SOMO la Hisabati ni moja ya masomo muhimu, katika msingi wa
wanafunzi, tukianzia ngazi ya shule za msingi, sekondari na kwa elimu ya
juu.
Sote tunaelewa kuwa taifa bila hisabati hakuna maendeleo ya sayansi na
teknolojia, hivyo kuna kila sababu ya somo hili kupewa kipaumbele.
Wataalamu wa Hisabati wamekuwa wakieleza kuwa mtu anayepuuza Hisabati ni
mtu wa maajabu na hushindwa kumudu hata matumizi ya kawaida.
Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita) ni moja ya wadau ambao wamekuwa
wakifanya jitihada, katika kuhakikisha Hisabati inapewa kipaumbele na
kupata mafanikio makubwa katika nchi.
Mwenyekiti wa Chahita), Dk Silvester Rugeihyamu, anasema kuwa pamoja na
juhudi za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa hisabati bado ufaulu wa
somo hilo ni wa kusuasua.
“Ufaulu wa Somo la Hisabati bado ni wa kususasua sana, hivyo tunaiomba
Serikali itoe umuhimu kwa somo hili, kutokana na kwamba ndio nguzo ya
masomo yote, na bila hisabati hakuna maisha ya sayansi na teknolojia,”
anasema.
Chama hiki kilianzishwa mwaka 1996 kwa malengo mbalimbali na moja ya
majukumu yake ni kuandaa na kuchapisha machapisho mbalimbali ya
hisabati, ikiwa ni pamoja na vitabu vya ziada na kiada kwa shule za
msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.
Jukumu lingine ni kuandaa mashindano katika somo la hisabati ya kila
mwaka, pamoja na kuendesha na kuratibu semina za hisabati na mikutano,
kwa ngazi ya wilaya, mkoa, kanda na kitaifa.
Anasema semina kwa walimu wa hisabati zina lengo la kuwaweka pamoja
walimu wa somo hilo, ili kuweza kuelimishana katika mada zilizongumu
kwenye eneo la ufundishaji na ujifunzaji.
Anasema Chahita inatambua wazi kuwa, matatizo mengi ya hisabati
yanaanzia katika elimu ya msingi, hivyo kuna haja ya viongozi wa ngazi
husika, kuhamasishwa ili kusukuma walimu kuhudhuria kwenye semina ambazo
zimekuwa zikitolewa na chama hicho.
‘Ruhusa na ufadhili kwa walimu wa shule za msingi katika kuhudhuria
semina za mafunzo ni shida, na bila walimu wa shule za msingi,
kuimarishwa, tutakuwa tunafanya kazi bure,” anasema.
Anasema Chama cha Hisabati, kimekuwa kikishirikiana na serikali
katika mipango mbalimbali kwa lengo la kuinua hisabati, lakini yapo
mambo ambayo wamekuwa wakiyapinga, ikiwa ni moja ya jitihada za
kuboresha somo hilo.
Pia, anasema moja ya mambo ambayo wamekuwa wakipingana na serikali ni
mfumo wa kuchagua jibu sahihi katika mtihani wa darasa la saba kwa somo
la hisabati.
“Chahita kilikataa mfumo wa kuchagua jibu sahihi katika mtihani wa
darasa la saba kwa somo la hisabati, na tulipeleka malalamiko yetu
Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), ambapo walitujibu kuwa mfumo wa
Multiple Choice unafaa.
“Baada ya majibu haya ya Necta, sisi hatukukubaliana nao na Juni
mwaka huu, tulikata rufaa Wizara ya Elimu na kwa sasa tunasubiri majibu.
“Tunasubiri majibu, lakini hatuelewi Wizara ya Elimu ikiwa kama Necta,
tutakata rufaa wapi, kwani malengo yetu ni kuona hisabati inaboreshwa na
kiwango cha ufaulu kwa somo hili kinapanda,” anasema.
Anasema suala la kuweka hisabati katika mfumo wa kuchagua jibu sahihi
chama hakikuhusishwa, licha ya kuwa wao ndio wataalamu wa hisabati.
Akizungumza Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa
Kilimanjaro, Ally Mmbaga, anasema, mfumo wa kuchagua jibu sahihi si
mfumo mzuri, hasa kwa somo la hisabati, kutokana na kwamba ikitokea
mwanafunzi akaamua kucheza na herufi, anaweza kufaulu vizuri, ilihali
hajui chochote.
