Image
Image

Tuchukue tahadhari kwenye hizi mvua za vuli.

Mamlaka ya Hali ya Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kuanza hivi karibuni kwa mvua kubwa za vuli ambazo zinatazamiwa kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kwamba huenda zikasababisha maafa kwa baadhi ya mikoa.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema mvua hizo  kubwa zitakuwa na athari mbalimbali ukiwamo mlipuko wa magonjwa na uharibifu wa miundombinu.

Mamlaka hiyo inaeleza kwamba mvua hizo zinatarajia kuanza wiki ya kwanza ya mwezi huo na kuendelea hadi Novemba mwaka huu, ingawa baadhi ya maeneo yatakuwa na mvua za wastani.

Awali zilitolewa taarifa kwamba zingenyesha mvua za el-nino, lakini taarifa za utabiri za hivi karibuni zinabainisha kwamba hatari hiyo haipo tena.

Taarifa za mamlaka hiyo kuhusiana na kuwapo kwa mvua kubwa za vuli zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa ikiwamo kuchukua tahadhari mapema. 

Hata hivyo, kutokana na sababu zisizoeleweka, baadhi ya wananchi wamekuwa wabishi na wakipuuza tahadhari inayotolewa na mamlaka hiyo kuhusiana na uwezekano wa kutokea kwa maafa.

Hii sio mara ya kwanza kwa mamlaka hiyo kutoa tahadhari za namna hiyo, lakini tatizo kubwa kwa baadhi ya wananchi viongozi kwa ujumla wake wanakuwa wagumu kuchukua tahadhari zinapotolewa taarifa za uwezekano wa kutokea kwa majanga.

Kutokana na kutotiliwa maanani kwa tahadhari hizo, kila mara wananchi wamekuwa wakipatwa na maafa na baada ya hapo kutolewa matamko balimbali na viongozi, lakini baadaye utekelezaji wa maagizo hushindikana.

Mvua kubwa zimekuwa zikisababisha mafuriko na kuwaathiri wananchi kadhaa hususani wanaoishi katika maeneo hatarishi kwa kubomoa nyumba zao na kukosa makazi huku wengine wakipoteza maisha.

Katika miaka ya hivi karibuni, wananchi katika maeneo kadhaa nchini wamejikuta wakikosa makazi na wengine kupoteza maisha hususani wakati wa mvua za masika.

Kwaka 2011 kwa mfano, mvua kubwa za masika zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 40 jijini Dar es Salaam na wengine takribani 500 walikosa makazi, baada ya nyumba zao kujaa maji na kulazimika kuhifadhiwa na serikali katika kambi za muda zilizowekwa kwenye shule.

Wengi wao ni wale waliokaidi kuhama katika makazi yao yaliyoko kwenye mabonde, licha ya TMA na mamlaka nyingine za serikali kutoa tahadhari na kuwataka wahame.

Pamoja na serikali kuwahifadhi na kuwapatia misaada ya kibinadamu, pia iliwapatia viwanja katika maeneo ya Mabwepande, wilayani Kinondoni kwa ajili ya makazi mapya, zipo taarifa kuwa baadhi ya waliopewa viwanja hivyo, waliamua kurejea katika maeneo ya mabondeni bila sababu za msingi.

Aidha, wapo baadhi ya wakazi katika Wilaya ya Ilala, ambao wanaendelea kukaidi kuhama wakidai kuwa wanasubiri kulipwa fidia licha ya halmashauri kuwaamuru waondoke kutokana na eneo lao kutokuwa salama zinaponyesha mvua kubwa.

Mvua za masika za mwaka huu pia zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 12 jijini Dar es Salaam na wengine kulazimika kuhama maeneo yao kutokana na nyumba zao kujaa maji.

Kutokana na ukaidi huo, serikali hususani mkoani Dar es Salaam imeshasema kuwa haitatoa msaada tena kwa waliokaidi kuhama ikiwa maeneo yao yatakumbwa tena na mafuriko ya mvua.

Tunawashauri wakazi wa maeneo yote hatarishi nchini kuitikia tahadhari iliyotolewa na TMA kwa kuhama maeneo yao ili kuepukana na uwezekano wa kupoteza mali zao, kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu  na hata vifo.

Tunazikumbusha pia mamlaka kadhaa zikiwamo halmashauri kuboresha miundombinu kama barabara na madaraja kabla ya mvua hizo kuanza.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment