VIONGOZI wakuu wa nchi na serikali zaidi ya 150 kutoka mataifa
mbalimbali duniani (leo) Septemba 25,watapitisha ajenda na malengo mapya
ya maendeleo endelevu (Ajenda 2030) kuchukua nafasi ya Malengo ya
Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayomaliza muda wake mwishoni mwa mwaka
huu.
Katika mkutano huu wa kihistoria unaofanyika miaka kumi na tano tangu
MDGs zilipopitishwa, utatanguliwa na hotuba ya Baba Mtakatifu Francis.
Baada ya kupitisha ajenda 2030 na ambayo imejikita zaidi katika
kuutokomeza umasikini na ulinzi wa mazingira pasipo kumwacha yeyote
nyuma,viongozi hao kila mmoja wao atapata fursa ya kuelezea matarajio ya
serikali yake katika utekelezaji wa ajenda hiyo yenye malengo 17.
Tayari viongozi hao wamekwisha wasili Jijini New York , yaliko Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa. Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
unaongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Siku moja kabla ya kupitishwa kwa ajenda 2030, baadhi ya viongozi
ambao wameambatana na Rais Kikwete walishiriki katika mijadala
mbalimbali ambayo maudhui yake yanashabihiana na ajenda nzima ya
Maendeleo Endelevu.
Akiwakilisha ujumbe wa Tanzania katika mikutano hiyo ya pembezoni,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi
Liberata Mulamula, alishiriki katika majadiliano kuhusu mabadiliko ya
tabia nchi na uendelevu wa usalama wa chakula, lishe na afya.
Balozi Mulamula alikuwa kati ya wanajopo watano katika majadiliano
hayo ambayo aliandaliwa na Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na
Maendeleo ya Ujerumani na Mashirika ya Kimataifa.
0 comments:
Post a Comment