Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema pamoja na vitisho
ambavyo amevipata kutoka kwa mahasimu wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
hatarudi nyuma mpaka atakapohakikisha chama hicho kimeng’oka
madarakani.
Kadhalika, amesema mwisho wa CCM kukaa madarakani ni mwaka huu kwa kuwa wananchi wameamua kufanya mabadiliko wenyewe.
Aliyasema hayo jana wakati akizindua kampeni za ubunge Jimbo la
Ubungo za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema ukiwa ndani ya CCM, ni vigumu kufanya mabadiliko kutokana
na mfumo uliopo, lakini hata mtu akiamua kwenda chama kingine kutokana
na ukiritimba wa CCM, anakuchukiwa.
Alisema kwa ambavyo ametembea katika mikoa mbalimbali kwa kampeni
za kitaifa za mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(Chadema) anayeungwa mkono vyama shirika vya Ukawa, Edward
Lowassa, CCM mwaka huu ni lazima iondoke madarakani.
Alitaja mambo manne ambayo yatachangia CCM kuondoka madarakani kuwa
ni pamoja na ukosefu wa Katiba ya Wananchi ya kudhibiti utawala mbovu
ambayo alisema Ukawa wakichukua dola, litakuwa jambo la kwanza kuanza
nalo na itawapa wananchi mamlaka ya kuwa watawala wa viongozi.
Nyingine ambayo alisema imewafikisha Watanzania katika hali hiyo ya
umaskini kuwa ni kukosekana kwa umoja, uzalendo, uadilifu wa utawala
ambao umesababisha kutowajibika kwa viongozi na hata kuacha mianya ya
rushwa.
Sumaye alisema yeye hajaenda upinzani kwa ajili ya uroho wa madaraka kama wengine wanavyodai, kwa kuwa hagombei nafasi yoyote.
Kwa upande wake, mgombea wa ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Ukawa,
Saed Kubenea, alisema endapo wananchi wa Ubungo watamchagua, hawatajuta
kamwe kwa kuwa amejipanga vya kutosha kuwasaidia.
Kubenea alisema akiingia madarakani, atashughulikia tatizo la
usafiri katika jimbo hilo, tatizo la maji, afya na matatizo mengine.
0 comments:
Post a Comment