WAZIRI wa zamani wa Serikali ya Tanzania, Nalaila Kiula, amemshangaa
mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward
Lowassa kuwa atafuata utawala bora kuwaachia kutoka gerezani watu ambao
tayari wamehukumiwa na Mahakama endapo atachaguliwa kuwa rais.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kiula alisema Lowassa hakuwa na sababu
ya kutoa kauli hiyo inayojenga chuki miongoni mwa watu walioathiriwa na
vitendo vya watu waliopo gerezani.
Lowassa ambaye anawania urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), amesema endapo Watanzania watamchagua kuwa Rais katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu, atatumia taratibu za utawala bora kuhakikisha
anawatoa gerezani mwanamuzi maarufu nchini, Nguza Viking maarufu kwa
jina la Babu Seya, pamoja na wanawe waliofungwa kifungo cha muda mrefu
kwa makosa ya kunajisi watoto.
“Mimi nafahamu sheria kidogo na usisahau pia nimewahi kuwa waziri katika
Wizara ya Mambo ya Ndani. Utaratibu ulivyo ni kwamba Mahakama ikishatoa
hukumu, utaratibu unaofuata ni rufaa. Huo ndio utawala wa sheria. Rais
wa nchi anaweza kutoa msamaha kwa wafungwa kwa kufuata utaratibu
maalumu, tena kwa baadhi ya makosa, na hili la ubakaji halimo,” alisema
Kiula.
Kiula ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Rais
Ali Hassan Mwinyi, alisema ni vema wanasiasa wakazungumzia mambo ya
msingi yanayolikabili Taifa hivi sasa, badala ya mambo madogomadogo
ambayo taratibu zake za kuyatatua zinafahamika na hazina matatizo.
Akizungumza mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu unaoendelea hivi sasa,
Kiula alikosoa pia utaratibu wa wagombea kutoa hotuba kwa kusoma kwenye
makaratasi au kuwataka watu wasome kwenye tovuti badala ya kueleza
waliyonayo vichwani mwao ili kudhihirisha kuwa wanakijua
wanachokizungumzia kwa wananchi.
Mmoja wa wanasheria maarufu aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya
kutotajwa jina akisema ataingizwa kwenye siasa, alisema kauli za
Lowassa kwenye uzinduzi wa kampeni zinashtusha na kushangazana kueleza
kuwa waziri mkuu huyo wa zamani haelewi maana ya dhana ya utawala wa
sheria na inaonesha ana viashiria vya udikteta.
Msomi huyo alisema Lowassa ameonesha kuwa ni mtu anayefuata upepo na anayeweza kufanya maamuzi kwa shinikizo la watu.
“Hili la kutaka kumwachia Babu Seya na wale masheikh wa kundi la Uamsho
kutoka Zanzibar amelitoa baada ya kushinikizwa na watu waliokuwa
wanamsikiliza wakati wa uzinduzi wa kampeni, na pale alipokuwa
anawatembelea wananchi wa kawaida kwenye mitaa ya Jiji la Dar es
Salaam,” alifafanua.
Alisema kama Lowassa angekuwa mtu makini na anayewajali wanyonge, kama
anavyodai, basi angezungumzia kuunda tume itakayochunguza matatizo ya
watu mbalimbali waliopo magerezani badala ya kuwazungumzia wahalifu
wachache wenye umaarufu kwa lengo la kuwavutia wapiga kura.
Akizungumzia suala hilohilo, Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK),
Constantine Akitanda, alisema kwa kauli ya kutaka kuwaachia watuhumiwa
wa Uamsho wanaodaiwa kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani Zanzibar,
Lowassa amedhihirisha kuwa akiingia madarakani atasababisha mfarakano
mkubwa zaidi kwenye jamii.
Amesema hali ya amani imerejea Zanzibar na sasa wananchi wanafanya
shughuli zao za maendeleo bila hofu ya vitendo vya kigaidi kama
ilivyokuwa awali.
Mmoja wa Watanzania maarufu katika mtandao wa twitter, Maria Sarungi,
alibandika katika ukurasa wako huo maneno yafuatayo; “kama vyombo vya
habari vya Tanzania vingekuwa kama vya Marekani, kichwa cha habari
kutoka mkutano wa Jangwani vingesema; “mgombea urais atangaza kuwasamehe
wabakaji.”
Sitta
Siku chache baada ya mgombea urais wa Chadema na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa kusema ataboresha sekta ya mawasiliano
nchini, ikiwemo reli ya kati, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amejibu
mapigo dhidi ya mgombea huyo.
Lowassa alitoa kauli hiyo katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam
wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chama hicho na kusisitiza kuwa
akifanikiwa kuingia madarakani atafufua Shirika la Ndege Tanzania (ATC).
Kutokana na kauli hiyo, Waziri Sitta alikutana na waandishi wa habari
jana na kubainisha kuwa Lowassa anazungumza mambo ambayo hayajui na
kwamba ujenzi wa reli ya kati unaendelea na upo katika hatua nzuri.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa reli hiyo, Sita alisema ujenzi upo katika
hatua nzuri na Septemba 15, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete anatarajia
kuweka jiwe la msingi katika reli hiyo iliyojengwa na Kampuni ya Ujenzi
wa reli ya China (CRCC) na Kampuni ya Ujenzi na Uhandisi wa Majengo ya
China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).
