578 kwa kila vizazi hai
100,000 mwaka 2005 hadi 432 mwaka 2012, vifo vya watoto vimepungua
kutoka 99 mwaka 1999 hadi 45 kwa kila vizazi hai 1000,” alisema.
Alisema maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008
hadi 5.3 mwaka 2012 na maambukizi kutoka kwa mjawazito kwenda kwa mtoto
yamepungua kutoka asilimia 26 mwaka 2010 hadi 15 mwaka 2012.
“Katika kuboresha zaidi, wizara iliongeza na kusogeza huduma za
upimaji wa VVU karibu na wananchi hatua iliyofanya idadi ya watu
waliopima kuongezeka kutoka milioni 4.9 mwaka 2013 hadi milioni 25.4
mwaka 2013,” alisema.
Alisema huduma za wagonjwa nyumbani zimepanuliwa na kufikia watu
338,547 na mashine ndogo 525 za kupima CD4 kwa ajili ya vituo vya afya
na zahanati.
Naibu Waziri alisema kiwango cha maambukizi ya malaria kimepungua
kutoka asilimia 18 mwaka 2008 hadi asilimia 9.2 mwaka 2012 ikiwa ni
asilimia 50.
“Hata hivyo suala la kukusanya fedha, utunzaji, matumizi na
uwajibikaji usioridhisha katika utekelezaji wa sera, kanuni na miongozo
ni changamoto zilizotukabili,” alisema.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal aliipongeza wizara hiyo kwa
jitihada zake za kupambana na magonjwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti
ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment