Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea
changamoto kubwa zinazozuia kukua haraka zaidi kwa sekta ya utalii katika
Afrika na hivyo kuliwezesha Bara hilo kuchuma matunda makubwa zaidi kutokana na
sekta hiyo.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na kuwa na vivutio vingi vya utalii, Bara la
Afrika, bado linabakia nyuma kwa kiasi kikubwa katika kuvutia watalii wa kimataifa
na katika mapato yanayotokana na utalii.
Rais
Kikwete vile vile amesema kuwa Tanzania itaendelea kutenga eneo kubwa la ardhi
yake kwa ajili ya hifadhi na pia itaendelea kukabiliana na ujangili dhidi ya
tembo, ambao hata hivyo amesema kuwa umepungua katika mwaka uliopita.
Rais
Kikwete ameyasema hayo, Alhamisi, Septemba 24 wakati alipotoa hotuba ya
ufunguzi wa shughuli za Miaka 10 ya Chama cha Usafiri cha Afrika – Africa
Travel Association (ATA) na Miaka 10 ya Jukwaa la Rais Kuhusu Utalii – Presidential
Forum on Tourism kwenye Kituo cha Kimmel cha Chuo Kikuu cha New York (New
York University Kimmel Center) Africa House, mjini New York.
Rais
Kikwete yuko New York, Marekani kwa ajili ya kuhudhuria shughuli za mwaka huu
za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA)
baada ya kumaliza kuendesha vikao vya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani ambao
wanatafuta jinsi gani dunia inavyoweza kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana na
magonjwa ya mlipuko ambavyo pia vilifanyika New York.
Rais
Kikwete ametambulishwa na kukaribishwa kutoa hotuba yake na Dkt. Yaw Nyarko,
Raia wa Ghana na Mkurugenzi wa Africa House ambaye pia ni Profesa wa Uchumi
kwenye Chuo Kikuu cha New York na Bwana Edward Bergman, Mkurugenzi Mtendaji Mwanzilishi
wa ATA.
Alikuwa
ni Rais Kikwete na familia ya Bergman ya New York ambao walianzisha na kujadili
wazo la kuanzishwa kwa chama hicho miaka
10 iliyopita.
Kabla
ya kutoa hotuba yake, washiriki wa Kumbukumbu hiyo ya miaka 10 wamesikia
maelezo ya kina kutoka kwa mawaziri wa nchi tano za Afrika kuhusu hali ya utalii
katika nchi hizo na katika Bara la Afrika kwa jumla.
Mawaziri
waliozungumza kwenye shughuli hiyo iliyoendeshwa na Bwana Peter Greenberg,
Mhariri wa Usafiri wa Televisheni ya CBS ni
Mheshimiwa Lazaro Nyalandu wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Maria Mutagamba, Waziri
wa Utalii, Wanyamapori na Nyaraka wa Uganda ambaye pia ni Rais wa ATA na Mheshimiwa N’Diaye Ramatoulaye
Diallo, Waziri wa Utamaduni, Utalii na Usanii wa Vinyango wa Mali.
Mawaziri
wengine ambazo wamezungumza katika shughuli hiyo ni Mheshimiwa Phylis Kandie
ambaye ni Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii wa Kenya na
Mheshimiwa Pohamba Shifeta, Waziri wa Mazingira na Utalii wa Jamhuri ya
Namibia.
Akizungumza
katika shughuli hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa “changamoto kuu zinazokabili
maendeleo ya utalii katika Afrika ni miundombinu ya kitalii, utangazaji wa
masoko ya utalii na matatizo ya usafiri wa anga kuingia na kutoka Afrika.”
“Lakini
pia kuna jambo kubwa la mtazamo hasi kuhusu Afrika. Kwa kawaida, vyombo vya
habari vya nje vinalielezea Bara la Afrika kama Bara hatari ambalo sifa zake kuu
ni migogoro, magonjwa na matatizo yanayotokana na umasikini. Haya yote siyo ya
kweli ni upotoshaji wa makusudi.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Ukweli kuhusu Afrika lazima uelezwe kwa usahihi na sisi wenyewe. Picha
inayojengwa kuwa tatizo katika nchi moja ni tatizo la Bara zima siyo ya kweli
na lazima itafutwe namna ya kulisahihisha jambo hilo. Afrika ni Bara la nchi 54
na siyo nchi moja ya majimbo 54.”
Ameongeza:
“Ni
upotoshaji huu ambao ulisababisha watu kufuta safari za kitalii kwenda Afrika
wakati ugonjwa wa Ebola ulipolipuka katika Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Lakini Zanzibar katika Tanzania ni safari ya saa tisa za ndege kutoka nchi hizo
tatu za Afrika Magharibi. Kwa hakika nchi hizo tatu ziko karibu zaidi na Bara
la Ulaya kuliko ilivyo Kenya. Hili ni tatizo kubwa ambalo lazima lisahihishwe
haraka iwezekanavyo.”
Kuhusu
mapato ya utalii, Rais Kikwete amesema: “Mwaka jana, Afrika ilipokea watalii wa
kimataifa milioni 56 ambalo ni ongezeko la asilimia mbili tu ya watalii wote wa
kimataifa waliotembelea maeneo mbali mbali ya dunia na asilimia tano ya watalii
wote waliotembelea dunia mwaka jana.”
Kuhusu
Tanzania, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inaendelea kutenga asilimia 36 ya
eneo lake lote kwa ajili ya shughuli za hifadhi.
“Tumefanya
hivyo tokea uhuru wetu. Tutaendelea kufanya hivyo. Kama mnavyojua pia tumekuwa
tunakabiliana na changamoto ya ujangili ambao ulitishia kumaliza idadi ya tembo
wetu. Tumechukua hatua na kuendesha kampeni dhidi ya janga hili. Sasa tunaanza
kuona matunda ya juhudi zetu. Mwaka 2012 walikuwa wanauawa tembo sita kwa
mwezi. Katika mwaka mmoja uliopita, hajauawa tembo yoyote.”
Rais
Kikwete pia ameshangiliwa sana wakati alipowaambia washiriki wa shughuli ya
leo: “Napenda
kuchukua nafasi hii, vile vile, kuwaageni marafiki zangu wote wa ATA kwa sababu
hotuba hii ni ya mwisho kwangu nikiwa Rais wa nchi yangu. Nitaondoka madarakani
baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015 baada ya kuwa
nimekamilisha vipindi viwili vya uongozi wangu kwa mujibu wa Katiba ya
Tanzania.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25
Septemba, 2015
0 comments:
Post a Comment