Alisema reli hiyo inajengwa kwa mkataba wa sh. trilioni 16 ambazo ni
sawa na sh. bilion 7.6 mapato ambayo yanapatikana Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), kwa mwaka.
Sitta alisema wanatarajia kutumia reli hiyo kwani tayari wametiliana
saini pamoja na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda huku akibainisha kuwa
endapo itakuwa imekamilika na nchi hizo zikaanza kupitisha mizigo ndani
ya miaka minne hali ya uchumi itabadilika.
Akizungumzia suala la Air Tanzania alisema Serikali inaendelea
kukamilisha taratibu za kuchukua madeni na kwamba wameingia mkataba na
Benki ya TIB ili iweze kuwakopesha fedha za kununua ndege nne ambazo
zitasaidia kurudisha Air Tanzania.
“Tuna imani kubwa kabla ya Oktoba mwaka huu tutakuwa tumenunua ndege
hizo nne, sasa tuna ndege moja ambayo haiwezi ikafanya kazi zote,”
alisema.
Kuhusu suala la ATC, Lowassa alisema atahakikisha anafufua shirika
hilo kwani ni aibu kuzidiwa na nchi ndogo kama Kenya na Rwanda huku
akiweka bayana kuwa hakuna sababu ya kushindwa.
Mbatia
Kwa upande wao, Ukawa, umesema taarifa zinazosambazwa katika mitandao na
baadhi ya vyombo vya habari kuhusu mgombea wao wa urais kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kuwa alisema
atawaachia masheikh na Nguza Vicking (Babu Seya) akifanikiwa kuwa rais
si za kweli.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mbatia alisema watu wanapotosha alichosema Lowassa kwa makusudi katika
kutimiza malengo yao ya kisiasa huku wakitumia nguzo ya dini kama njia
ya kutetea maovu yao.
Mwenyekiti Mwenza huyo alisema Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya
viongozi wa Ukawa kukaa na kujadili malalamiko mengi ambayo wananchi
walionesha kuhitaji ufumbuzi mojawapo ikiwa ni kufungwa kwa Babu Seya na
masheikh.
Alisema walijadiliana na kuona kuwa suala hilo linahitaji kupewa nafasi
iwapo watapata nafasi ya kushinda katika uchaguzi kwa kufuata misingi ya
utawala bora, sheria na kanuni za nchi na si vinginevyo.
“Inasikitisha sana kuona viongozi wetu wa vyama wanaamua kupotosha umma
kuhusu kauli ya Lowassa kushughulikia tatizo la wafungwa ambao
wanaonekana kufungwa kwao kuna maswali mengi, ila jambo la kushangaza ni
udini nao unahusishwa ni aibu na hii haikubaliki,” alisema.
Alisema suala hilo lisipewe nafasi katika jamii kwani athari yake
inaweza kuwa mbaya tofauti na watu wanavyofikiria ambapo mawazo yao
yanaelekezwa Ikulu na si haki za binadamu.
Mbatia alisema iwapo kutakuwepo na mazingira ya ukiukwaji wa haki za
binadamu ni wajibu kuangalia njia ya kutatua matatizo yaliyopo kwa
utaratibu sahihi ambazo zitamtendea haki kila mtu.
Alisema ni jambo la aibu kufananisha ugaidi na imani za dini kwani ni
wazi kuwa wanaofanya ugaidi si kwamba wanasimamia misingi ya dini zao
ila mahitaji yao binafsi.
“Nadhani tunafanya mzaha na hizi kauli lakini vyanzo vya mifarakano
katika nchi ni kauli za viongozi ambao hutumia majukwaa vibaya kupotosha
umma wakiamini kuwa hiyo ndiyo njia ya wao kufanikiwa kisiasa,”
alisema.
Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi, alisema katika kuonesha kuwa
upotoshaji huo umepangwa ndiyo maana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
inashindwa kuchukua hatua jambo ambalo linasababisha vyama kutokuwa na
imani nayo.
Pia, aliweka bayana kuwa Jeshi la Polisi linashiriki kuwepo na
muendelezo wa kauli hizo za kupotosha na kulitaka lichukue hatua stahiki
kwa faida ya nchi na wananachi.
Dk. Kahangwa
Akizungumzia upotoshaji huo, Mratibu wa Kamepeni za Ukawa Taifa, Dk
George Kahangwa alisema kimsingi kinachoonekana kwa sasa ni siasa za
Tanzania kuonekana kutokidhi mahitaji sahihi.
Dk. Kahangwa alisema vyama vinashindwa kutoa sera kwa wananchi na
kinyume chake vinatumia muda mrefu kutukanana jambo ambalo linaenda
kinyume cha hitaji la wananchi.
“Kinachoondelea ni kuonesha kuwa siasa za Tanzania bado hazijakidhi
mahitaji ya wananchi na hao ambao wanatumiwa pia wana dalili za
kutojitambua ndiyo maana mtu anadiriki kutukana akiona ndiyo anafanya
kampeni, kampeni sahihi inahitaji sera na mipango yautekelezaji si
matusi,” alisema.
Home
News
Nalaila Kiula aibuka*Ashangaa msamaha wa Lowassa kwa Babu Seya *Mbatia atoa ufafanuzi, asema suala hilo linapotoshwa Mwandishi Wetu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment