Tanzania
ni nchi ya kwanza duniani kutoa huduma za pesa, kutoa mikopo na kutoa riba kwa
kutumia mawasiliano ya simu, Benki ya Dunia imesema na kuongeza kuwa Tanzania
ni moja ya masoko makubwa zaidi duniani ya kutoa huduma ya fedha kwa njia ya
simu.
Benki
hiyo ya Dunia pia imesema kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza kwa kiwango cha
juu katika mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ikilinganishwa na
nchi nyingine duniani na kulingana na uwezo wake.
Benki
hiyo pia imesema kuwa nchi jirani ya Kenya inaongoza kwa kutuma pesa kupitia
mfumo wa M-Pesa katika eneo ambalo miaka michache iliyopita lilikuwa eneo la
kujidai la nchi tajiri tu duniani.
“Huuni
mfano kutoka Afrika ambao unaweza kuigwa na nchi zote duniani,”
amesema Profesa Kaushik Basu, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB) wakati
akiwasilisha kwa ufupi tu yaliyomo katika Ripoti ya Benki hiyo ya
World Development Report ambayo itatolewa hivi karibuni.
Profesa
Basu alikuwa anazungumza jana, Jumatatu, Septemba 28, 2015 kwenye Mkutano wa
Wakuu wa Nchi uliozungumzia Hali ya Enzi za Digitali (Digital Age) uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
(UN), ikiwa ni sehemu ya majadiliano kuhusu Malengo ya Maendeleo Mapya (SDG’s) ambayo yanachukua nafasi ya
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s)
ambayo muda wake wa utekekezaji wa miaka 15 umefikia mwisho mwaka huu.
Akizungumza
katika mkutano huo uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Estonia Mheshimiwa Toomas Hendrik
Ilves na Rais wa Benki ya Dunia (WB) Dkt. Jim Kim, Profesa Kaushik alisema:
“Tuko
katikati ya mapinduzi makubwa ya teknolojia, ambayo athari zake bado ni ngumu
sana hata kubashiri. Na hizi ni shughuli ambazo miaka michache iliyopita
zilikuwa hata hazina jina, lakini sasa inteneti na teknolojia ya digitali
inabadilisha maisha ya kijamii na kisiasa ya binadamu,” alisema
Profesa Basu.
Aliongeza:
“Chukulia
takwimu hizi – kuna kiasi cha utafuta habari kwenye google kiasi cha bilioni
4.2 kwa siku moja, kila sekunde watu wanatuma tweet 6,000 na rekodi ilikuwa
Agosti mwaka 2013 wakati zilipotumwa tweet 143,199 kwa sekunde wakati ilikuwa
inaonyeshwa filamu moja ya sanaa.”
Aliongeza:
“Mfumo
wa uwekaji na utumaji pesa wa M-Pesa katika Kenya sasa unashindana na mifumo ya
siku nyingi ya nchi matajiri duniani. Kila watu wazima 1,000 kuna akaunti 700
katika Kenya ikiwa ni ongezeko 103 kutoka mwaka 2013.”
“Jirani
na Kenya kuna mfano mwingine wa mafanikio makubwa zaidi duniani katika nchi
jirani ya Tanzania. Tanzania imewekeza sanakatika ICT na katika mfumo wa
kuhamisha na kusambaza fedha. Sasa Tanzania ni soko kubwa zaidi duniani la
kutuma fedha kwa njia ya simu,” alisema Profesa
Kaushik.
Aliongeza:
“Tanzania
sasa ni nchi ya kwanza duniani kutoa huduma ya pesa, kutoa mikopo na kutoa riba
kwa njia ya simu. Hii ni mifano ambayo nchi zote duniani zinaweza kuiga kutoka
Afrika.”
Wakati
huo huo, Rais Kikwete leo, Jumanne, Septemba 28, 2015, amekutana na kufanya
mazungumzo na Malkia wa Uholanzi, Malkia Maxima wa Uholanzi, Mke wa Mfalme
Willem-Alexander kuhusu jinsi gani ya kuzidi kuisaidia Tanzania kuongeza kasi
yake katika kuboresha huduma za pesa kupitia ICT.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29
Septemba, 2015
0 comments:
Post a Comment