“Mfumo huu unaweza kusababisha mwanafunzi akafaulu vizuri sana na
ukaona ni mwanafunzi bora kumbe amecheza tu na herufi na hata hawezi
kuonesha njia ya kazi yake, tunapaswa kuondoa mfumo huu,” anasema
Mmbaga.
Anasema serikali inapaswa kubadilisha mfumo wa kuchagua majibu sahihi na
kuhakikisha wanafunzi, wanaonesha njia za maswali watakayofanya badala
ya kuweka herufi ya jibu sahihi pekee.
Pia, anasema kwenye mitihani ya darasa la kwanza hadi la sita hakuna
mfumo wa kuchagua herufi ya jibu sahihi katika mitihani, lakini jambo la
kushangaza katika mtihani wa taifa kumewekwa mfumo huo jambo ambalo si
sahihi.
“Kimsingi ni kwamba, Serikali inapaswa kubadili mfumo huu wa kuchagua
herufi ya jibu sahihi katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa
somo la hisabati, na kuwataka wanafunzi waoneshe njia, kwani hata
ikitokea mwanafunzi ameibia jibu kwa mwenzake, hataweza kupata maksi
zote kwenye hilo swali kwa sababu atakosea kuonesha njia aliyofanya
kupata jibu hilo.
“Ipo hatari kubwa ya kuchagua jibu sahihi hasa katika somo la hisabati
ambalo ni muhimu sana, kwani akipiga kengeza anaweza kupata jibu sahihi,
hivyo ni vyema serikali ikaondoa mfumo huu,” anaeleza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, anasema wizara inatambua
kwamba hisabati ni somo lenye changamoto nyingi katika ufundishaji na
ujifunzaji katika ngazi zote za elimu.
“Ufaulu wa Somo la Hisabati katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari
katika Taifa letu kwa kipindi kirefu umekuwa na changamoto nyingi,”
anasema.
Anasema wastani wa waliofaulu katika miaka saba iliyopita kwenye mtihani
wa hisabati kitaifa shule za msingi ni 28.1 huku katika shule za
sekondari ikiwa wastani wa 18.1.
Aidha, anasema hali hiyo haiwezi kuachwa iendelee, hivyo ni jukumu la
wadau wote wa elimu nchini, kuunganisha nguvu zao, ili kuweza
kubadilisha hali hiyo.
“Ujenzi wa Taifa lenye uchumi imara, na maendeleo ya sayansi na
teknolojia hauwezi kufikiwa kama ufaulu wa somo la hisabati, utakuwa
chini, kwani hisabati ni msingi wa maendeleo kwa maeneo mengi kama vile
uchukuzi, mawasiliano, ufundi, ujenzi, viwanda, fedha, madini, kilimo,
maji, takwimu, sayansi na teknolojia.
Anaongeza kuwa “Tukumbuke kuwa ufaulu katika hisabati, huathiri
upatikanaji wa wanaojiunga katika vyuo vikuu na vyuo vingine, vinavyotoa
elimu katika ngazi ya stashahada kwa masomo ya sayansi na hisabati,”
anasema.
Anasema ni vyema kila mdau akashiriki, kikamilifu kwa nafasi yake katika
harakati za kuinua ufaulu wa somo la hisabati katika ngazi zote za
elimu.
Anatumia pia nafasi hiyo, kuwataka walimu wa hisabati nchini, kuchunguza
kwa kina sababu ambazo zinafanya somo la hisabati kutopendwa na
wanafunzi wengi.
“Naomba mtafakari ni kwa namna gani ninyi kama wataalamu wa hisabati,
mtaboresha ufundishaji na ujifunzaji, hasa katika mazingira ya ndani ya
darasa, ili kuwezesha ufaulu wa somo hili kupanda,” anasema.
Anasema kuna haja ya kuangaliwa matumizi ya Tehama katika kurahisisha
ufundishaji wa hisabati shuleni hatua ambayo itasaidia kuleta mvuto wa
aina yake kwa wanafunzi kujifunza hisabati hata wakiwa peke yao.
Aidha, anaeleza kuwa ufundishaji bora wa somo la hisabati, unapaswa
kutumia vifaa vya kutosha katika mazingira halisi, ili matumizi ya
hisabati yaweze kuwa bayana zaidi kwa wanafunzi.
Anasema kuna haja sasa ya walimu wa hisabati kutumia mazingira halisi ya
shule, katika ufundishaji, na utoaji mifano ya matumizi ya hisabati,
kama vile vifaa vya kiteknolojia ya kisasa na vitu mbalimbali
vinavyotumia dhana ya hisabati katika matumizi au uundwaji wake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment