JANA Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa amesema
Sheria ya Makosa ya Mtandao na Miamala ya Kieletroniki inaanza kutumika
rasmi leo nchini kote.
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa Watanzania wanatakiwa kuwa makini na
matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepukana na adhabu kali za sheria
hiyo.
Prof. Mbarawa alisema Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015
imeanisha makosa na adhabu za uhalifu wa mitandao na kwamba itasaidia
kuzuia wizi wa fedha mitandaoni, picha chafu na ujumbe wenye matusi.
Waziri huyo amekaririwa pia akisema Serikali baada ya kujiridhisha
kuwa maandalizi yote muhimu ikiwemo elimu kwa umma na kujenga uelewa
yamefanyika, ni wakati muafaka kwa sheria hiyo kuanza kutekelezwa.
Ujio wa sheria hiyo kwa kiwango fulani unalenga kuhakikisha mitandao
ya kijamii na vyombo vingine vya utoaji habari kwa umma vinafanya kazi
kwa umakini na kuzingatia miiko inayotakiwa. Ni jambo jema kwa sababu
baadhi ya mitandao inatumika vibaya tofauti na malengo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo, hatuoni kama kweli wananchi wameelimishwa vya kutosha
kuhusu sheria hiyo kama Prof Mbarawa anavyosema kwa sababu haikutungwa
muda mrefu. Kwa msingi huo kuna kila sababu ya kuendelea kuelimisha umma
kuhusu sheria husika.
Kama sheria hiyo imetungwa kwa lengo kuzua utumiaji mbaya wa mitandao
sawa, lakini adhabu zilizopo na faini zinakatisha tamaa hususan katika
ujenzi wa demokrasia hasa kwa nchi changa kama zetu ambazo mifumo ya
uwajibikaji si mizuri kwa kiwango cha kutia matumaini.
Kwa msingi huo kama wadau wataona sheria hiyo ni kitanzi katika uhuru
wa watu kutoa maoni, ni muhimu kwa wabunge kuipitia upya kwa lengo la
kutoa usawa kwa watumiaji wake ili kuendelea kurutubisha uhuru wa watu
kujieleza au kutoa hisia zao.
Vinginevyo tunaamini kwa upande mwingine sheria hiyo itaziba nyufa
ambazo zilianza kuonekana hususan katika suala zima la mmomonyoko wa
maadili. Chini ya sheria hiyo tunaamini utu na thamani ya kila mwananchi
itaheshimiwa badala ya kudhalilishwa kwa njia za mitandao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment