Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa, imekamata pombe
mbalimbali bandia za ‘viroba’ aina ya rider, empire, na signature vodka,
zilizokuwa zikidaiwa kutengenezwa bila kibali na kiwanda cha Mwanza
Lakeline Ltd, zikiwa zimehifadhiwa ghala la kampuni ya Ikohi lililopo
jijini Mwanza.
Bidhaa hizo ziligunduliwa katika ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa
na mamlaka hiyo zikidaiwa kuhifadhiwa katika ghala hilo linalomilikiwa
na kampuni ya Ikohi, lakini zikidaiwa zilitoroshwa katika kiwanda cha
Mwanza Lake Line, wakati kikifanyiwa ukaguzi na mamlaka hiyo.
Mkaguzi wa TFDA Kanda ya Ziwa, Nuru
Mwasulama, alisema kiwanda hicho kilichopo jijini Mwanza, hakijasajiliwa
kuzalisha bidhaa hizo zilizokamatwa, hivyo kilikuwa kikizalisha kwa
njia ya ujanja wakati ‘viroba’ vya kuwekea pombe hiyo vikinunuliwa
nchini Uganda.
“Tumechukua hatua ya haraka kukifungia kiwanda hicho na kuzuia
bidhaa zake kutokana na kucheza mchezo mchafu na kuhatarisha afya za
watumiaji wa bidhaa hizo,” alisema Mwasulama.
Alisema baada ya kufanya msako wa kushtukiza kiwandani hapo, siku
ya kwanza hawakufanikiwa kuingia ndani, lakini waliona ‘mzigo’ ukiwa
ndani ya kiwanda kupitia dirishani, isipokuwa kilichofanyika ni mmiliki
wa ghala la Ikohi kuuhamisha usiku na kuuweka ghalani mwake ili
usambazwe kwa walaji bila ya ruhusa ya mamlaka.
Mwasulama alisema kiwanda hicho kilipewa kibali na mamlaka
kusindika pombe ya ‘viroba’ aina ya simba gine pekee, lakini walikiuka
masharti ya leseni na kuzalisha bidhaa ambazo hawakupewa kibali
kuzalisha.
Alisema bidhaa zilizokamatwa ni masanduku 1,246 na magunia 25, ambayo thamani yake inakadiriwa kuwa Sh. milioni 75.
Hata hivyo, mmiliki wa ghala hilo, Ikohi alikataa kuzungumza na
waandishi wa habari kwa madai msemaji ni mmiliki wa kiwanda cha Mwanza
Lakeline, Chola Maginga, ambaye yupo safarini China.
0 comments:
Post a Comment