SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuanza kukata umeme
leo kwa mikoa inayotumia gridi ya taifa kwa wiki moja kwa saa 12 kila
siku.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alitaja baadhi ya
mikoa ambayo itakumbwa na tatizo hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Mbeya,
Lindi, Mwara, Mwanza, Arusha na mingine.
Alikuwa akizungumza na wandishi wa habari jana kwenye ziara ya kutembelea mitambo ya Kinyerezi na Ubungo, Dar es Salaam.
“Umeme utazimwa kila siku kwa wiki moja kwa saa 12, kuwezesha
mitambo ya Symbion na Ubungo 2 ipate kuunganishwa kwenye gridi ya taifa
kwa kutumia nishati ya gesi,” alisema.
Mramba alisema wakati mitambo hiyo inayotumia gesi itakapozimwa,
mtambo pekee utakaobaki ukifanyakazi ni Ubungo 1 ambao unaendesha mikoa
michache ambayo haiko kwenye gridi ya Taifa.
Alisema kazi ya kuunganisha mitambo hiyo inatarajiwa kukamilika
katika wiki moja na itawezesha kukamilika mradi huo uliozinduliwa miaka
miwili iliyopita na Rais Jakaya Kikwete.
Mramba alisema kama mradi huo utafanikiwa, mitambo ya Symbion pekee
itazalisha umeme wa Megawatt 102, mtambo wa Ubungo 2 utazalisha
Megawatt 105.
Akielezea faida zitakazopatikana baada ya kukamilika mtambo huo
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk. James
Mataragio alisema ni pamoja na Watanzania kupata umeme wa uhakika.
Faida nyingine ni kuondokana na utegemezi wa kuzalisha umeme kwa
kutumia mafuta yaliyokuwa yakiipa Tanesco hasara ya Sh bilioni moja kwa
mwaka.
Dk. Mataragio alisema hatua hiyo pia itasaidia kutunza mazingira kwa
kutumia gesi ikilinganishwa na aina nyingine ya nishati inazotumiwa
likiwamo na ongezeko la shughuli za uchumi kwa watu wa kawaida kutokana
na ajira mpya.
Mkurugenzi huyo alitaja faida nyingine kuwa ni kuanza uzalishaji wa
umeme kwenye mashine zilizopo Ubungo zenye uwezo wa Megawatt 200 ambazo
zilikuwa hazipati gesi ya kutosha.
Dk. Mataragio alisema uzalishaji huo utasaidia kuongezeka shughuli za utafiti na uendeshaji wa mafuta na gesi nchini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment