Katika toleo letu la jana la gazeti hili, kulikuwa na habari
iliyozungumzia kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya, inaongoza
kwa kuuza dawa na vipodozi haramu.
Operesheni zilizofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania
(TFDA) katika maeneo mbalimbali nchini hivi karibuni, ndiyo iliyobaini
kuwa mikoa hiyo ni vinara katika biashara hiyo.
TFDA imeeleza kuwa kuna majalada 19 ya kesi zinazohusiana na biashara hiyo yamefunguliwa sehemu mbalimbali nchini.
Dar es Salaam ndiyo inaongoza kutokana na kufunguliwa kwa majalada
10, Mbeya sita, Arusha mawili na Mwanza jalada moja lililofunguliwa.
TFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, waliendesha operesheni
katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Mara, Kilimanjaro, Arusha,
Mwanza, Mbeya na Dodoma.
Tunashauri juhudi hizi za TFDA ziungwe mkono na serikali na wananchi wote kutokana na athari mbaya za matumizi ya vipodozi feki.
Tatizo la vipodozi feki ni kubwa na hasa katika wakati huu wa
utandawazi na biashara huria na hivyo kutoa mwanya kwa uingizaji holela
wa dawa hizo.
Wateja wengi wa bidhaa hizo wamekuwa wakidanganyika kutokana na
ukweli kuwa watengenezaji wa vipodozi hivyo feki mara nyingi hutumia
majina ya kampuni kubwa.
Vipodozi hivi feki mara nyingi vimekuwa vikiuzwa kwenye maduka ya dawa, yale ya kawaida na maduka makubwa (supermarkets).
Kuna aina nyingi za vipodozi feki kama vile vya kutengeneza nywele, kuchubua mwili na hata sabuni mbalimbali za kuogea.
Mifano ya madhara yanayotokana na matumizi ya vipodozi feki ni
pamoja na ugonjwa wa saratani, mwili kuota vipele, kuwashwa na macho
kuvimba.
Jambo la kusikitisha ni kuwa wananchi walio wengi hawana uelewa wa
kutosha jinsi vipodozi feki vinavyosambazwa kwenye maduka mbalimbali
nchini.
Tunashauri TFDA na hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
kuanzisha elimu maalum kwa kutumia njia mbalimbali kusaidia wananchi
kupata uelewa jinsi ya kung’amua vipodozi feki.
Wananchi wa kawaida ni wadau muhimu katika mapambano haya ya
kukabiliana na tatizo la uingizaji wa vipodozi feki kwani kadiri
wananchi watakavyopata elimu hiyo, ndivyo itakavyorahisisha hata
operesheni za TFDA.
Tunaamini kuwa wananchi ni sehemu muhimu kwani wamegawanyika kwenye
makundi mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara ambao husafiri kwenda nchi
mbalimbali duniani kusaka bidhaa hizo.
Kwa kutoa elimu kwa wananchi hawa, ina maana kwamba hata serikali
kwa upande mmoja, itapunguza uingizaji wa dawa hizo kwani hata waagizaji
watakuwa na uelewa wa vipodozi feki.
Tunatoa wito kwa vyombo husika kuongeza nguvu katika mapambano
dhidi ya tatizo hili ili vipodozi feki visiendelee kuleta madhara kwa
jamii ya Watanzania hii ikienda sambamba na elimu ya kutosha kwa
wananchi kuhusiana na tatizo hili.
0 comments:
Post a Comment