Rais wa Marekani Barack Obama amekutana na mwenzake wa Urusi Vladimir
Putin pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kuujadili mzozo wa
Syria.
Katika hotuba zao tofauti katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo
jana, Rais Obama amemtaja Rais wa Syria Bashar al Assad kama kiongozi wa
kiimla anayewaua watoto huku Putin akisema ulimwengu unapaswa kumuunga
mkono Assad katika kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la
kiislamu IS na kuonya ana mipango ya kuimarisha misaada ya kijeshi kwa
utawala wa Assad.
Baada ya hotuba zao katika mkutano huo mkuu wa Umoja wa Mataifa, Obama
na Putin walikutana kwa mkutano wa ana kwa ana uliodumu dakika tisini
ambapo pia walikubaliana kuwa majeshi yao yanapaswa kufanya mazungumzo
ili kuzuia mkwaruzano kati yao kwani majeshi yote yanafanya kampeini za
kijeshi nchini Syria.
Putin aahidi kuendelea kumuunga mkono Assad
Marekani, Ufaransa na nchi washirika zinafanya mashambulizi ya angani
dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS
ambao wamechukua fursa ya kuwepo msukosuko nchini humo na kuyadhibiti
maeneo makubwa Syria na Iraq.
Baada ya mkutano huo, Rais Putin amewaambia wanahabari kuwa nchi yake
inafikiria ni njia zipi zaidi zinaweza kuisadia serikali ya Syria na
wapiganaji wa kikurdi kupambana dhidi ya IS na kuongeza kuna fursa ya
kufanya kazi kwa pamoja na Marekani kushughulikia tatizo hilo la IS.
Kiongozi huyo wa Urusi hata hivyo amesema sio wajibu wa Marekani au
Ufaransa kuamua ni nani anastahili kuwa kiongozi wa Syria kwani hilo
linaweza tu kuamuliwa na wasyria
Obama kushirikiana na Urusi kupambana dhidi ya IS
Rais Obama kwa upande wake amesema yuko tayari kushirikiana na Urusi na
hata Iran kuvimaliza vita vya Syria ambavyo vimedumu zaidi ya miaka
minne ambapo zaidi ya watu laki mbili wameuawa na mamilioni ya wengine
wameachwa bila ya makaazi lakini hakubaliana na pendekezo la kusalia
madarakani Rais Assad kwani yeye ndiye mhalifu mkubwa zaidi wa mzozo wa
Syria.
Obama hakutaja moja kwa moja kuondolewa madarakani Assad na badala
yake amedokeza kuwa kunaweza kuwa na kile alichokitaja kipindi cha mpito
hiyo ikiwa dalili ya hivi karibuni kuwa Marekani inazingatia kumuacha
Assad kusalia madarakani kwa muda, mtizamo ambao unazingatiwa na nchi za
Umoja wa Ulaya.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet
Davutoglu wamepinga uwezekano wa Assad kuruhusiwa kusalia madarakani.
Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Khalid al Attiya ameionya Urusi kuwa
imeshindwa kushughulikia chanzo cha mzozo wa Syria ambacho anasema "ni
utawala wa Assad." Putin na Obama pia waliuzungumzia mzozo wa Ukraine
katika mkutano wao, suala ambalo limesababisha hali ya vita baridi kati
yao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
0 comments:
Post a Comment