Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, ameyasema hayo jana
katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM zilizofanyika
Kijiji cha Michamvi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema tayari kuna baadhi ya wanasiasa, wameanza kujiandaa kutumia
makundi ya vijana ili kuleta fujo wakati wa uchaguzi mkuu kama mkakakti
wao wa kufikia malengo yao kisiasa.
“Natahadharisha asijaribu mtu au kikundi chochote kufanya vurugu,
safari hii tumejitayarisha kisawasawa…hatutakubali zitokee ghasia kama
zile za Uamsho, atakayejaribu kuvuruga utulivu na amani atakiona cha
mtema kuni,” alisema Balozi Seif.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona kampeni chafu zimeanza, ikiwamo
kuchanwa picha za mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein katika
visiwa vya Pemba na Unguja.
“Mabango ya picha za Dk. Shein yanabanduliwa, ukimuona mtu anachana
kitu kisichosema ni sawa na kugombana na mwehu, hiyo ni dalili tosha
kuwa wapinzani wa CCM wameshindwa kabla ya Oktoba 25,” alisema Balozi
Seif.
Alisema SMZ imenunua meli ya kisasa, kupeleka nishati ya umeme wa
gridi ya taifa Pemba kutoka Tanga hadi Pemba, ujenzi wa miundombinu ya
barabara za viwango vya lami, uwanja wa ndege wa kisasa wa Abeid Amani
Karume mbali na kupandisha bei ya zao la karafuu toka Sh 5,000 hadi Sh
14,000 kwa kilo.
Katika mkutano huo, Balozi Seif aliwanadi na kuwaombea kura wagombea
wa nafasi za ubunge na uwakilishi wa majimbo yote ya Mkoa wa Kusini
Unguja wanaowania kupitia CCM.
Naye mwanasiasa mkongwe, Sukwa Said Sukwa, akizungumza katika mkutano
huo, alisema viongozi wastaafu wanaopanda kwenye majukwaa ya kampeni za
CCM na kushindwa kuwaombea kura Dk. Shein na Dk. John Magufuli
wanastahili kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Sukwa alisema haiwezekani kiongozi mstaafu ambaye alifanyiwa kampeni
na viongozi wenzake, leo ashindwe kumfanyia kampeni mgombea wa CCM.
0 comments:
Post a Comment