Image
Image

Stars yaonesha mwanga.

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema licha ya timu yake kupata matokeo ambayo sio mazuri sana dhidi ya Nigeria Super Eagles, kikosi chake kimeonesha mwanga katika mechi hizo za kufuzu kwa fainali za Afcon 2017.
Taifa Stars juzi iliikaribisha Super Eagles na kutoka nayo suluhu katika mchezo wa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Fainali hizo za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 zitafanyika nchini Gabon.
Mkwasa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kama alivyowaelekeza na kufanikiwa kuibana Nigeria katika mchezo huo.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa matokeo haya, kwa kweli nimeridhika na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wa timu yangu kwani wamecheza kama nilivyowaelekeza,” alisema Mkwasa. Alisema walichopungukiwa wachezaji wake ni uzoefu wa kimataifa ukilinganisha na Nigeria, ambao asilimia kubwa ya wachezaji wake wanacheza soka Ulaya.
Mkwasa aliipongeza Nigeria kwa kucheza vizuri kwani uzoefu wao kwa kiasi kikubwa ndio walichangia Taifa Stars kucheza kwa kiwango kile walichocheza hadi kusababisha kuondoka na pointi moja.
Alisema Taifa Stars ilicheza mchezo wa kujituma zaidi na kila mchezaji alitekeleza jukumu lake kama alivyokabidhiwa. Alisema kikosi chake kilicheza kwa tahadhari na kwa kujituma sana ili kutopoteza mchezo huo wa nyumbani mbele ya mashabiki wao waliofika kuishuhudia timu yao iliyocheza na timu yenye uwezo mkubwa.
Mkwasa alisema watajipanga vizuri zaidi ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi zao zijazo dhidi ya Chad, Misri (marudio) na Nigeria (marudio) na kuhakikisha wanafuzu kucheza fainali hizo za Afrika.
Kwa upande wake kocha wa Super Eagles, Sunday Oliseh alisema kuwa, timu yake ilionekana kucheza vizuri katika vipindi vyote ukiondoa makosa madogo madogo waliyoku wa wakiyafanya wachezaji wake.
Alisema timu yake bado mpya na wanaijenga na ni matumaini yake kuwa, wataendelea kufanya vizuri siku zinavyozidi kwenda.
Aliitetea timu yake kuwa ilikuja siku mbili kabla ya mchezo na hilo liliwafanya kuwa wachovu licha ya wakati fulani kuonekana wakishambulia kwa nguvu na wakati mwingine wakipunguza kasi yao, ambapo alisema matokeo hayo ni sehemu ya mchezo.
Alisema wanatarajia kufanya vizuri zaidi katika michezo ijayo kwani watakuwa na muda zaidi wa kufanya marekebisho ili kuhakikisha wana fuzu kwa fainali hizo. Stars katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Misri ilichapwa 3-0 huku Nigeria wenyewe waliifunga Chad 2-0 katika mchezo wao wa awali.
Taifa Stars mchezo wake ujao watacheza ugenini dhidi ya Chad Machi 25, 2016 kabla ya kurudiana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Machi 28, huku Nigeria watakuwa na kibarua kigumu watakapocheza na mabingwa wa kihistoria wa Afrika Misri wakiwa nyumbani Machi 23 mwakani.
Kimsimamo, Stars iliyokuwa inashika mkia imepanda na kuipiku Chad iliyokuwa katika nafasi ya tatu.
Msimamo Kundi G kabla ya mechi ya jana:
             P  W  D  L  GF GA GD Pts
Nigeria    2  1   1   0  2   0   2    4
Misri       1  1   0   0  3   0   3    3
Tanzania 2  0   1   1  0   3  -3    1
Chad      1  0   0   1  0   2  -2    0
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment