KAULI za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Dk Mohamed
Gharib Bilal pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein za
kuwataka Watanzania kuendeleza amani, upendo na mshikamano, katika
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba 25 mwaka huu, hazina
budi kutekelezwa kwa vitendo.
Viongozi hawa wakuu wa kitaifa waliitoa kauli hizi wakati wa hotuba
zao kwenye sherehe ya Sikukuu ya Idd el Haj jana. Dk Bilal alikuwa mgeni
rasmi katika sherehe hizo zilizofanyika kitaifa katika Manispaa ya
Musoma mkoani Mara, huku Dk Shein akiwa mgeni rasmi katika Ukumbi wa
Chuo cha Amali Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dk Bilal alisema, Watanzania hawapaswi kuichezea amani iliyopo kwa
namna yoyote ile, badala yake akawaomba kuilinda na kuiendeleza, huku
akisisitiza kuwa, maendeleo ya nchi yoyote duniani yanategemea amani.
Aliongeza pia kwamba mshikamano na upendo sanjari na haki, ni msingi
wa maendeleo na kuwaomba viongozi wa dini kuyapa vipaumbele katika
misikiti na makanisa yote nchini. Dk Bilal pia akawakumbusha viongozi wa
dini kuwa wana wajibu wa kuisaidia Serikali, iwapo watahubiri amani
katika makanisa na misikiti kwani haitatumia gharama nyingi kujenga
magereza, vituo vya polisi na badala yake itatumia gharama hizo
kuzielekeza katika shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.
Aidha aliwataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wa madhehebu yao,
ifikapo Oktoba 25 mwaka huu wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua
viongozi waadilifu watakaoletea maendeleo wananchi na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa, kila Mtanzania ana wajibu wa kufuata sheria taratibu
na kanuni za nchi hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu kwani
matukio mengi ya umwagaji damu hutokea pindi kunapokosekana amani na
haki, huku akiwaomba wanasiasa kufanya kampeni zao kwa mujibu wa sheria
za nchi na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa Tanzania Bara na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Wakati Dk Bilal akisema hayo, Dk Shein alisisitiza kwamba Serikaili
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kukabiliana na wale wote
watakaofanya vitendo vitakavyoashiria kutaka kuvunja amani ya nchi
wakati wote hasa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu,
wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Dk Shein aliwahakikishia wananchi kuwa hakuna atakayeonewa au
kudhulumiwa kwa njia yoyote ile, lakini ni vizuri wajue kuwa Serikali
ina wajibu wa kikatiba wa kuwalinda watu wote na mali zao.
Tunasema kauli hizo zichukuliwe kwa uzito mkubwa kwani amani
tuliyonayo imewezekana kwa vile, viongozi wote waliotangulia na waliopo
madarakani wameweka misingi iliyo bora na Watanzania wana wajibu wa
kuilinda pia.
Tunaamini kwamba kila Mtanzania atatafakari kauli hizi kwa vitendo,
kwani kama alivyosema Rais Shein, Serikali haijalala na haitalala, la
msingi, ni kila mmoja kuzingatia sheria na kuachana na vitendo
vinavyoashiria uvunjifu wa amani ambapo yeyote anaweza kujikuta mikononi
mwa dola badala ya kwenda kupiga kura kwa amani hapo Oktoba 25 ili
kumchagua kiongozi amtakaye.
0 comments:
Post a Comment