MSHAMBULIAJI nyota wa Tanzania, Mbwana Samata juzi alifunga mabao
matatu kuiwezesha TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
TP Mazembe yenye makazi yake Lubumbashi, imesonga mbele pamoja na Al
Hilal ya Sudan baada ya michezo iliyokuwa na ushindani katika Kundi A
lililomaliza mechi zao juzi. Klabu tatu katika kundi hilo, Mazembe,
Hilan na Moghreb Tetouan ya Morocco zilianza mechi hiyo ya mwisho ya
makundi zikiwa zimefungana kwa kuwa na pointi nane.
Mabao matatu ya Samata yaliisaidia TP Mazembe kusonga mbele kwa
ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Moghreb Tetouan, na Al Hilal
ilisonga mbele baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Smouha ya Misri. Mabingwa
mara nne, Mazembe sasa watacheza na mshindi wa pili wa Kundi B, El
Merreikh ya Sudan katika nusu fainali.
Mshindi wa Kundi B, USM Alger ya Algeria itacheza na mshindi wa pili
mara mbili, Al Hilal. Ikitumia uwanja wake wa nyumbani mjini Lubumbashi,
TP Mazembe ilianza haraka kujichuja katika mechi hiyo ya mwisho dhidi
ya Moghreb Tetouan kwa Samata kufunga bao la kwanza katika dakika ya 12.
Rainford Kalaba aliongeza bao jingine katika dakika ya 30, huku
Samata akifunga la kwake la pili dakika ya 53. Mchezaji kutoka Ivory
Coast, Roger Assale alifanya matokeo yawe 4-0 kwa TP Mazembe zikiwa
zimebaki dakika mbili pambano kumalizika, kabla ya Samata kufunga bao
lake la tatu katika dakika ya 90.
Licha ya kipigo hicho kikubwa, Moghreb Tetouan ingeweza kusonga mbele
kama Al Hilal ingepoteza mechi yake ugenini kwa Smouha nchini Misri.
Kufikia mapumziko, Moghreb ilikuwa bado ina nafasi kwa sababu Al Hilal
ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 baada ya Smouha kupata bao la kuongoza
lililofungwa na Amr El Menoufy katika dakika ya 21.
Lakini Hilal ilipigana kiume na kusawazisha katika dakika ya 73 kwa
bao la Nasreldin Al Shigail kuivusha katika nne bora. Wakati Kundi A
likimaliza kwa mchuano mkali, Kundi B lilimaliza kazi yake hata kabla ya
kumalizika kwa mechi zao za Ijumaa, ambako USM Alger ilipoteza mechi
yake ya kwanza.
0 comments:
Post a Comment